• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 5:55 AM
Wapwani kweli wataungana kisiasa au ni ndoto ya mchana?

Wapwani kweli wataungana kisiasa au ni ndoto ya mchana?

Na PHILIP MUYANGA

KUTENGWA kwa chama kinachohusishwa na gavana Amason Kingi na vyama vitano ambavyo chimbuko lao ni pwani kumeibua mjadala iwapo kutawahi kuwa na umoja wa vyama na wanasiasa wa pwani.

Wanachama wa vyama vitano vyenye mizizi yake pwani ambavyo ni Communist Party of Kenya, Shirikisho Party, Kadu Asili, Umoja Summit Party of Kenya na Republican Congress party walisema kuwa chama cha Pamoja African Alliance (PAA) kinachohusishwa na Bw Kingi kimeachwa katika muungano wao.

Swala la umoja wa pwani wa kisiasa limekuwa likijadiliwa kila mara na limekuwa kama wimbo hususan wakati uchaguzi mkuu wa kitaifa ukiwa umekaribia.Wanasiasa ambao hujadili umoja wa pwani kila kukaribiapo uchaguzi mkuu hudai kuwa muungano wa kisiasa wa jamii za wapwani ndio unaweza kuwatoa katika lindi la upweke wa siasa za kitaifa.

WANASIASA WENGINE

Hata hivyo, baadhi ya wanasiasa hususan wale ambao wako katika vyama visemekavyo ni vya kitaifa nchini kama vile United Democratic Alliance (UDA) na Orange Democratic Movement (ODM) wanadai kuwa pwani haiwezi kusimama peke yake bila ya kujihusisha na wanasiasa wengine nchini.

Kulingana na baadhi ya wachanganuzi wa siasa, umoja wa pwani utazidi kuwa ndoto iwapo hakutaundwa mikakati mwafaka ihusishayo wakaazi ili kusaidia kuzindua umoja huo.Wachanganuzi hao wanasema kuwa tofauti na maeneo mengine nchini ambayo yanaonekana kuwa na umoja wa kisiasa,eneo la pwani lina makabila mengi ndiposa umoja huo unaonekana kuwa hauwezi kutekelezwa

.Kulingana na mchanganuzi wa siasa ambaye pia ni mhadhiri katika chuo kikuu cha Pwani Prof Hassan Mwakimako wanasiasa wa pwani hawaangalii taratibu zinazotumiwa na sehemu zingine nchini kuimarisha umoja wa maeneo yao.Alisema kuwa muungano wa kisiasa wa maeneo tofauti huwa kwa mara nyingi ni wa kikabila na kwamba tofauti na maeneo mengine, eneo la pwani lina makabila mengi na sio kabila moja pekee.P

rof Mwakimako aliongeza kusema kuwa mfano wa jamii ya Mijikenda ni kuwa hawajawahi kukubaliana ni nani kati ya makabila tisa chini ya nyumba hiyo anaweza kuwaongoza.“Ni kwa misingi gani ndio umoja huo wa pwani unaanzishwa ama utakuwa? eneo la pwani lina makabila mengi kama vile jamii tisa za Mijikenda, Waswahili, Wataita na jamii zingine, ni vigumu wote kukubaliana kwa pamoja,” alisema Prof Mwakimako.

Prof Mwakimako aliongeza kusema kuwa suluhisho la swala la umoja wa pwani ni kuhakikisha ya kuwa viongozi wa makabila yote ya pwani wanakutana na kuweka baraza la viongozi ili kujadili maswala yanayowakumba.Kulingana na Prof Mwakimako, baraza hilo la viongozi litachukua jukumu la kuunganisha jamii zote za eneo la pwani na kutoa maoni katika kila sekta yanayohusika na jimbo zima la pwani.

Aliyekuwa mwenezi wa chama cha Kanu tawi la Mvita Bw Adulrahman Abdallah asema kuwa umoja wa pwani ni swala lililokuwa linajadiliwa kutoka wakati wa marehemu Waziri Shariff Nassir ambaye alitaka wapwani waungane wawe kitu kimoja.

“Tumejadili sana swala la umoja wa pwani hapo awali,lakini hatukufaulu kwa sababu wanasiasa wengine walikuwa na nia ya kujifaidisha wenyewe badala ya kusaidia jimbo la pwani kwa kuwa pamoja,” alisema Bw Abdallah.Bw Abdallah alisema kuwa kusambaratika kwa umoja wa pwani kunachangiwa pia na wakuu wa vyama mbali mbali kuteua watu wao kuendesha siasa za pwani bila kujadiliana na wanachama wa vyama hivyo.

Mchanganuzi wa siasa Bi Naomi Cidi alisema kuwa yuko na imani ya kuwa umoja wa pwani utapatikana hata kabla ya uchaguzi mkuu ujao wa 2022.“Umoja wa pwani uko, wakati huu hatutakubali kugawanywa kisiasa, vyama vingine vinaletwa kuvuruga wapwani,”alisema Bi Cidi ambaye pia ni katibu mkuu wa chama cha Umoja Summit Party of Kenya.

UNITED PROGRESSIVE FRONT

Umoja Summit Party of Kenya ni mojawapo ya vyama vitano ambavyo vimemuandikia msajili wa vyama vya kisiasa kutengewa jina la United Progressive Front, muungano ambao unatarajiwa kuzinduliwa Januari mwaka ujao.

Bi Cidi aliongeza kusema kuwa muungano wa vyama vyao ulikataa kuvunja vyama hivyo na kuingia kile cha PAA kwani wanachohitaji ni muungano na sio kuvunja vyama.“Nataka utoe ujumbe wazi kabisa ya kuwa watu wanaofikiria umoja wa pwani hautakuwa wajue utakuwa,” alisema Bi Cidi.

Akizungumza na Jamvi hivi majuzi,mchanganuzi wa siasa Bi Maimuna Mwidau alisema kuwa kwa sasa eneo la pwani halijatoa msimamo litapigia kura mrengo upi wa kisiasa na kwamba ilikuwa muhimu wananchi waungane na kutoa kauli moja wakati wa kura ukiwadia.

Takriban wiki mbili zilizopita katika mkutano wa chama cha PAA mjini Mombasa, Bw Kingi alisema kuwa kila kona ya nchi watu wanajipanga na kwamba wakati wa eneo la pwani wa kujipanga ni sasa.“Tumezoea kupangwa, wakati sasa umefika tujipange sisi wenyewe,” alisema Bw Kingi katika mkutano huo.

Akizungumza pia wakati wa mkutano huo aliyekuwa mbunge wa Malindi Bw Lucas Maitha alisema kuwa ni lazima wakazi wa pwani waingie katika uchaguzi ujao kama wapwani wakiwa katika chama kimoja.Bw Maitha alisema kuwa vyama walivyokuwa navyo hapo awali havijawatumikia wapwani ipasavyo.

You can share this post!

Mwiraria: Waziri stadi na mweledi wa uchumi

Rais azindua rasmi sanamu ya Ronald Ngala

T L