• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Azimio la Raila lamtikisa Ruto

Azimio la Raila lamtikisa Ruto

Na CHARLES WASONGA

NAIBU Rais William Ruto alihisi uzito wa Azimio la Umoja, kundi linaoongozwa na kinara wa chama cha ODM, Bw Raila Odinga, baada ya juhudi za wabunge wanaomuunga mkono kuangusha Mswada wa Marekebisho ya Sheria za Vyama vya Kisiasa kugonga mwamba bungeni.

Dkt Ruto na washirika wake wanapinga mswada huo lakini hawakuweza kupata idadi ya wabunge wa kutosha kupenyeza mabadiliko ya kutimiza malengo yao.

Naibu Rais ametaja sheria hiyo iliyotarajiwa kurekebishwa kama utapeli wa Bw Odinga na chama tawala cha Jubilee, wa kulazimishia wanasiasa na raia kukubali miungano kama vile Azimio la Umoja “yenye maslahi fiche”.

Hata hivyo, Jumatano, wabunge wanaomuunga Dkt Ruto waliona kivumbi waliposhindwa kuzima mchakato huo na wanaounga juhudi za Bw Odinga.

Wabunge washirika wa Bw Odinga na Rais Uhuru Kenyatta waliwalemea wale wa kambi ya Ruto kwa kuangusha tatu kati ya hoja nne zilizolenga kudhoofisha mswada huo unaopendekeza kuundwa kwa miungano ya vyama vya kisiasa.

Hii ni licha ya wabunge hao wa mrengo wa ‘Tangatanga’ kuleta sarakasi nyingi bungeni wakilenga kuchelewesha kukamilishwa kwa awamu ya tatu ya mjadala kuhusu mswada huo.

Aidha, waliwasilisha hoja nyingi za marekebisho ya sehemu mbalimbali za mswada huo; mengi ya mapendekezo hayo yakifanana.

Juhudi za Mbunge wa Kandara, Alice Wahome za kutaka sehemu ya sita ya mswada huo inayopendekeza kuhalalishwa kwa vyama hivyo, ziliangushwa baada ya kupingwa na wabunge 158 wa ‘handisheki’ dhidi ya 134 waliounga mkono.

Kuzimwa kwa hoja hiyo kunaashiria kuwa vuguvugu la Azimio la Umoja ambalo Bw Odinga anapania kulitumia kuwania urais sasa litaweza kudhamini wagombeaji katika uchaguzi mkuu ujao, baada ya Rais Kenyatta kuutia saini mswada huo kuwa sheria.

Vuguvugu hilo lililozinduliwa rasmi mnamo Desemba 10 katika uwanja wa Kasarani, Nairobi linapania kugeuzwa kuwa chama cha muungano kitakachoshirikisha chama tawala cha Jubilee chake Rais Kenyatta, ODM na vyama vingine kadhaa vinavyounga mkono sera za Bw Odinga.

Akitetea hoja yake Jumatano katika kikao maalum kilichoendelea hadi usiku wa manane, Bi Wahome aliteta kuwa sehemu ya 6 ya mswada huo inakiuka Katiba kwa kupendekeza kuundwa kwa chama cha muungano.

“Bunge hili litakuwa likihujumu vipendele vya 91 na 260 kuhusu sifa za vyama vya kisiasa endapo tutapitisha mswada huu jinsi ulivyo. Ndiposa ninapendekeza kuondolewa kabisa kwa sehemu ya sita ya mswada huo,” akasema mbunge huyo ambaye ni mfuasi sugu wa Dkt Ruto.

Pia, jaribio la mbunge wa Garissa Mjini, Aden Duale la kuifanyia marekebisho sehemu ya 5 ya mswada huo ili kuondoa hitaji kwamba wanaotaka kusajili vyama vya kisiasa wawasilishe taarifa ya sera na itikadi zake kwa afisi ya msajili wa vyama, lilifeli.

Hii ni baada ya jumla ya wabunge 150 wa mrengo wa handisheki kupiga kura ya kudumishwa kwa hitaji hilo huku wabunge 136 wa mrengo wa ‘Tangatanga’ wakitaka liondolewe.

Bw Duale alitaka sehemu hiyo iondolewe ili watu wanaotaka kusajili chama cha kisiasa wasihitajike kuandamanisha taarifa kuhusu sera na itikadi za chama kwenye maombi yao kwa afisi ya msajili wa vyama vya kisiasa.

Lakini watetezi wa mswada huo wakiongozwa na Kiongozi wa Wengi Amos Kimunya walipinga kuondolewa kwa hitaji hilo wakisema kutachangia kuchipuka kwa vyama vidogovidogo “visivyo na maana yoyote” almaarufu, vyama vya mikoba.

Wandani wa Dkt Ruto pia walishindwa na nguvu za wenzao wa mrengo wa handisheki pale hoja nyingine ya marebisho ya mswada huo iliyowasilishwa na Bi Wahome iliposhindwa.

Kwa mara nyingine, mbunge huyo alitaka sehemu ya 7 ya mswada huo inayopendekeza kuwa vyama vya kisiasa viwe na kauli mbiu mahsusi iondolewe.

Hata hivyo, wabunge wa mrengo wa handisheki, wakipigwa jeki na wenzao wa vyama vya Wiper na ANC, waliangusha pendekezo hilo kwa kura 142 dhidi ya kura 15 za wabunge wa ‘Tangatanga’.

Kura hiyo ilipigwa mwendo wa saa sita za usiku, wakati ambapo wengine wa wandani hao wa Dkt Ruto walikuwa wameondoka bungeni kwa kuvunjika moyo.

You can share this post!

Lamu yaongoza kwa ajali za mashua baharini – ripoti

‘Niko tayari kuwa rais wa muhula mmoja’

T L