• Nairobi
  • Last Updated October 1st, 2023 9:40 PM
Polisi wapata viungo zaidi vya mwanamume

Polisi wapata viungo zaidi vya mwanamume

NA ALEX NJERU

POLISI katika Kaunti ya Tharaka Nithi wamepata sehemu nyingine za mwili wa mwanamume kutoka kijiji cha Giankanja anayeshukiwa kuuawa kikatili na mwanawe na kupika baadhi ya sehemu za mwili wake.

Kiuno na miguu ilipatikana Jumamosi ikielea katika maji mtaroni, mita chache kutoka nyumba ya mshukiwa.

Ijumaa, maafisa walipata sehemu za juu za mwili ndani ya gunia lililokuwa limefunikwa kwa mawe ndani ya mto Nithi.

Ndani ya nyumba ya mshukiwa walipata sufuria lililokuwa na mboga zilizopikwa, na fuvu lililoshukiwa kuwa la binadamu na linaloaminiwa kuwa la marehemu, Nevert Miriti aliyekuwa na umri wa miaka 70.

“Tumekamilisha utafutaji baada ya kupata sehemu zote za mwili katika maeneo tofauti na tunaamini kwamba fuvu la kichwa tulilopata ni la marehemu,” alisema mkuu wa polisi katika kaunti ndogo ya Muthambi Bw John Manei.

Bw Miriti alitoweka kwa siku tatu kabla ya watu wa familia na wanakijiji kuanza kumtafuta Alhamisi wiki jana na wakapata baadhi ya sehemu za mwili ndani ya mtaro lakini waliporudi baada ya kupiga ripoti kwa polisi hawakuvipata.

Polisi wanachunguza kubaini iwapo mshukiwa huyo kijana anaweza kuwa mlaji wa watu baada ya kupata mkoba uliokuwa na kitambulisho cha mwanamke kutoka Imenti Kusini kaunti jirani ya Meru.

Wakazi wanahofia kuwa huenda alikuwa akiua watu na kuwaficha ndani ya mtaro alioanza kuchimba miaka sita iliyopita.

 

  • Tags

You can share this post!

Serikali ya kaunti kutuza watunza mazingira

Polisi watwaa vifaa vya kanisa la Ezekiel Odero

T L