• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:05 PM
Wanahabari wa NMG wazoa tuzo za OFAB-Kenya

Wanahabari wa NMG wazoa tuzo za OFAB-Kenya

NA RICHARD MAOSI

WANAHABARI wa kutoka Shirika la Nation Media Group (NMG) wametia fora kwenye tuzo za OFAB Media Awards 2023, katika hafla ya kipekee iliyoandaliwa jijini Nairobi wiki iliyopita. 

Brygettes Ngana, ambaye ni ripota wa kituo cha runinga cha NTV anayeripoti kutoka Nakuru alichukua nambari moja naye Sammy Waweru ambaye ni ripota anayeandikia ‘Taifa Leo’ na ‘Daily Nation’ akiibuka nambari tatu.

Wametunukiwa kutokana na mchango wao mkubwa kuripoti maswala halisia ya bioteknolojia kwenye kilimo.

Bw Waweru ni mwandishi wa makala ya kilimo ya Seeds of Gold ambayo huchapishwa  kwenye gazeti la Daily Nation kila siku ya Jumamosi. Aidha huandika makala ya Akilimali kwenye gazeti la kipekee la Kiswahili nchini Kenya Taifa Leo. Alipata tuzo hiyo baada ya kuangazia changamoto ambazo wakulima wa pamba aina ya BT Cotton hukumbana nazo mashinani, mojawapo ikiwa ni ukosefu wa mbegu za kutosha.

Jambo ambalo huwafanya kupanda mbegu wakiwa wamechelewa, hivyo basi hawawezi kuyafikia mahitaji ya soko kwa wakati unaofaa.

Ikumbukwe Kenya huagiza mbegu za pamba kutoka nchini India na hatimaye husambazwa kwa wakulima kupitia shirika la Fibre Crops Directorate.

Mwenyekiti wa OFAB Margret Karembu alitambua mchango wa wanahabari akitaja juhudi zao kuelimisha jamii kuhusu uvumbuzi na ukuaji wa bioteknolojia kuwa ni za kupigiwa mfano.

“Teknolojia ya kisasa itasaidia kukwamua nchi kiuchumi na vilevile kupiga jeki kilimo kwa kuangazia changamoto za mabadiliko ya tabianchi,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

Macho kwa Kipchoge akivizia taji la tano la Berlin Marathon

Polisi wachunguza kisa cha mwalimu kuita mwanafunzi...

T L