• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Wafichua ukatili wa genge la askari jijini

Wafichua ukatili wa genge la askari jijini

Na COLLINS OMULO

IMEFICHUKA kuna genge hatari la askari karibu 2,000 katika Kaunti ya Nairobi, ambao wamekuwa wakiwakamata na kuwahangaisha wachuuzi huku wakiwaitisha hongo kwa nguvu kabla ya kuwaachilia.

Wachuuzi wanawake wanaokamatwa na wanachama wa genge hilo huwa wanalazimishwa kushiriki nao ngono ili kuachiliwa huru.

Kulingana na simulizi za watu waliojipata mikononi mwa genge hilo, wanachama wake huwa katili na hawajali njia wanazotumia kuwaitisha wachuuzi pesa.

Kasisi Paul Wachira wa Kanisa la Anglikana (ACK) ni mmoja wa waathiriwa wa dhuluma na unyama wa genge hilo.

Akielezea masaibu yake mbele ya Kamati ya Masuala ya Haki na Sheria ya Bunge la Kaunti ya Nairobi, Bw Wachira aliwashtua wengi aliporejelea yale aliyopitia mikononi mwa genge hilo, lilipomkamata mara tu alipowasili mahali anapofanyia biashara zake.

Pamoja na mkewe, Bw Wachira huwa anafanya biashara ya kufuga kuku, ijapokuwa ndiye huwa anasafirisha bidhaa tofauti kama vile mayai kwa wateja.

“Nilikuwa tu nimemaliza kupeleka kreti ya mwisho ya mayai kwa mkahawa nilikokuwa nimeitishwa. Niliporejea, nilimkuta askari mmoja wa kaunti akiwa ameketi katika kiti cha dereva katika gari langu,” akasema kwenye kikao na kamati hiyo.

Akaeleza: “Askari huyo aliniambia kutoelekea popote, lakini nifungue gari hilo hilo ili kuwaruhusu wenzake kuingia ndani. Nilipokataa, walianza kuligongagonga gari langu huku wakiita tingatinga kulivuta.”

Alisema kuwa baada ya mvutano wa karibu dakika 20, askari hao walimzidi nguvu.

Walimwingiza katika gari lao na kumzungusha jijini bila kufahamu alikokuwa.

Alipokataa kuwapa pesa, walimpeleka katika seli maalum katika Jumba la City Hall na kumfungia huko.

Hata hivyo, aliokolewa na baadhi ya washiriki wa kanisa lake na madiwani walioingilia kati.

Kabla ya kuachiliwa, aliwapa Sh2,000 baada ya baadhi yao kuondoka.

Simulizi ni kama hiyo kwa Bi Mary Wanjiku, ambaye alivunjika jino na kupoteza mkoba wake kwenye patashika kati yake na genge hilo.

“Sikuwa nimefanya kosa lolote waliponikamata na kunipeleka katika Kituo cha Polisi cha Central. Ikizingatiwa nilikuwa na mtoto mchanga aliyekuwa akilia sana, walinipeleka katika ghala la kuwekea bidhaa tofauti. Waliniachilia baadaye,” akasema.

Mchuuzi ambaye hakutaka kutajwa, alisema baadhi ya wanachama wa genge hilo huwa wanawalazimisha wanawake ambao hawana uwezo wa kulipa fedha wanazowaitisha kushiriki nao ngono ili kuachiliwa huru.

“Unakamatwa ghafla na kuwekwa katia gari lao bila kujua. Baadaye huwa wanaanza kukulazimisha kushiriki nao ngono ili kukuachilia huru,” akasema.

Waathiriwa walitoa kauli hizo kwenye kikao maalum ambacho kimeandaliwa na kamati hiyo kupokea malalamishi ya wachuuzi kuhusu dhuluma wanazopitia mikononi mwa askari wa Kaunti.

  • Tags

You can share this post!

Leicester City yajinyanyua na kunyanyasa Newcastle katika...

Kananu ageuzwa ‘gavana kinyago’ mbele yake Uhuru

T L