• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 2:33 PM
WANGARI: Kongamano kuu la mazingira lizindue viongozi usingizini

WANGARI: Kongamano kuu la mazingira lizindue viongozi usingizini

Na MARY WANGARI

MATAIFA ya dunia yaliungana mnamo Jumapili kuanza rasmi Kongamano la Awamu ya 26 la Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Hali ya Anga, almaarufu COP26, huku ripoti zikiashiria nyakati hatari zinazokabili ulimwengu.

Kongamano hilo linalofanyika jijini Glasgow, Scotland, litaendelea hadi Novemba 12, 2021, ambapo litawaleta pamoja viongozi wa ulimwengu katika juhudi za kutafuta suluhisho la kudumu dhidi ya athari hasi za mabadiliko ya hali ya anga.

Madhara yanayosababishwa na mabadiliko ya hali ya anga kama vile viwango vya joto duniani na viwango vya maji kupanda, mafuriko, maporomoko ya ardhi, hali ya anga isiyotabirika (mara joto mara baridi) tayari yameanza kujitokeza bayana duniani huku yakisababisha maafa na uharibifu wa mali.

Kinyume na hapo awali ambapo suala la mabadiliko ya hali ya anga lilikuwa likichukuliwa kama tatizo la siku za usoni, ni dhahiri sasa kwamba ni kero linalotukodolea macho wakati huu na ambalo linastahili suluhisho la dharura.

Ripoti mpya iliyotolewa na Jopokazi la Kimataifa kuhusu Mabadiliko ya Hali ya Anga inaashiria kuwa ulimwengu ungali na kibarua kigumu cha kupunguza kiasi cha gesi hatari kwenye mazingira ili kutimiza viwango salama vya joto duniani, huku muda ukizidi kuyoyoma kwa kasi.

Kulingana na wanasayansi, mataifa makuu ya dunia ikiwemo Amerika, Ufaransa, Ujerumani, Japan na mengineyo yananing’inia hatarini na huenda yakatumbukia kwenye mashaka makuu kufikia 2050 endapo mikakati ya kukomesha athari za mabadiliko ya hali ya anga haitatekelezwa kikamilifu.

Licha ya kuwasilisha hapo mbeleni mipango kuhusu jinsi yanavyokusudia kupunguza kiwango kinachozidi kupanda cha gesi hatari kutokana na maendeleo kiviwanda, mataifa makuu duniani yamefeli kutimiza malengo yaliyowekwa hivyo kuhatarisha mustakabali wa dunia, jinsi tafiti zinavyoashiria.

Iwapo mkondo huu utaendelea, viwango vya joto duniani vimekadiriwa kuongezeka hadi karibu 2.7°C kufikia mwisho wa karne hii hali ambayo kwa kweli itakuwa balaa kwa binadamu na viumbe wote katika sayari ya Dunia.

Tafiti zinaashiria kuwa serikali za mataifa zina muda wa miaka minane tu kuunda mikakati, kubuni sera na kuzitekeleza ili kuweza kupunguza viwango vya joto duniani hadi kufikia kiasi kinachohitajika.

Japo tafiti zinatabiri kuhusu nyakati za kutamusha siku za usoni, wanasayansi wanasema kuna matumaini ya kuokoa mazingira asilia kwa kutumia malighafi na kawi salama.

Wakati huu ambapo tishio la mabadiliko ya hali ya anga linajidhihirisha waziwazi ni sharti jamii ya kimataifa imaanishe katika juhudi za kuokoa maisha na miundomsingi dhidi ya athari hasi za uharibifu wa mazingira.

Kongamano la mwaka huu liwape viongozi mwamko mpya kuhusu kuimarisha kudhibiti na kukabiliana na mabadiliko ya hali ya anga yanayotishia kuangamiza ulimwengu.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Polisi watahadharishwa kuwaomba raia ‘mafuta’

Eric Omondi ashauriwa ajihusishe kikamilifu na majukumu ya...

T L