• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Wanahabari wafukuzwa wakifuatilia stori ya moto shuleni Mukumu

Wanahabari wafukuzwa wakifuatilia stori ya moto shuleni Mukumu

NA SHABAN MAKOKHA 

BWENI katika shule ya The Sacred Heart Girls’ Mukumu High limeteketea Jumamosi, mkasa huu ukitokea miezi michache tu baada ya wanafunzi kadha kuaga dunia baada ya kula chakula kilichokuwa kimeharibika.

Waandishi wanaofuatilia matukio na visa Kaunti ya Kakamega, wametimuliwa wakifuatilia habari kuhusu mkasa huo wa moto ulioanza saa nne na nusu asubuhi.

Wanafunzi, walimu na wafanyakazi wenye ghadhabu wamewatimua wanahabari wakidai kwamba wamekuwa wakichafulia shule hiyo jina.

Mwalimu mmoja wa kike amewaambia wanahabari kwamba hawakuhitajika kunakili matukio shuleni hapo.

 

Ghafla wanafunzi na wafanyakazi wakawatimua wanahabari

“Hatutaki wanahabari, hatutaki picha,” imesikika sauti ya baadhi ya wanafunzi.

Imewalazimu wanahabari kuondoka upesi kujinusuru.

“Imenilazimu kufunga kamera na vyombo vingine vya kazi na kuondoka ili kujinusuru,” akasema Bw Abel Amala wa MediaMax Networks Limited.

Kulikuwa na mlipuko wa ugonjwa ambao dalili zake zilikuwa ni kuharisha. Mwalimu na wanafunzi watatu waliaga dunia.

Zaidi ya wanafunzi 500 walilazwa walipoanza kuhara na kutapika na vile vile kuhisi maumivu ya tumbo baada ya kula chakula kibovu na maji machafu. Hali ililazimu shule kufungwa mnamo Aprili 3, 2023, lakini ikafunguliwa baada ya wiki tano.

Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu alizuru shule hiyo mnamo Aprili 14, 2023, ambapo alivunja Bodi ya Usimamizi (BoM) na kubuni bodi mpya upesi.

Aliyekuwa mwalimu mkuu wa Mukumu Bi Fridah Ndolo alihamishwa na nafasi hiyo ikajazwa na Mtawa Jane Mmbone Amukoya aliyekuwa katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Shikoti.

Tani 73 za mahindi, maharagwe na mchele ziliharibiwa huku kituo cha maji safi kikijengwa.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Mchakato wa kumtimua Nyaribo waanza mzozo ukichacha

Abiria 4 waaga dunia, tisa wajeruhiwa kwenye shambulio...

T L