• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 11:54 PM
Kananu ageuzwa ‘gavana kinyago’ mbele yake Uhuru

Kananu ageuzwa ‘gavana kinyago’ mbele yake Uhuru

Na WANDERI KAMAU

MASWALI yameibuka baada ya Gavana Anne Kananu wa Nairobi kukosa kupewa nafasi ya kuhutubu wakati wa sherehe za Sikukuu ya Jamhuri katika Bustani ya Uhuru, Jumapili.

Ilitarajiwa Bi Kananu angepewa nafasi kuwahutubia wenyeji wa Nairobi, ikizingatiwa imekuwa kawaida kwa magavana wa kaunti ambako sherehe za kitaifa zinafanyika kuhutubia washiriki na kuwakaribisha.

Ni hali ambayo imeibua maswali, baadhi ya wadadisi wakisema hilo haliashirii taswira nzuri kwa Bi Kananu, ambaye aliapishwa rasmi mwezi uliopita kuwagavana mpya wa Nairobi.

“Yalikuwa matumaini ya wengi kwamba ikizingatiwa hiyo ndiyo ilikuwa sherehe ya kwanza ya kitaifa chini ya uongozi wake, angaa angepewa nafasi kuwahutubia wenyeji. Hilo pia lingemkweza kisiasa na kuboresha mwonekano wake,” asema Bw Javas Bigambo, ambaye ni mdadisi wa siasa.

Mchanganuzi huyo anasema ni pigo kubwa la kisiasa kwa Bi Kananu, kwani hiyo ilikuwa nafasi ya kipekee kuonyesha mamlaka yake kama gavana.

“Alipoteza pakubwa. Baada ya kukosa kuonekana kama ilivyofaa, taswira inayoibuka ni ya gavana kinyago, ambaye anadhibitiwa na nguvu kutoka nje na asiye na mamlaka hata kidogo,” akasema.

Tangu kuapishwa kwake, Bi Kananu hajawahi kuiongoza kaunti katika hafla yoyote ya umma.

Wadadisi wanasema udhibiti wa jiji uko mikononi mwa watu wenye ushawishi serikalini, ambao huenda “wakamwadhibu” Bi Kananu ikiwa atakosa kutii na kuzingatia maagizo yao.

Bi Kananu aliapishwa kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Mike Sonko, ambaye alitimuliwa na madiwani wa Nairobi mnamo Desemba 2020.

You can share this post!

Wafichua ukatili wa genge la askari jijini

Kimunya apuuza waundao vyama vidogo Mlimani

T L