• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 7:05 PM
Wizara yatoa onyo dhidi ya matumizi ya dawa ya kuua chawa

Wizara yatoa onyo dhidi ya matumizi ya dawa ya kuua chawa

Na JACKLINE MACHARIA

WIZARA ya Afya imewaonya wahudumu wa afya wasitumie dawa aina ya Ivermeclin, ambayo inatumika kuwaua chawa, kutoa tiba ya virusi vya corona.

Waziri Msaidizi wa Afya, Rashid Aman badala yake ametoa wito kwa wahudumu hao wazingatie kanuni za wizara na maadili ya utendakazi wao kwa kutotumia dawa hiyo.

Hii ni baada ya ufichuzi wa Taifa Leo mnamo Septemba na ambao ulibaini kuwa Ivermeclin inatumika sana katika maeneo ya Nairobi, Kisumu na Mombasa kutibu corona kinyume cha sheria za afya.

“Ni vyema kwa wahudumu wetu wa afya kufuata mwongozo wa serikali katika kupambana na janga la corona ili kuzuia matatizo ya kiafya yanayotokana na matumizi ya dawa zisizoidhinishwa,” akasema Bw Aman.

Dkt Loice Ombajo, ambaye ni mtaalamu wa magonjwa ya kuambukizana katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta, alisema kuwa hakuna ushahidi wa kutosha kuwa dawa hiyo inasaidia kukabiliana na corona.

“Hakuna ushahidi wa kutosha kuwa ivermectin inatumika kutibu Covid-19 au kuonyesha kuwa inazuia virusi hivyo,” akasema Dkt Ombajo.

Mnamo Agosti 2021, Bodi ya Famasia na Sumu (PPB) ilifafanua kwamba iliidhinisha matumizi ya Ivermeclin kutibu matende wala si corona.

“Uchunguzi wa kimatibabu na ushahidi uliopo unaonyesha kuwa hakuna leseni kutoka kwa PPB wa kuruhusu ivermectin itumike katika kupambana na corona. Ni dawa ambayo ni sumu kwa binadamu kulingana na Shirika la Afya Duniani,” likasema Shirika la Kudhibiti Matumizi ya Dawa Nchini Marekani (FDA).

Pia matumizi ya Ivermectin yanaweza kusababisha mgonjwa kutapika, kuendesha, shinikizo la damu na hata kifo.

You can share this post!

Muhsin aombolezwa kama shujaa wa uanahabari, kukuza...

Dinamo anayochezea Mkenya Onsando kuwania shaba Ligi Kuu ya...