• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 3:09 PM
Yaya aliyeangamiza afisa mkuu Kilifi alitoroshwa usiku kwa bodaboda

Yaya aliyeangamiza afisa mkuu Kilifi alitoroshwa usiku kwa bodaboda

MAUREEN ONGALA NA VALENTINE OBARA

MAJIRANI wa afisa mkuu wa uchumi wa baharini katika Kaunti ya Kilifi ambaye aliuawa wiki iliyopita, wamedai kuwa mjakazi anayeshukiwa kutenda unyama huo alitoroshwa kwa bodaboda.

Afisa mkuu huyo, Bi Rahab Katana, aliuawa nyumbani kwake Alhamisi iliyopita katika mtaa wa Mnarani Classic saa chache baada ya kuwasili kutoka ziara ya kikazi nchini Italia.Kulingana na jirani aliyezungumza na Taifa Leo, mjakazi huyo alitoroka wakati majirani walipotambua kisa cha mauaji.

“Tulisikia nduru mara moja lakini tukafikiria ilikuwa inatoka katika kilabu cha burudani ambacho kiko hapa karibu. Tulipochungulia nje tulimuona mama mdogo wa marehemu pamoja na mjakazi huyo. Yule mjakazi alikuwa akijaribu kumsongelea huyo mama ambaye alikuwa akisema kwa sauti ‘shetani, shetani’ na alishinda hivyo hadi tulipoteremka,” akasimulia jirani huyo.

Imedaiwa mama mdogo wa Bi Katana alikuwa anaishi hapo tangu Julai 12, ili kuwalea watoto wawili wa marehemu ambao ni wa kiume wenye umri wa mwaka mmoja na mitatu.

“Tulimuuliza mjakazi huyo tatizo lilikuwa nini lakini alikuwa anachekacheka tu na tukadhania kuwa marehemu alikuwa amepigana na mamake mdogo,” akasema jirani.

Wakati huo wote, hakuna mtu alizungumzia kuhusu mauaji. Walifaulu kumbembeleza mama na kuenda naye nyumbani na hapo ndipo akawaambia kuwa, mfanyakazi alikuwa amemuua tajiri wake.

Kulingana na jirani huyo, waliamrisha baadhi yao kutupa jicho ili mfanyakazi asitoroke lakini alitumia nafasi ya watu kuangalia mwili kutoroka.

Inasemekana msimamizi wa ploti hiyo alibonyeza king’ora na baada ya muda mfupi maafisa kutoka kampuni ya kibinafsi ya ulinzi wakawasili lakini mfanyakazi huyo alikuwa ashatoroka.

Inasemekana aliabiri bodaboda, na maafisa wa polisi sasa wanachunguza ikiwa mwanabodaboda huyo alikuwa ni mshirika wake.

Uchunguzi wa Taifa Leo ulibainisha kuwa, mjakazi huyo alikuwa akifanya kazi katika mtaa wa Mtopanga, Kaunti ya Mombasa, kabla aende Kilifi.

Alikuwa akimfanyia kazi Bi Achieng Agolla Biwott, hadi mapema mwaka huu ambapo alihamia nyumbani kwa mamake Bi Katana, ambaye ni jirani ya Bi Biwott.

Duru zilisema aliishi na mamake marehemu kwa miezi michache kabla apelekwe Kilifi ambapo alifanya kazi kwa karibu miezi mitatu iliyopita.Kwenye mahojiano na Taifa Leo, Bi Biwott alisema alikuwa akimshuku mjakazi huyo tangu alipoanza kumfanyia kazi mwaka uliopita na alikuwa amepanga kumsimamisha kazi lakini akajiuzulu mwenyewe.

Kulingana naye, ishara za kukosa uaminifu zilionekana kwa jinsi alivyojitambulisha kwa jina ambalo si lake wakati alipoletwa kwake, kisha alipoleta kitambulisho kikawa kinaonyesha jina tofauti.Alidai pia kuwa, pesa na mali nyingine zilianza kupotea nyumbani na wakati mwingine zikipatikana kwenye mikoba ya mjakazi huyo alidai ziliwekwa hapo na watoto.

“Nilianza kuwa na wasiwasi kwamba huyu ni mtu ambaye angeweza hata kuniibia mtoto wangu mchanga,” akasema Bi Biwott.

Marehemu alikuwa ameajiriwa katika Kaunti ya Kilifi miezi saba iliyopita, chini ya utawala wa Gavana Gideon Mung’aro.

Upasuaji wa mwili uliofanywa Ijumaa ulionyesha alifariki kwa kudungwa kisu kwenye mapafu kupitia mgongoni.

Alikuwa pia na uvimbe kando ya uso wake.

 

  • Tags

You can share this post!

Gavana Wanga alia kupokonywa mlinzi

Ajabu polo akimnyunyizia bawabu mkojo na kuacha kinyesi...

T L