• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
Wanaochapisha jumbe za ugaidi na uchochezi mtandaoni wawindwa

Wanaochapisha jumbe za ugaidi na uchochezi mtandaoni wawindwa

NA KALUME KAZUNGU

TAHARUKI imetanda miongoni mwa wasimamizi wa makundi ya mitandao ya kijamii na watumiaji wake katika Kaunti ya Lamu kufuatia tangazo la serikali kwamba itawaendea na kuwakamata kwa ugaidi na uchochezi.

Akitamatisha ziara yake kaunti ya Lamu juma hili, Mshirikishi wa Usalama Ukanda wa Pwani, Bi Rhoda Onyancha alionya wale wanaoeneza chuki kwa mitandao ya kijamii kuhusiana na utovu wa usalama na mauaji yanayoshuhudiwa Lamu kwamba chuma chao ki’ motoni.

Bi Onyancha aliweka wazi kwamba wasimamizi wa makundi ya WhatsApp, Facebook, Instagram, Twitter na wanablogi ambao wamekuwa wakieneza uvumi kuhusu magaidi na chuki mitandaoni hawatasazwa.

Aliwataka wasimamizi wa makundi ya mitandao ya kijamii kuwa tayari kubeba msalaba wa madhambi ya wanachama wao wote ambao ni wachochezi.

Bi Onyancha aliamuru maafisa wa jinai, ujasusi na polisi kuanza mara moja misako na kuwatia mbaroni wahusika wa uchochezi mitandaoni na pia wale wanoeneza picha za watu wanaouawa na magaidi Lamu, hivyo kumpa umaarufu adui.

Kati ya Juni na Septemba 2023, kaunti ya Lamu imeshuhudia uvamizi na mauaji ya zaidi ya watu 30 na nyumba zipatazo 20 na Kanisa zikiteketezwa na magaidi hao wanaoshukiwa kuwa wa kundi la Al-Shabaab lenye makao yake makuu nchini Somalia.

Vijiji vilivyoathiriwa zaidi na mashambulio hayo ni Juhudi, Salama, Widho, Mashogoni, Marafa, Ukumbi na viunga vyake, vyote vikipatikana eneobunge la Lamu Magharibi.

Katika eneobunge la Lamu Mashariki, vijiji vilivyoathiriwa na uvamizi na mauaji ya Al-Shabaab ni vile vipatikanavyo msitu wa Boni, ikiwemo Baure, Bodhei, Milimani, Mararani, Mangai, Sankuri, Sarira na viunga vyake.

Bi Onyancha alishikilia kuwa utovu wa usalama si suala la kuletewa gumzo na kejeli mitandaoni ilhali wengine wakiingiza siasa, uchochezi, chuki na migawanyiko.

“Punde nikitoka hapa, nimeamuru polisi kuanza msako mitandaoni. Wasimamizi wa makundi ya WhatsApp, Facebook na mabloga, iwe ni wa wanasiasa au vibaraka wa magaidi, tutawakamata na kuwashtaki. Yale yanayoendelea mitandaoni tumekuwa tukiyafuatilia kwa karibu na hayaridhishi kamwe. Hatutamsaza yeyote mwenye kuchochea wakazi na kuleta migawanyika kupitia maandishi yao kwa mitandao ya kijamii,” akasema Bi Onyancha.

Aliwashauri wenye mapenzi kwa mitandao ya kijamii kuhubiri amani, uwiano na utangamano wa kijamii kwenye kumbi hizo badala ya kutekeleza uhalifu, hasa uchochezi.

“Ni hatia kisheria kuchochea wananchi, iwe ni kupitia kusambaza picha, maandishi, video na mbinu yoyote ile kwenye mitandao ya kijamii. Sisi hatutawaendea wanachama wote wa makundi husika lakini tutahakikisha wasimamizi wa makundi hayo wanabeba msalaba. Chungeni,” akasema Bi Onyancha.

Pia aliwataka wanasiasa wa Lamu kujitenga na uchochezi na chuki na pia waepuka kuingilia masuala ya usalama wa eneo hilo.

“Kama walinda usalama, tumefanya makubwa hapa Lamu na tunaendelea. Tunachunguza mienendo ya kila mmoja na hivi karibuni tutaanza kamatakamata. Sitaki mwanasiasa yeyote kunifuata eti unataka mtu wako tuliyemkamata aachiliwe. Hilo sitakubali. Kweli ni watu wako lakini mhalifu ni wa serikali. Utuachie jukumu hilo na ukae mbali,” akasema Bi Onyancha.

Baadhi ya wakazi waliohojiwa na Taifa Leo kuhusu tangazo hilo walikuwa na hisia mseto.

Kamau Mwangi, mkazi wa Kibaoni, Lamu Magharibi, alisema itakuwa bora ikiwa serikali itachunguza na kuwakamata watu binafsi mitandaoni badala ya kuwasulubisha wasimamizi wa makundi ya kijamii ambao wengine hawana hatia yoyote.

“Kuwa msimamizi wa kundi la WhatsApp au Facebook haimaanishi wewe utalinda au kudhibiti yanayosambazwa hapo na wanachama. Walioko mitandaoni ni watu wazima na wana fikra tofauti. Serikali ikamate watu binafsi badala ya kulenga wasimamizi wa makundi ya kijamii,” akasema Bw Mwangi.

Hussein Omar alisema anapongeza tangazo la Bi Onyancha la kuwafuatilia watumiaji wa mitandao ya kijamii, akisema hatua hiyo itazidisha nidhamu na mpangilio kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii.

“Nakubaliana na Bi Onyancha kwamba wengi wameitumia vibaya hii mitandao ya kijamii kueneza chuki. Maadui pia husajili wengine kwenye makundi ya uhalifu. Wasiowajibika wakamatwe ili liwe funzo kwa wengine,” akasema Bw Omar.

  • Tags

You can share this post!

Mke alia akidai mume hampi haki yake chumbani

Madai wazazi wengi Rabai wanathamini matanga kuliko...

T L