• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 9:50 AM
Washukiwa wa genge linalojumuisha polisi washtakiwa kwa wizi wa mabavu

Washukiwa wa genge linalojumuisha polisi washtakiwa kwa wizi wa mabavu

NA RICHARD MUNGUTI

WAENDESHAJI bodaboda wawili wanaodaiwa kuwa wanachama wa genge la majambazi lililomjumuisha afisa wa polisi aliyeuawa kwa kupigwa mawe mkesha wa sikukuu ya Krisimasi wameshtakiwa kwa wizi wa mabavu.

Genge hilo la majambazi lilikuwa linawapora mali wakazi wa mtaa wa Kilimani mnamo Desemba 24, 2022 wananchi walipowafumania na kumuua Konstebo Ken Kavulanga Wali kwa mawe na vifaa butu.

Kavulanga alikuwa na umri wa miaka 28.

“John Kyalo Makau almaarufu Jonte na Thomas Malusi Kilonzo almaarufu Bosco waliokuwa pamoja na Kavulanga walifaulu kutoroka kwa pikipiki,” hakimu mwandamizi Mahakama ya Milimani Bi Esther Kimilu alifahamishwa jana Jumatano na kiongozi wa mashtaka Bi Anne Munyua.

Bi Munyua alieleza mahakama kwamba polisi wakitumia picha zilizonaswa na kamera za CCTV katika Kilabu cha Bently kilichoko kando ya barabara ya Muchai Drive, Kilimani walifaulu kuwatambua na kuwatia nguvuni Kyalo na Malusi mnamo Desemba 26, 2022.

Kyalo na Malusi walio na umri wa miaka 18 walizuiliwa kwa siku 10 kuhojiwa na kusaidia polisi kukamilisha uchunguzi.

Waliporudishwa kortini jana Jumatano Bi Munyua alimweleza hakimu “sasa uchunguzi umekamilishwa na polisi wameandika taarifa za mashahidi. Wawili hawa wanaweza kusomewa mashtaka.”

Bi Kimilu aliamuru washtakiwa wasomewe mashtaka yanayowakabili ya wizi wa mabavu.

“Je mnaelewa lugha gani. Kiingereza ama Kiswahili ndipo msomewe shtaka,” Bi Kimilu aliwauliza Kyalo na Malusi.

Kwa kauli moja wote walijibu: “ Kiswahili.”

John Kyalo Makau (kulia) almaarufu Jonte na Thomas Malusi Kilonzo almaarufu Bosco walioshtakiwa kwa wizi wa mabavu. PICHA | RICHARD MUNGUTI

Shtaka dhidi yao lilisema mnamo Desemba 24, 2022 wakiwa wamejihami kwa bastola katika barabara ya Muchai Drive wakishirikiana na mtu mmoja aliyeuawa (Konstebo Ken Kavulanga Wali) walimnyang’anya kimabavu Rahab Muthoni simu ya kiunga mbali ya thamani ya Sh7,000.

Kyalo na Malusi walikana shtaka na kuachiliwa kwa dhamana ya Sh500,000.

Kesi hiyo itatajwa tena Januari 18, 2023 kwa maagizo zaidi.

  • Tags

You can share this post!

KINYUA BIN KING’ORI: Viongozi washirikiane mwaka huu...

MAPISHI KIKWETU: Jinsi ya kuandaa shakshuka

T L