• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 10:01 AM
Jinsi Tuntigi Gaming wanavyovutia vijana wanaotaka kucheza na kuvuna hela

Jinsi Tuntigi Gaming wanavyovutia vijana wanaotaka kucheza na kuvuna hela

NA MAUREEN ONGALA

VIJANA kutoka Mombasa na Kilifi wameonyesha ari ya kujiunga na Tuntigi, mchezo wa E-Sport ili kuonyesha weledi wao na kusaka pato la kujikimu maishani.

Mchezo huo unachezwa kupitia mtandao na washindi katika fainali ya ligi zote hutuzwa pesa taslimu zisizopungua Sh100,000.

Akizungumza na wanahabari baada ya fainali ya Tuntigi 32 FIFA 2023 mjini Mombasa, Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni ya Tuntigi Gaming nchini Bw Munyutu Mwangi alisema kuwa ligi za mchezo huu hufanyika ndani ya siku 28 kabla ya washindi katika timu tofauti kujumuika pamoja katika fainali.

“Tuntigi imejitokeza kuwa sekta mpya ya kutoa nafasi za ajira kwa vijana kwa sababu siku za nyuma, jamii haijakuwa ikitilia maanani michezo ya E-sport kama kitega uchumi,” akasema Bw Mwangi.

Bw Mwangi alisema kuwa licha ya kuwa sekta hiyo ya E-Sport inatoa ajira kwa vijana, pia inasaidia katika ukuaji wa uchumi nchini kwani michuano hiyo pia inahusisha mataifa ya kigeni.

Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni ya Tuntigi Gaming Bw Munyutu Mwangi akizungumza na wanahabari wakati ya fainali ya ligi ya mchezo wa Tuntigi katika ukumbi wa Nyali Cinemax jijini Mombasa. PICHA | MAUREEN ONGALA

Alisema kuwa kuna umuhimu wa serikali za kaunti kuboresha na kuichunga sekta hiyo ya E-Sport.

“Sekta ya E-sport ni mpya sana na ni lazima tuichunge na tujadiliane pamoja kuona jinsi tukavyoimarisha sekta hii kwa manufaa ya mamilioni ya vijana wetu ambao hawana ajira. Kila mwaka, maelefu ya vijana wanafuzu kutoka vyuo vikuu mbalimbali nchini na kuanza kutafuta ajira ambayo haitoshi kwa sababu nafasi za kazi ambazo zinapatikana ni chache ikilinganishwa na idadi ya vijana,” akasema.

Bw Mwangi alisema kuna umuhimu pia wa vijana na jamii kuhamasishwa kuhusu sekta hii mpya ya E-Sport ikiwemo uwezo wa wachezaji kucheza na kupata nafasi ya kujulikana ulimwenguni.

“Jambo la muhimu hata tutakopokuwa tunafanya hamasa zetu hata vijijini ni kwa vijana kuona kuwa wanaweza kupata pesa baada ya kila ligi hata bila ya kuhusika katika ligi,” akasema.

Alitoa wito kwa washikadau wanaojihusisha na maswala ya vijana nchini kujitokeza na kuinua sekta ya E-Sport.

Bw Mwangi alisema kuwa watashirikiana na wazazi kuona kuwa wanalinda watoto kutoka na hathari za kutumia mitandao na pia kutoa mwelekeo mwafaka kwa wale ambao wana nia ya kuanza kujifunza E-Sport.

Afisa huyo mkuu alisema kuwa licha na kuwapa vijana hao pesa taslimu, watapata nafasi ya kujiunga na klabu katika nchi tofauti ulimwenguni na pia kupata wafadhili watakaowainua kuwa bora na pia mabalozi wa mchezo huo kuwapiga jeki.

Mchezaji mmoja, Bw Simon Munywa kutoka Kaunti ya Mombasa alisema kuwa wakati umefika wa vijana kutafuta njia mbadala za kupata kipato kufuatia ukosefu wa ajira na hali ngumu ya maisha inayozidi kushuhudiwa nchini.

“Wakati umepita wa kusema kuwa E-Sport ni ya watu ambao wamekosa kazi ya kufanya. Hii ni kwa sababu imejitokeza kuwa njia mojawapo ya kutoa ajira kwa vijana,” akasema Bw Munywa.

Alisema idadi kubwa ya vijana katika Kaunti ya Nairobi walianza kujihusisha na E-Sport na kutoa wachezaji wengi ikilinganishwa na kaunti nyingine nchini zikiwemo za eneo la Pwani na kwa sasa wanavuna.

Kulingana na Bw Munywa, kuwepo na ukumbi wa vijana kuendeleza E-Sport katika Kaunti ya Mombasa kutawasaidia wao kuona umuhimu wa kujihusisha na ligi zinazoendelea na kuwa na maisha bora siku za usoni.

“Vijana katika Kaunti ya Mombasa wamekuwa wakijihusisha na E-Sport ili kujifurahisha na kusukuma muda tu lakini sasa watauchukulia kwa uzito kwa sababu watapata pesa,” akasema.

Alitoa wito kwa vijana kufanya mazoezi kila mara ili kuwa washindi katika michezo hiyo.

Bw Munywa alitoa mfano wake na kusema kuwa amecheza E-Sport kwa zaidi ya miaka tisa.

Mwanzoni alikuwa anapoteza michezo mingi lakini kadri muda ulivyosonga ndivyo alivyopata uzoefu na kujua mbinu za kucheza na kushindwa.

Alisema mara ya kwanza alipata pingamizi kutoka kwa wazazi wake ambao walihofia kuwa angeathirika kwa kutumia mtandao lakini wanamuunga mkono baada ya kuona kuwa michezo ilikuwa inamjenga.

“Wazazi wangu walinifuatilia kwa ukaribu na walipoona manufaa yake, wamenishikilia mkono hadi sasa na wakati mwingine hunipa pesa za kujisajili katika ligi,” akasema.

Kwa upande wake Bw Samwel Muthui, 22, ambaye ni mwanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Technical University of Mombasa (TUM), amewataka wazazi kuwapa motisha watoto wao kujihusisha na E-Sport ili kuwalinda wasijihusishe na uhalifu.

Alisema kuwa alianza kucheza alipongia chuo kikuu na kisha akaendeleza ujuzi wake kwa kujihusisha kwa mashindano mbalimbali.

“E-Sport ni silaha ya kuwalinda vijana sasa kutokana na uhalifu na matumizi ya mihadarati kwa sababu wengi hujihusisha na uovu kwa sababu ya kukosa jambo la msingi la kuwajenga maishani,” akasema.

Katika fainali hiyo, vijana kutoka Kaunti ya Kilifi walipambana na wenzao kutoka Mombasa.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Wazee wampongeza Uhuru kwa kusema ‘Ruto ni prezzo...

MCA wa Kayafungo awahimiza wakazi kuyahifadhi mazingira

T L