• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 8:55 PM
Cynthia Wanjala apigwa breki katika awamu ya robo-fainali ya tenisi ya J30 Nairobi

Cynthia Wanjala apigwa breki katika awamu ya robo-fainali ya tenisi ya J30 Nairobi

Na GEOFFREY ANENE

MREMBO Cynthia Wanjala Cheruto, ambaye ni Mkenya pekee aliyekuwa amesalia kwenye kitengo cha mchezaji mmoja kila upande cha mashindano ya tenisi ya chipukizi ya J30 Nairobi ugani Nairobi Club, alibanduliwa mnamo Alhamisi.

Mwanafunzi huyo wa Kidato cha Nne kutoka Shule ya Upili ya Mbagathi Road mwenye umri wa miaka 18 anayeshikilia nafasi ya 1,352 duniani, alilemewa na Mwingereza Ophelia Korpanec Davies, 13, (2,070 duniani) kwa seti mbili bila jibu za 7-6(3), 7-5 katika robo-fainali.

Mchuano huo ulidumu muda wa saa mbili na dakika 30.

Korpanec atakutana na Farah Heddar kutoka Algeria katika nusu-fainali leo Ijumaa.

Nusu-fainali nyingine itakutanisha Mtanzania Shana Martin Mao na Julia Weissenboeck kutoka Austria.

Mao alimchapa Avani Chitale kutoka India 7-6(3), 7-5. Heddar alimlima Janvi Asawa kutoka India 6-0, 6-1 naye Julia akampepeta Mzimbabwe Zahara El-zein 6-3, 7-6.

Wanjala atapata fursa ya kuwania taji la J30 Nairobi la wachezaji wawili kila upande akishirikiana na Mao baada ya kupiga Chitale/Mia Milisavljevic 6-3, 6-2.

Wanjala/Mao watamenyana na Asawa/Heddar waliobwaga Korpanec/Karina Kiss katika fainali ya wachezaji wawili kila upande. 

  • Tags

You can share this post!

Mzozo wa madiwani na SRC kutatiza shughuli muhimu

SABA SABA: Yanayojiri kutoka kona zote za nchi

T L