• Nairobi
  • Last Updated November 28th, 2023 6:55 PM
Wakeketaji wavuka mipaka, wawakeketa watoto wa umri wa wiki moja

Wakeketaji wavuka mipaka, wawakeketa watoto wa umri wa wiki moja

NA FARHIYA HUSSEIN

MAAFISA wa kutetea haki za watoto katika Kaunti ya Taita Taveta wametoa malalamiko kwamba visa vya ukeketaji katika kaunti hiyo vimeongezeka.

Kulingana na Bi Mercy Nyambu, mmoja wa maafisa wa haki za watoto, ni kuwa licha ya kupitishwa kwa Sheria ya Marufuku ya Ukeketaji ya 2011, ukeketaji bado umeenea katika Kaunti ya Taita Taveta, huku watoto wachanga wa umri wa wiki moja tu wakikeketwa haswa katika maeneo ya vijijini.

“Ni hali ya kusikitisha kuona kwamba watoto wachanga walio na umri wa wiki moja tu wanaletwa kwenye kituo cha afya wakiwa na uchungu baada ya kufanyiwa ukeketaji. Wengine wamefariki kutokana na kuvuja damu nyingi huku wengine wakikabiliana na matatizo ya kiafya baada ya kukeketwa,” alisema Bi Nyambu.

Bi Nyambu alieleza ya kuwa wengine wanasafirishwa kuelekea Tanzania kufanyiwa ukeketaji.

“Wanasafirishwa na waendeshaji pikipiki kwa kutumia njia za ndani ambapo mtu hawezi kujua na kurudishwa saa sita za usiku wakati hata hajapona. Hapa ndipo wengine huanza kutokwa na damu kupita kiasi,” alieleza Bi Nyambu.

Wakati huo huo, Bi Nyambu alilaumu hospitali za kibinafsi kwa usiri mwingi wa kufanya ukeketaji.

“Matokeo yetu yanaonyesha kuwa watoto wapatao 20 wanapitia ukeketaji ndani ya mwezi mmoja na wakati shule zimefungwa, visa vinaongezeka. Itakuwa tatizo ikiwa hakuna kitakachofanyika kuhusu hilo. Tunaomba kikundi cha wanawake kiwekwe mipakani ili tusaidie kuwadhibiti wanaovuka na kutoka nje ya nchi,” alisema Bi Nyambu.

Maeneo ambayo yameorodheshwa kuwa yanayokithiri kwa ukeketaji katika kaunti hiyo ni pamoja na Mata, Kitobo, Salaita, Timbila, Olkug, Ngutini, Eldoro na Marodo, yote katika Kaunti Ndogo ya Taveta, huku katika Kaunti Ndogo ya Taita mila hiyo ikisalia kutawala Sagalla na Kasighau.

  • Tags

You can share this post!

Viongozi 001 waahidi kushirikiana na EACC, ripoti ikitaja...

Jinsi mrembo Patricia Muthoni alivyoongeza ladha kwenye...

T L