• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 2:31 PM
Mjane asimulia jinsi Al-Shabaab walivyofanya maisha yake kufunikwa na wingu jeusi

Mjane asimulia jinsi Al-Shabaab walivyofanya maisha yake kufunikwa na wingu jeusi

NA KALUME KAZUNGU

KWA mama Joyce Wanjiru,39, maisha kwake yanaendelea kufunikwa na doa jeusi tangu alipompoteza mumewe, John Murimi kupitia shambulio la Al-Shabaab mnamo Januari 2, 2022.

Bw Murimi alikuwa miongoni mwa watu sita waliochinjwa na wengine wakateketezwa ndani ya nyumba zao kwenye eneo la kibiashara la Widho katika Kaunti ya Lamu magaidi wa Al-Shabaab walipowavamia usiku.

Bi Wanjiru ambaye anatoka kijiji cha Salama, anasema mumewe alikuwa akiendeleza biashara yake mjini Widho wakati alipokumbwa na mauti yake.

Magaidi walimchinja Bw Murimi na kisha kumteketeza ndani ya nyumba yake ya kibiashara.

Agosti 21, 2023, magaidi walirudi tena na kuvamia boma la Bi Murimi lililoko kijijini Salama na kuliteketeza, ambapo mali ya thamani kubwa iliharibika na kumwacha mjane huyo hohe hahe.

Ni siku hiyo ambapo pia magaidi wa Al-Shabaab walichoma nyumba nane na kanisa la Redeemed Gospel Church kijijini Salama, Lamu Magharibi kabla ya kufululiza hadi eneo la Lango La Simba, kwenye barabara kuu ya Lamu-Witu-Garsen, ambapo waliua watu wawili, akiwemo dereva wa lori na msaidizi wake asubuhi iliyofuatia.

Katika mahojiano na Taifa Jumapili bomani kwake kijijini Salama Ijumaa, Bi Wanjiru alieleza jinsi maisha yalivyombadilikia ghafla na kumgeuza kuwa omba omba.

Mama huyo wa watoto watano hana pa kuishi.

Isitoshe, nguo zake na za watoto wake zote ziliteketezwa ndani ya nyumba yao nao kuku na mbuzi aliokuwa akifuga wakiibwa na magaidi hao.

Mjane Joyce Wanjiru,39, ambaye alimpoteza mumewe John Murimi. PICHA | KALUME KAZUNGU

Bi Wanjiru aliiomba serikali na wahisani kumsaidia kwani maisha yanaendelea kumuia magumu kila kukicha.

“Mimi ni mama wa watoto watano. Mzee wangu aliuawa na hao Al-Shabaab Januari, 2022. Tangu hapo nimekuwa nikitegemea msaada kutoka kwa majirani na kanisa. Kutokana na misaada ambayo nimekuwa nikipokea, niliweza kujiinua tena, japo kwa kiasi. Magaidi walirudi tena hapa usiku wa Agosti 21 na kuchoma kila kitu, ikiwemo nyumba ya familia. Kwa sasa sina mbele wala nyuma. Naomba usaidizi,” akasema Bi Wanjiru.

Kifungua mimba wa mjane huyo yuko kidato cha nne, akitarajia kukalia mtihani wake wa kitaifa (KCSE) mwaka huu.

Wa pili yuko darasa la sita, wa tatu yuko Gredi ya 5, wa nne akiwa shule ya chekechea ilhali mwingine akiwa bado hajafikisha umri wa kwenda shule.

“Hawa watoto wote unaowaona wanapitia shida nyingi. Nguo zote zilichomwa na magaidi. Mali yetu ikaibwa, nyumba na vyote vilivyokuwemo vikachomwa. Nasumbuka kutafuta karo. Sina kazi yoyote na ni mjane. Wahisani wajitokeze kunisaidia,” akasema Bi Wanjiru.

Baadhi ya wakazi waliozungumza na Taifa Jumapili kwenye vijiji vilivyoathiriwa na mashambulio ya kigaidi mwaka huu kaunti ya Lamu waliisisitizia serikali kuzidisha doria za walinda usalama maeneo yao ili waweze kurudi vijijini mwao kutekeleza shughuli za kilimo na maendeleo mengine.

Tangu Juni 2023, zaidi ya familia 200 zimekuwa zikilala kwenye kambi ya wakimbizi ya shule ya msingi ya Juhudi usiku na kurudi makwao mchana.

Bi Ruth Njeri Muhia, mama wa watoto sita, alisema tangu jirani yake, Lucas Mwang’ombe, alipochomwa ndani ya nyumba yake eneo la Salama Block 17 mnamo Julai 12 mwaka huu, hajathubutu kulala nyumbani kwake kwa kuhofia kulengwa na magaidi.

“Hatuwezi kukaa tena majumbani mwetu kutunza haya mashamba. Kama uonavyo yamesheheni magugu ilhali mazao yakiharibika kwa kukosa wa kuyatunza. Kila usiku unapoingia mimi hulala kichakani. Nahofia kulengwa na kuuawa kwa kuchomwa ndani ya nyumba yangu sawa na vile ilivyomfanyikia jirani yangu Lucas Mwang’ombe. Serikali iangalie suala hili,” akasem Bi Muhia.

Bw Shadrack Njuguna, ambaye ni katibu wa kamati inayosimamia maslahi ya kambi ya wakimbizi ya shule ya msingi ya Juhudi. PICHA | KALUME KAZUNGU

Shadrack Njuguna, ambaye ni katibu wa kamati inayosimamia maslahi ya kambi ya wakimbizi ya shule ya msingi ya Juhudi, alisema furaha yake ni kuona hali shwari imerejea vijijini ili maisha ya kawaida yarejee.

Vijiji ambavyo kila mara vimeshuhudia uvamizi wa Al-Shabaab na kuacha makumi ya nyumba zikiteketezwa na watu kuuawa ni Juhudi, Salama, Widho, Marafa, Mashogoni na viungani mwake.

Bw Njuguna alisema suluhu ya kipekee itakayosaidia kurudisha imani ya wakazi kurudi vijijini kuendeleza shughuli zao za kawaida ni kambi za walinda usalama zijengwe maeneo yaliyoathiriwa.

“Twashukuru serikali kuzidisha doria za walinda usalama maeneo haya. La ziada tunalohitaji ni kuona kambi za jeshi (KDF) na polisi zimejengwa vijijini mwetu. Tukipata kambi eneo kama vile Salama, Juhudi na Marafa ninaamini hizi njia wanazotumia hawa magaidi kufikia vijiji vyetu kutekeleza mashambulio zitakuwa zimezibwa, hivyo wakazi kuishi raha mustarehe,” akasema Bw Njuguna.

Wakati wa ziara yake kaunti ya Lamu kutahmini hali ya usalama eneo hilo mwezi jana, Waziri wa Ulinzi Aden Duale aliahidi kushirikiana na mwenzake wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki na kuhakikisha kambi ya walinda usalama inajengwa sehemu zilizoathiriwa na mashambulio ya Al-Shabaab Lamu.

Hatua hiyo hata hivyo bado haijachukuliwa wakazi wakiisihi serikali kutimiza ahadi hiyo.

Kwa upande wake, Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Louis Rono alishikilia kuwa usalama umedhibitiwa vilivyo kote Lamu na kuwataka wenyeji, wageni, watalii na wawekezaji kuja eneo hilo.

“Hapa Lamu ni amani tupu. Tumefanya juhudi zote kuona kwamba usalama unaimarishwa. Ningeomba hata wawekezaji waje kuwekeza viwanda na miradi mingine hapa wakijua fika kwamba serikali inawalinda,” akasema Bw Rono.

  • Tags

You can share this post!

Siri ya familia ya Kenyatta yafichuliwa

BAHARI YA MAPENZI: Ndoa huyumba pale mume na mke wote ni...

T L