• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Madai wazazi wengi Rabai wanathamini matanga kuliko michango ya kuwasomesha watoto

Madai wazazi wengi Rabai wanathamini matanga kuliko michango ya kuwasomesha watoto

NA ALEX KALAMA

WADAU katika sekta ya elimu eneobunge la Rabai wameanza kutafuta suluhu ya kuboresha viwango vya elimu eneo hilo baada ya kushuhudia matokeo duni kwa miaka mitatu sasa.

Wakiongozwa na shirika lisilo la kiserikali la Boresha Elimu, wadau hao wanasema Rabai imeporomoka viwango na si ile ya zamani.

Wamesikitika kwamba wanafunzi wengi eneo hilo wanakumbana na changamoto nyingi shuleni na nyumbani.

Harrison Mtsunga Tsuma, ambaye ni mwalimu aliyestaafu, amedokeza kuwa changamoto kuu ni idadi ndogo ya walimu ambao wanalazimika kuhudumia mamia ya wanafunzi darasani.

“Uhaba wa walimu umekithiri na mwalimu hawezi kuwa na ile nafasi ya kumfuata mtoto ambaye ana changamoto,” alisema Bw Tsuma.

Kijana Shem Karisa aliambia Taifa Leo kuwa jamii haijathamini elimu na badala yake imekuwa ikithamini sherehe za harusi na matanga.

“Utaona mwanafunzi akiwa katika chuo kikuu, au mtu kama anafanyiwa mchango wa kuenda chuo kikuu ama mtu anafanyiwa mchango ili aende shule ya upili, anahangaika kwa sababu watu wachache tu ndio wanaojitokeza,” akasema Bw Karisa.

Lakini katika shughuli nyingine kama ni mambo ya harusi au mazishi, Karisa alisema, watu wanajitokeza kwa wingi na kutoa michango.

“Ni jambo la kuhuzunisha sana kuona watu wetu wanathamini sherehe za harusi na matanga kuliko elimu,” alisema Bw Karisa.

Shirika la Boresha Elimu kupitia mwenyekiti wake Geofrey Tawa limebaini kuwa hali hiyo imechangiwa ni kwamba hakuna ushirikiano wa kijamii katika kufanikisha masomo ya watoto haswa kwa wale wanaotoka katika familia zisizojiweza.

“Watu katika vile vikao waligundua kwamba kuna ubinafsi, uchoyo na kutopendana katika jamii. Vile vile wakazi kadhaa walisema baadhi ya wanajamii hawathamini elimu,” Bw Tawa akasema.

Kwa upande wake naibu kamishna wa Rabai Ahmed Mahmud ameitaka jamii kukaa pamoja na wadau wengine ili kutafuta suluhu kwani anadai kuwa wanafunzi wengi wanaofanya vyema katika shule za eneo hilo ni wale wanaotoka nje ya Kaunti ya Kilifi.

“Wanafunzi ambao husoma na kupita vizuri katika hizi shule za hapa Rabai, wengi wao huwa wametoka nje ya kaunti hii ya Kilifi,” alisema Bw Mahmud.

  • Tags

You can share this post!

Wanaochapisha jumbe za ugaidi na uchochezi mtandaoni...

Wadau waambiwa utalii na usafi ni kitu kimoja

T L