• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 3:46 PM
Mwanasiasa Githurai ajitia kitanzi

Mwanasiasa Githurai ajitia kitanzi

NA SAMMY WAWERU

POLISI katika mtaa wa Githurai 45, Nairobi wameanzisha uchunguzi kubaini kiini cha mwanasiasa kujitia kitanzi Jumatatu, Juni 12, 2023.

Samson Kimani maarufu kama Wa Kim, anadaiwa kujirusha kutoka ghorofa ya sita katika kilabu chake, Gazani Guest House eneo la Toezz, Githurai.

Uchaguzi mkuu 2022, Bw Kimani aligombea kiti cha udiwani (MCA) wadi ya Mwiki, iliyoko katika eneobunge la Ruiru, Kiambu.

“Jumapili (Juni 11, 2023) hakuhudhuria ibada ya misa, kinyume na tunavyomjua kama muumini asiyekosa kanisani,” alisema Josphine Wanjiru, mkazi na mmoja wa washirika wa kanisa analohudhuria.

Baadhi ya walioshuhudia mkasa huo, walidai usiku wa kuamkia Jumatatu ugomvi baina yake na mmoja wa wake zake uliskika.

Umati wa watu uliokusanyika eneo ambalo mwanasiasa Samson Kimani alijitia kitanzi, Githurai, mnamo Juni 12, 2023. Picha / SAMMY WAWERU

Marehemu Kamau anasemekana kuwa bibi watatu.

“Kabla kukumbana na mauti, kulikuwepo na mzozo wa kifamilia uliojiri usiku kucha,” alisema Jared Wafula, mkazi mwingine.

Bw Kimani Agosti 9, 2022, aliwania MCA Mwiki kupitia tikiti ya Orange Democratic Movement (ODM), ambapo aliibuka wa tatu, nyuma ya mgombea wa United Democratic Alliance (UDA) na wa chama cha Jubilee.

Mwaniaji wa chama tawala cha UDA, hata hivyo, alitwaa ushindi.

“Huenda Wa Kim aliandamwa na changamoto nyingi kifedha baada ya kampeni ya uchaguzi mkuu 2022 na hakushinda kiti cha kisiasa alichomezea mate,” alisema mwenyeji aliyeomba kubana jina lake kwa sababu za kiusalama.

Waliomjua Bw Kimani, walimtaja kama kiongozi, mwanasiasa na mfanyabiashara aliyekuwa rafiki wa watu.

Bw Edwin Muturi, mmoja wa wandani wake alimuomboleza Kimani akisema amepoteza rafiki aliyempalilia kimaadili na kiuongozi.

“Kila nilipotangamana naye, alinishauri umuhimu wa kuishi na watu na kusaidiana. Hakukosa kunipa wosia; sisi vijana ndio viongozi wa kesho hivyo basi tujitume kuhudumia jamii na umma,” Bw Muturi aliambian Taifa Leo Dijitali.

Baadhi ya wanasiasa waliopoteza nyadhifa walizowania 2022, wametajwa kulemewa na msongo wa mawazo hasa baada ya kutumia maelfu na mamilioni ya pesa kufanya kampeni bila mafanikio.

Mwili wa Bw Kimani ulipelekwa katika Hifadhi ya Maiti ya Chuo Kikuu cha Kenyatta (KU), huku askari wakianzisha uchunguzi.

Gari la polisi lililopeleka katika hifadhi ya maiti ya KU mwili wa mwanasiasa Samson Kimani aliyejitia kitanzi eneo la Githurai, Juni 12, 2023. Picha / SAMMY WAWERU
  • Tags

You can share this post!

Turathi na vivutio vya kipekee vya Lamu

Jinsi ya kudumisha usafi wa ndani ya chumba chako cha kulala

T L