• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 6:55 AM
Hatutabebwa na ‘tam tam’ za Ruto, magavana wahakikishia Raila

Hatutabebwa na ‘tam tam’ za Ruto, magavana wahakikishia Raila

Na RUSHDIE OUDIA

[email protected]

Magavana kutoka ngome ya Kinara wa Upinzani Raila Odinga wameapa kukataa kuchotwa na mapochopocho ya Rais William Ruto ili kuunga mkono serikali.

Wakuu hao wa Kaunti, wakithibitisha kwamba kweli Rais amekuwa akiwawinda ili waingie boksi yake, walisema kwamba licha ya kuandamwa huko bado watabakia waaminifu kwa kiongozi wa ODM.

“Sisi tunajijua na tuna tajriba ya kutosha kujua yule mtu aliye na nia njema na yule aliye na nia fiche,” akasema Gavana wa Kisumu Anyang Nyong’o.

Profesa Nyong’o alizungumza kwa niaba ya wakuu wa kaunti ambao walikongamana katika hoteli moja ya Kisumu kwa mkutano wa kiuchumi wa kaunti zilizo kanda ya Ziwa ambao ulihudhuriwa na Kiongozi wa Azimio Raila Odinga na Naibu Kiongozi wa ODM Wycliffe Oparanya.

Magavana waliohudhuria mkutano huo walikuwa Nyong’o (Kisumu), James Orengo (Siaya), Wilbur Ottichilo (Vihiga), Fernandes Barasa (Kakamega) na Paul Otuoma (Busia).

Wale ambao hawakuwemo ingawa walituma risala zao ni Ken Lusaka (Bungoma), George Natembeya (Trans Nzoia) na Amos Nyaribo (Nyamira).

Magavana hao walikuwa wamewasili mapema asubuhi kwa mkutano wa faragha ambao duru zinasema kwamba walijadili jinsi ya kunufaika na uchumi wa kijani na jinsi pia ya kunufaika na usafiri wa majini.

Walikaa pia na maafisa wa Kitengo cha Kuzuia na Kupambana na maradhi (CDC) kujadiliana mbinu za kuendeleza miradi ya kupambana na virusi vya Ukimwi na majanga mengine ya maradhi.

Wakati wa mkutano na wanahabari, ni Magavana Arati na Ayacko pekee waliandamana na Gavana Nyong’o huku wengine wakienda kushiriki chakula cha mchana na Bw Odinga.

Bw Barasa ambaye amekuwa akifanya kazi kwa karibu na Dkt Ruto aliondoka mapema wakati wengine wakiendelea na mkutano.

Kiongozi wa Azimio hakuzungumza na wanahabari lakini alichapisha baadaye kwenye ukurasa wake wa Twitter kwamba anakutana na magavana kwa majadiliano kuhusu masuala ya ugatuzi.

“Nimekuwa na mkutano wa maana sana na magavana wa Azimio kutoka kwa kanda ya Ziwa kuhusu kutathmini hali ya ugatuzi katika miaka 10 iliyopita. Mengi bado yanahitajika kufanywa kuhakikisha kwamba mustakabali wa ugatuzi unadhibitiwa,” akaandika.

Siku moja iliyopita kabla ya mkutano huo, Bw Odinga alimshutumu Rais Ruto kwa kunyemelea viongozi wa upinzani katika juhudi zake za kutafuta uungwaji mkubwa.

Chama chake cha ODM ndicho kilichopata pigo kubwa zaidi huku wabunge wake wakimkaidi waziwazi na kufanya kazi na serikali ya Kenya Kwanza.

Hili limefanya baadhi yao kutemwa. Wabunge hao ambao mnamo Februari walikutana na Rais katika Ikulu na sasa wametemwa kutoka ODM ni Gideon Ochanda (Bondo), Caroli Omondi (Suba Kusini), Elisha Odhiambo (Gem), Felix Odiwuor ‘Jalang’o’ (Lang’ata) na Seneta wa Kisumu Tom Ojienda.

Wengine, Esther Passaris (Nairobi) na  Mark Nyamita (Uriri) walipigwa faini kwa kwenda kinyume na msimamo wa chama na kupigia kura ya ndio Mswada tata wa Fedha 2023.

  • Tags

You can share this post!

Wanaotumia bangi Kenya wameongezeka pakubwa katika miaka...

Mume wangu na meidi wanatumiana SMS za siri

T L