• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:50 AM
Turathi na vivutio vya kipekee vya Lamu

Turathi na vivutio vya kipekee vya Lamu

NA KALUME KAZUNGU

MJI wa kale wa Lamu ni miongoni mwa turathi saba za dunia nchini Kenya zinazotambuliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco).

Mbali na mji wa Kale wa Lamu, turathi nyingine ni Mbuga ya Kitaifa ya Wanyama ya Ziwa Turkana, Mbuga ya Msitu wa Mlima Kenya, Msitu Mtakatifu wa Kaya kwa Wamijikenda, Maziwa ya Bonde la Ufa, Ngome ya Fort Jesus-Mombasa, na Thimlich Ohinga katika Kaunti ya Migori.

Huku watalii wengi wa nyumbani na wa kimataifa wakizuru maeneo haya kila mara kujionea turathi hizi na kujivinjari, kuna watu ambao bado hawajafahamu fika baadhi ya mambo ambayo yana upekee, hasa kwa eneo kama Lamu.

Huku dunia ikiwa na maajabu yake saba ya asili yanayokushangaza, usishtuke kwamba Lamu ni zaidi kwani pia iko na mengi ya ajabu.

Mambo hayo ya kipekee na ya kimaajabuajabu ndiyo yaliyosukuma Unesco kuorodhesha Lamu kuwa miongoni mwa sehemu zenye turathi za asili duniani – yaani Unesco World Heritage Site.

Taifa Leo iliorodhesha baadhi ya mambo ya asili yanayoweka Lamu kwenye ramani ya maeneo yenye utajiri mkubwa wa historia.

Mambo hayo kwa miaka mingi pia yamekuwa vivutio vikuu kwa mamia ya watalii na wageni wanaozuru visiwa vya Lamu kila mwaka kujionea ufahari huo.

Mojawapo ya maajabu ya Lamu ni Makavazi na Turathi ya Mji wa Takwa unaoaminika kuwa chimbuko la jamii ya Waswahili.

Majengo makuukuu na kuta kwenye Turathi na Makavazi ya Takwa kisiwani Manda, Kaunti ya Lamu. Ni mji uliohamwa miaka zaidi ya 300 iliyopita baada ya kisima kugeuka kuwa chumvi. Ni miongoni mwa maajabu yapatikanayo Lamu na kuwa kivutio kikuu cha watalii.

Makavazi hayo yanapatikana katika kisiwa cha Manda.

Kulingana na Halmashauri ya Usimamizi wa Turathi na Makavazi nchini (NMK), mji wa Takwa, ambao pia ulitambulika kwa biashara kati ya Wareno na Waswahili, ulisambaratika zaidi ya miaka 300 iliyopita baada ya kisima cha pekee kilichokuwa kikitumika na wakazi kupata maji ya matumizi ya nyumbani kugeuka na kuanza kutoa maji ya chumvi.

Hali hiyo ilisukuma wakazi wote walioishi kwenye kijiji hicho kukikahama na kuelekea katika kisiwa jirani cha Shella kilichoko umbali wa kilomita moja kutoka Takwa.

Maajabu mengine yanayopatikana Lamu ni nyumba za zamani, ikiwemo misikiti ya jadi ambayo mingine imedumu kwa zaidi ya miaka 600.

Kwa mfano, Msikiti unaofahamika kwa Kimombo kama Pwani Friday Mosque ulioko katika kisiwa cha Lamu umedumu kwa zaidi ya miaka 600 kwa mujibu wa NMK huku ikiaminika kwamba ule wa Siyu kisiwani Pate umedumu kwa karibu miaka 700.

Misikiti hii hadi wa leo bado inashuhudia mahudhurio makubwa ya waumini wa dini ya Kiislamu wanaofika kuswali.

Msikiti mwinge wa Shella Friday Mosque, umedumu kwa karibu miaka 194.

Msikiti wa Mwenye Kombo, ulioko kisiwa cha Pate na ule wa Shalafatani kisiwani Faza pia huipa Lamu fahari kuu kwa kuwa miongoni mwa maabadi ya jadi kuwepo eneo hilo.

Ikumbukwe kuwa kama wewe ni mtalii ambaye azma yako ni kuifahamu historia ya Lamu ndani na nje, basi huna budi ila kutembelea misikiti hii ambayo imejikita kuwa vivutio mwafaka kwa historia yake.

Vivutio vingine vya kipekee vipatikanavyo Lamu ni Jumba la Ngome ya Lamu (Lamu Fort). Jumba hili pia ni kiungo muhimu kwa historia ya Lamu.

Watalii wakiwasili kujionea Jumba la Ngome ya Lamu. PICHA | KALUME KAZUNGU

Jumba la Ngome ya Lamu limedumu kwa zaidi ya miaka 200. Liwali Zahidi Ngumi aliyekuwa mtawala wa kisiwa cha Lamu kwa wakati huo alikuwa na mchango mkubwa katika kuongoza ujenzi wa jumba hilo tajika la Ngome ya Lamu.

Sehemu mojawapo ya Jumba la Ngome ya Lamu. PICHA | KALUME KAZUNGU

Jumba hilo lilijengwa kuanzia 1813 na kukamilika 1821. Jumba hilo bado lipo na linatumika. Linapatikana katika eneo la Mkunguni lililoko katikati ya mji wa kale wa Lamu.

Makaburi ya jadi ya Liwali Zahid Ngumi, mkewe na watu wengine wanoaminika kuwa watawa wa dini kama vile Mwana Hadie Famau pia hupatikana kwenye mji wa kale wa Lamu, hivyo kuupa hadhi na utajiri mkubwa wa historia.

Makaburi ya Liwali Zahid Ngumi na mkewe yaliyoko katika eneo la Langoni kisiwani Lamu. Makaburi hayo yamekuwepo kwa miaka zaidi ya 200. PICHA | KALUME KAZUNGU

Makaburi ya Zahid Ngumi na mkewe yote yanapatikana kwenye mtaa wa Langoni kisiwani Lamu.

Makaburi hayo yanaaminika kudumu kwa zaidi ya miaka 200.

Kaburi la mtawa Mwana Hadie Famau liko kwenye mtaa wa Mkomani mjini Lamu. Kaburi hilo linaaminika kudumu kwa zaidi ya miaka 400. Bi Hadie anachukuliwa kuwa ‘mwanamke mtukufu’ wa Lamu aliyekuwa na nguvu za miujiza na aliyeishi maisha ya utawa kwa kuheshimu dini.

Hadi wa leo, baadhi ya wakazi wa Lamu na wageni kutoka pande mbalimbali za nchi na dunia kwa ujumla hufika kwenye kaburi la Mwana Hadie Famau kuomba mema maishani.

Ufikapo Lamu, pia utapata fursa ya kutembelea nyumba ya msomi anayeaminika kuweka mizizi ya dini ya Kiislamu kisiwani Lamu na kusaidia ikaenea Afrika Mashariki, Bw Habib Swaleh. Nyumba hiyo ya udongo inapatikana mtaa wa Riyadha na inaaminika kudumu eneo hilo kwa zaidi ya miaka 120.

Bw Habib Swaleh ni mashuhuri hadi leo kisiwani Lamu kwani ndiye mwanzilishi wa msikiti maarufu na chuo tajika cha Mafundisho ya Dini ya Kiislamu Afrika Mashariki cha Riyadha.

Wanaotembelea nyumba ya Habib Swaleh hupata fursa ya kujifunza maisha ya utawa aliyokuwa akiishi msomi, mdini na mwanachuoni huyo kabla ya kifo chake mwaka 1935.

Ni kutokana na maajabu haya na mengine mengi ambapo NMK inaiorodhesha Lamu kuwa kaunti iliyobahatika kwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya makavazi na turathi ikilinganishwa na kaunti nyingine zilizosalia. Kenya ina jumla ya kaunti 47.

  • Tags

You can share this post!

Seahorses Aquatic Center yatawala mashindano ya kuogelea ya...

Mwanasiasa Githurai ajitia kitanzi

T L