• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:50 AM
El Nino: Hofu ya wakazi wa Mukuru-Kayaba jijini Nairobi

El Nino: Hofu ya wakazi wa Mukuru-Kayaba jijini Nairobi

NA SAMMY KIMATU

WAKAZI wa mtaa wa mabanda wa Mukuru-Kayaba ambao huathiriwa na mafuriko, wamesimulia jinsi ambavyo mvua kubwa husababisha madhara na kuleta changamoto tele.

Wakazi wa mtaa huo ambao uko South B, kaunti ndogo ya Starehe na mitaa mingine, wametangaziwa maeneo ambayo serikali ilitambua kuwa watayatumia kama sehemu za kukimbilia usalama wao endapo mvua ya El Nino iliyotabiriwa na idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa itanyesha kuanzia Oktoba 2023.

Mwenyekiti wa Kike katika eneo la Crescent aliye kadhalika mdau wa afya mtaani, Bi Jane Mbula, ameambia Taifa Leo kwamba watu watapiga kambi katika Masjid Qubaa na wengine katika kanisa la AIC Mukuru.

Mdau wa afya mtaani, Bi Jane Mbula akihojiwa na mwanahabari wa shirika la NMG. PICHA | SAMMY KIMATU

“Maabadi hayo mawili yatatumika kama ni maeneo ya waathiriwa kupiga kambi wakati wa El-Nino,” Bi Mbula akasema.

Bi Mbula amesema hayo Jumatano wakati wanahabari wa shirika la Nation Media Group (NMG) linalomiliki vitengo vya Taifa Leo, kituo cha runinga cha NTV Kenya, gazeti la Daily Nation pamoja na majukwaa ya kidijitali wamefika mtaani Mukuru-Kayaba kujionea utayarifu wa kukabiliana na majanga, likiwemo la mvua kubwa.

Mkazi wa Mukuru-Kayaba Bi Nuriah Ali, ambaye ni mama wa watoto wawili, alipoteza jirani yake kwenye mafuriko ya mwaka 1998.

“Kando na mafuriko, familia nyingi huathirika na magonjwa yanayotokana na maji machafu ikiwemo ugonjwa wa tumbo, kuhara, kutapika na hata malaria,” Bi Nuriah akasema.

Ameongeza kwamba serikali kupitia kwa wahudumu wa afya ya jamii na viongozi wa Nyumba Kumi huwa mstari wa mbele kutembea nyumba kwa nyumba kuhamasisha wakazi na pia kuwapeleka hospitalini walioathiriwa.

Waliozungumza wamesema kuwa kutokana na changamoto za mapato, wengi wao hawawezi kuhama kugharimia kodi za nyumba zilizojengwa kwa mawe wakisema kodi yake iko juu.

Badala yake hufunga vitu muhimu kama vile stakabadhi muhimu na wakati mwingine kuzibeba na kuziweka pahala salama kwa marafiki na wasamaria wema hadi maji ya mvua yatakapopungua.

“Tukiondoa vitu muhimu ndani ya nyumba, tunaondoka na kuenda katika maeneo salama kwa majirani wetu kisha tunarudi maji yakiisha. Tunapiga deki kuondoa matope yaliyoachwa na maji kisha tunaendelea na maisha kama kawaida,” Bi Gloria Charles, mkazi wa Kambi Moto amesema.

Vilevile, wamesimulia kwamba kutokana na ugumu wa maisha unaochangiwa na uchumi mbaya na ukosefu wa ajira, hawawezi kumudu kulipa kodi ya nyumba za mawe wakisema mapato yao ni duni.

Kodi ya nyumba ya mabati ya chumba kimoja ni Sh3,000 huku kodi ya nyumba iliyojengwa kwa mawe na ya chumba kimoja ikiwa kati ya Sh5,000 na Sh8,000 kwa mwezi kutegemea ukubwa wake.

  • Tags

You can share this post!

Tineja mshukiwa wa mauaji ya Eric Maigo kuzuiliwa kwa siku...

Kipa Annette Kundu aendelea kusherehekea ushindi wa Kenya...

T L