• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 7:50 AM
Wafuasi wa UDA, Jubilee walimana mangumi Nyahururu

Wafuasi wa UDA, Jubilee walimana mangumi Nyahururu

NA WANDERI KAMAU

WAFUASI wa chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA) na wale wa Jubilee, Jumamosi, Desemba 30, 2023 walikabiliana vikali mjini Nyahururu, Kaunti ya Laikipia, kutokana na sera za utozaji ushuru zinazoendeshwa na serikali ya Kenya Kwanza.

Chama cha UDA kinaongozwa na Rais William Ruto.

Makabiliano hayo yalianza baada ya wafuasi wa Jubilee kuilaumu serikali ya Kenya Kwanza, wakisema inawahangaisha Wakenya kutokanana na hatua yake kuongeza ushuru inaowatoza raia.

Hata hivyo, wafuasi wa UDA waliwakabili vikali, wakishikilia kwamba hakuna serikali inayoweza kuendesha mipango yake bila kutoza raia ushuru.

Vurugu hizo zilianza wakati wafuasi wa UDA walivamia wenzao wa Jubilee, kwenye mkutano wao uliokuwa ukiendelea katika hoteli moja mjini humo.

Wafuasi wa UDA waliongozwa na diwani Irene Wachuka wa wadi ya Igwamiti.

Kikao cha Jubilee kilikuwa kikiongozwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Bw Jeremiah Kioni.

Akiwahutubia wanahabari muda mfupi baada ya vurugu hizo, Bi Wachuka alisema kuwa hawatamruhusu mtu yeyote kuiharibia sifa serikali wakati inafanya kila iwezalo kuboresha maisha ya Wakenya.

“Hatutamruhusu Bw Kioni kuipaka tope serikali. Kama kiongozi aliyechaguliwa na raia, ni jukumu langu kuitetea serikali yetu. Ukweli ni kuwa, hakuna serikali inayoweza kutimiza malengo yake kimaendeleo bila kutoza raia ushuru. Huu ni upotoshaji ambao hatutaruhusu kuendelea katika eneo hili,” akasema Bi Wachuka.

Bw Kioni amekuwa akiendesha ukosoaji mkali dhidi ya serikali ya Rais William Ruto kupitia vuguvugu lake la ‘Sufuria Movement’, akidai kwamba Wakenya hawawezi kumudu hata chakula kutokana na gharama ya juu ya maisha.

Juhudi za ‘Taifa Leo Dijitali’ kumfikia Bw Kioni hazikufua dafu.

 

  • Tags

You can share this post!

Hali ngumu ya maisha thamani ya shilingi ikizidi kudorora

Wanajeshi 1, 000 wa Burundi walitumwa kisiri mashariki mwa...

T L