• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:05 PM
Vilio vyazuka kuhusu masharti mapya ya Mpango wa Elimu Finland

Vilio vyazuka kuhusu masharti mapya ya Mpango wa Elimu Finland

TITUS OMINDE na BARNABAS BII

MZOZO kuhusu mpango tata wa masomo katika mataifa ya Finland na Canada ulioanzishwa na serikali ya Kaunti ya Uasin Gishu umeshika mkondo mpya.

Hii ni baada ya serikali ya kaunti hiyo kutoa masharti mapya kwa wanafunzi wanaotaka kuenda nchi hizo za kigeni kwa masomo ya juu.

Kati ya masharti hayo ni kulipa karo ya masomo ya mwaka mzima wa masomo tofauti na hitaji la awali ambapo karo ilihitajika kulipwa kwa kila muhula. Aidha, wanafunzi walihitajka kulipa Sh610,000 nyingine za kugharimia nauli na mahitaji mengine ya kimsingi.

Serikali ya Uasin Gishu pia imetia saini Mkataba wa Maelewano (MoU) na taasisi mbalimbali kuhusu jinsi zitakavyotoa hifadhi kwa wanafunzi na kuwapa leseni zitakazowawezesha kusoma na kufanya kazi ili kupata pesa za kujikimu.

Masharti haya mapya yamewagawanya zaidi ya wanafunzi 300 ambao sasa wanataka warejeshewe pesa zao baada ya sakata kukumba mpango huo wa masomo ng’ambo.

Hata hivyo, wanafunzi 22 ambao wametimiza masharti hayo mapya waliondoka nchini wikendi iliyopita kujiunga na vyuo mbalimbali kwa masomo ya juu nchini Finland na Canada.

Lakini wanafunzi wengi waliosalia wameishutumu serikali ya kaunti hiyo, wakisema kuwa maafisa wake wamekuwa wakiwafikia kibinafsi kuwajulisha kuhusu masharti hayo mapya.

Sasa baadhi yao wanataka warejeshewe pesa walizolipa kugharimia masomo yao na mahitaji mengineyo.

“Hatujafikia maelewano yoyote na serikali ya Kaunti ya Uasin Gishu. Kwa hivyo, inasikitisha kuwa viongozi wake wanapotosha umma kwamba tumekubaliana,” akasema Mercy Tarus, mmoja wa wanafunzi waathiriwa.

Wameelekeza kidole cha lawama kwa utawala wa Gavana Jonathan Bii wakisema walilipa pesa za kugharimia mpango huo baada ya serikali hiyo kuingia afisini na hivyo wanamtaka kuwajibika na kuharakisha mpango wa kuwarejeshea pesa zao.

“Hatuko tayari kusikia chochote kutoka kwa serikali ya Kaunti isipokuwa kurejeshwa kwa pesa zetu. Hatutanyamaza hadi pesa zetu zirejeshwe,” akaongeza Bi Tarus.

Wanafunzi hao wenye hasira pamoja na wazazi wameapa kufanya maandamano wiki ijayo kushinikisha warejeshewe pesa zao.
Aidha, wametishia kuchukua hatua za kisheria dhidi ya watu binafsi waliohusika na mpango huo.

“Inasikitisha kuwa juzi, polisi walitutaka kusitisha maandamano kwa sababu zisizo na mashiko. Lakini sasa tuko tayari kurejelea maandamano hadi pesa zetu zitakaporejeshwa,” akasema Kezia Kosgei, mhasiriwa mwingine katika sakata hiyo.

Wanafunzi hao walitishia kuwasilisha kesi mahakamani dhidi ya washukiwa walioshiriki katika sakata hiyo ili mahakama iwalazimu kurejesha pesa zao.

Kupitia wakili wao, Kevin Kimaru kila mlalamishi atawasilisha kesi kivyake kushikinikiza warejeshewe pesa zao.

Seneta wa Uasin Gishu Jackson Mandago na maafisa wa Kaunti, Meshack Rono, Joseph Maritim na Joshua Lelei tayari wameshtakiwa katika mahakama kuu ya Nakuru kwa njama ya kulaghai Sh1.1 bilioni kupitia mpango huo.

  • Tags

You can share this post!

Mshambulizi Judith Atieno arefusha mkataba klabuni Rayon...

‘Ex’ wa Diamond Platnumz, Hamisa Mobetto akana...

T L