• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Utalii Lamu wayumbishwa na Al-Shabaab

Utalii Lamu wayumbishwa na Al-Shabaab

NA KALUME KAZUNGU

WADAU wa utalii Lamu wameeleza hofu kuwa visa vya mashambulizi ya kigaidi vinavyoendelea kushuhudiwa katika kaunti hiyo miezi ya hivi karibuni huenda vikaathiri pakubwa idadi ya watalii wanaozuru eneo hilo.

Tayari msimu wa juu wa utalii ulishaanza tangu Julai mwaka huu, wakati ambapo watalii wengi, hasa wale wa ng’ambo hutarajiwa kufurika Lamu na Pwani ya Kenya kujivinjari.

Kufikia sasa aidha, jumla ya watu wanane wameuawa na magaidi wa Al-Shabaab ilhali nyumba 11, magari na pikipiki vikiteketezwa kwa moto na magaidi hao kwenye sehemu tofauti za Lamu kati ya Juni na Agosti mwaka huu.

Tukio la hivi punde zaidi la uvamizi wa Al-Shabaab kushuhudiwa Lamu ni lile la Jumanne, Agosti 1, 2023, ambapo magaidi zaidi ya 60 wa Al-Shabaab waliokuwa wamejihami kwa silaha hatari, ikiwemo bunduki walivamia magari yaliyotumia barabara ya Lamu-Witu-Garsen katika eneo la Mwembeni, karibu na Lango la Simba na kuanza kuyafyatulia risasi.

Watu wawili miongoni mwao akiwa ni mke wa diwani wa Wadi ya Hindi, Charles Njaaga waliuawa ilhali watu zaidi ya 10, akiwemo diwani huyo wakijeruhiwa vibaya.

Magari na pikipiki pia zilichomwa kwenye shambulizi hilo la saa mbili kasorobo asubuhi.

Wakizungumza na Taifa Leo Alhamisi, wadau hao wa utalii, ikiwemo wamiliki wa hoteli, vijana wa huduma za matembezi ya watalii ufukweni na wale wa mashua za kusafirisha watalii walisema licha ya maeneo yaliyoshambuliwa na Al-Shabaab kuwa mbali na kisiwa cha Lamu ambacho ndicho ngome kuu ya watalii, picha mbaya inayojichora bado ni kwamba kaunti ya Lamu si salama.

Omar Ali ambaye ni msemaji wa vijana wa huduma kwa watalii ufukweni alisema idadi ya wageni wanaozuru eneo hilo bado ni finyu, akinyoshea kidole cha lawama mashambulizi ya kigaidi kwa kuchangia pakubwa hali hiyo.

Kulingana na Bw Ali, wao wamezoea punde msimu wa watalii ukifika wageni wengi zaidi kutoka sehemu mbalimbali za Kenya na ulimwengu waanze kuporomoka kuingia Lamu kujivinjari likizo zao.

“Tukilinganisha na miaka miwili iliyopita ambapo Lamu ilikuwa tulivu hasa msimu wa wingi wa watalii ulipoanza, tunapata kuwa wageni waliofika Agosti walikuwa wengi kinyume na mwaka huu. Ni dhahiri kwamba watalii wengi wamekatiza safari kuja Lamu baada ya kusikia kila mara vile Al-Shabaab wanavyoshambulia na kuua wakazi kwenye vijiji vya eneo hili. Wameingiwa na hofu,” akasema Bw Ali.

Swaleh Shekuwe, mmoja wa wamiliki wa hoteli kisiwani Lamu aliiomba serikali kukaza kamba katika harakati zake za kukabiliana na kumaliza kero la Al-Shabaab.

Bw Shekuwe alieleza hofu kuwa ikiwa hali itaendelea hivyo, sekta ya utalii Lamu itadidimia hata zaidi siku za usoni.

“Twatambua na kushukuru juhudi zinazofanywa na serikali kukabiliana na Al-Shabaab msituni Boni na maeneo ya mpakani mwa Kenya na Somalia. Hata hivyo twahofia ikiwa mashambulizi na mauaji yanayoshuhudiwa eneo letu yataendelea kujirudiarudia, utalii utakuwa ndoto. Ni wajibu wa serikali kuibuka na mbinu mbadala zitakazomaliza kabisa hili zogo la Al-Shabaab,” akasema Bw Shekuwe.

Kisiwa cha Lamu pekee kila mwaka hupokea zaidi ya watalii 30,000.

Said Twalib ambaye ni mhudumu wa mashua kisiwani Lamu alisema idadi ndogo ya watalii wanaozuru eneo hilo kwa sasa imeathiri pakubwa biashara yao.

“Huu msimu wa juu wa utalii huwa Baraka kwetu kwani hutuwezesha kupata wateja wengi ambao ni watalii kuwasafirisha kutoka uwanja wa ndege hadi kwenye hoteli au makazi yao mengine. Kwa sababu watalii hakuna, unaweza kukaa kwa karibu siku mbili bila mteja yetote,” akasema Bw Twalib.

Kwa upande wake aidha, Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Louis Rono aliwasihi wananchi kuondoa shaka na badala yake washirikiane na walinda usalama kwa kutoa ripoti zitakazosaidia kukabiliana na wahalifu.

Bw Rono alisema serikali inafanya kila jitihada kuona kwamba amani na utulivu unadumu Lamu.

“Serikali iko imara kumlinda mwananchi na mali. Ninaloomba ni ushirikiano kuona kwamba amani inadumishwa eneo hili. Tujitokeze kuwasema hawa wahalifu ili wakabiliwe vilivyo,” akasema Bw Rono.

Mnamo Juni 24, 2023, watu watano waliuawa ilhali nyumba sita zikiunguzwa moto na magaidi wa Al-Shabaab waliovamia vijiji vya Juhudi na Salama, Lamu Magharibi usiku.

Julai 12 mwaka huu, mwanamume kibarua wa shambani aliyetambuliwa kwa jina Lucas Mwang’ombe alichomwa ndani ya nyumba yake magaidi walipovamia vijiji vya Salama Block 17 na Widho, Lamu Magharibi majira ya saa nane unusu alfajiri.

Nyumba tano pia ziliteketezwa na magaidi hao.

Agosti 1, 2023, watu wawili waliuawa ilhali wengine 10 wakijeruhiwa magaidi wa Al-Shabaab walipovamia magari na kuanza kuyafyatulia risasi eneo la Mwembeni, kwenye barabara kuu ya Lamu-Witu-Garsen.

Matatu aina ya Toyota na pikipiki mbili zilichomwa kwenye shambulizi hilo la majira ya saa mbili kasoro dakika ishirini asubuhi.

  • Tags

You can share this post!

AAR kutoa huduma za afya katika eneo pana la Tatu City

Nyati FC pabaya katika Ligi ya NERL

T L