• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Macho kwa Kipchoge akivizia taji la tano la Berlin Marathon

Macho kwa Kipchoge akivizia taji la tano la Berlin Marathon

NA GEOFFREY ANENE

REKODI za dunia za kilomita 42 zinazoshikiliwa na Wakenya Eliud Kipchoge (saa 2:01:09) na Brigid Kosgei (2:14:04) zitakuwa hatarini kufutwa makala ya 49 ya Berlin Marathon mnamo Jumapili nchini Ujerumani.

Mabingwa watetezi Kipchoge (2:01:09) na mwanadada Tigist Assefa (2:15:37) kutoka Ethiopia wako katika orodha ya wanaopigiwa upatu kuibuka na ushindi katika mbio hizo, ambazo mashabiki nchini Kenya watapata uhondo moja kwa moja kupitia runinga ya NTV.

Kipchoge, ambaye atafikisha umri wa miaka 39 hapo Novemba 5, anaendea taji lake la tano la Berlin Marathon baada ya kuibuka mfalme 2015, 2017 na 2018 alipoweka rekodi ya dunia ya 2:01:39 kabla kuiimarisha kwa sekunde 30 mwaka jana.

Nafasi mbaya ambayo bingwa huyo mara mbili wa Olimpiki amewahi kumaliza jijini Berlin ni nambari mbili mwaka 2013 alipokuwa akianza marathon.

“Berlin kwangu ni kama nyumbani. Nia yangu kushiriki mwaka huu ni kujitayarisha vyema kwa Michezo ya Olimpiki jijini Paris mwaka 2024,” alinukuliwa na Shirikisho la Riadha Duniani.

Washindani wake wakuu ni Wakenya Amos Kipruto, Jonathan Maiyo, Eliud Kiptanui, Ronald Korir, Philemon Kiplimo, Enock Onchari, Mark Korir, Josphat Boit, Abel Kipchumba, Denis Chirchir, Justus Kangogo, Titus Kipkosgei, Dominic Nyairo na Vincent Kipkemoi.

Pia raia wa Eritrea Ghirmay Ghebreslassie na Muethiopia Andamlak Belihu ni miongoni mwa wengine watakaowinda taji hilo.

Katika kitengo cha wanawake, macho yatakuwa kwa Wakenya Sheila Chepkirui (2:17:29) na Margaret Muriuki (2:23:52) ambao wanatarajiwa kupata mtihani mkali kutoka kwa Muethiopia Assefa, Mjapani Hitomi Niiya, Delvine Meringor (Romania) na Muingereza Charlotte Purdue, kati ya wengineo.

  • Tags

You can share this post!

Man-U imeisha hakuna timu hapo, Ole Gunnar atoboka!

Wanahabari wa NMG wazoa tuzo za OFAB-Kenya

T L