• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 7:05 PM
KDF: Nembo ya utu kwa raia wema

KDF: Nembo ya utu kwa raia wema

NA KALUME KAZUNGU

MAAFISA wa Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) wanaoendeleza operesheni ya kuwasaka magaidi wa Al-Shabaab kwenye msitu wa Boni katika Kaunti ya Lamu, juma hili waligusa mioyo ya wenyeji walipookoa maisha ya kijana wa umri miaka 16 aliyekuwa akitapatapa msituni baada ya kuumwa na nyoka.

Omar Hamisi ambaye ni mwanafunzi wa Gredi ya Sita katika Shule ya Msingi ya Mangai iliyoko kwenye msitu wa Boni, mnamo Jumanne aliumwa na nyoka huyo aina ya swila au fira wakati akichota maji kwenye kisima kilichoko karibu na mto Mangai.

Aidha juhudi za familia yake na chifu wa eneo hilo, Bw Farah Khalif Sagar, kujaribu kumganga kienyeji zilishindikana, hali iliyomsukuma chifu kutafuta usaidizi kutoka kwa maafisa wa KDF wanaoendeleza operesheni ya kutokomeza Al-Shabaab katika eneo hilo.

Wakati huo, Omar alikuwa katika hali mbaya na kifo kilikuwa kikimkodolea macho kutokana na sumu kali ya nyoka huyo iliyokuwa ikisambaa mwilini haraka.

Isitoshe kiza kilikuwa kimeanza kutanda.

Muda mfupi baada ya Chifu Sagar kupiga simu, Kamanda Msimamizi wa Operesheni ya Msitu wa Boni, kanali Joel Tanui aliagiza chopa ifikishwe mara moja kijijini Mangai, ambapo walimchukua kijana huyo aliyekuwa hali mahututi na kumkimbiza kwenye kambi ya wanajeshi wa ujuzi wa baharini iliyoko Manda, Lamu Magharibi kwa huduma ya kwanza kabla ya kumfikisha kwenye Hospitali ya Mokowe ambapo kwa sasa anapokea matibabu na hali yake ikiwa imedhibitiwa vilivyo.

“Mbali na kukabiliana na kumaliza kero la Al-Shabaab msituni Boni, KDF na walinda usalama wengine bado tuko na jukumu la kuokoa maisha na kuhakikisha maendeleo yanaafikiwa eneo la operesheni. Na hii ndiyo sababu tukafika haraka Mangai kumuokoa kijana aliyeumwa na nyoka na kumfikisha haraka hospitalini kutibiwa. Hiki ni kisa kimoja tu lakini tumetoa huduma nyingi za kibinadamu msituni Boni katika harakati za kuboresha uhusiano wetu na jamii,” akasema Bw Tanui.

Babake Omar, Bw Hamisi Sudi hakuficha furaha yake kufuatia kitendo cha KDF kumsafirisha kijana wake kwa ndege hadi hospitalini kwa matibabu.

“Nawashukuru KDF. Wasingekuwa wao kuingilia kati ninaamini kijana wangu hangekuwa hai sai. Tulijaribu kila namna kumtibu kwa miti shamba lakini wapi. Baada ya kufikishwa hospitalini, kijana amehudumiwa vyema na yuko sawa. Tunatarajia kutoka hospitalini wakati wowote,” akasema Bw Sudi.

Mkurugenzi wa Huduma za Dharura, Kaunti ya Lamu, Bw Shee Kupi, ambaye pia alikuwa miongoni mwa timu iliyofika kusaidiana na KDF kumsafirisha kijana hospitalini kwa helikpopta ya kijeshi alisifu ushirikiano uliopo kati ya walinda usalama na wakazi wa vijiji vya msitu wa Boni na Lamu kwa ujumla.

Bw Kupi aliahidi kuendeleza kampeni za kuhakikisha raia wa Lamu wanashikana vilivyo na KDF na walinda usalama wengine ili kufaulisha juhudi za kumaliza ugaidi na kudhibiti usalama Lamu.

Ikumbukwe kuwa vijiji vya msitu wa Boni – Basuba, Milimani, Mangai, Mararani na Kiangwe – vimekosa huduma za afya kwa karibu miaka 10 sasa baada ya zahanati zilizokuwa zikihudumia wakazi eneo hilo kufungwa kutokana na kukithiri kwa mashambulio ya kila mara ya wanamgambo wa Al-Shabaab.

Madaktari na wauguzi waliokuwa wakihudumia wananchi katika eneo hilo pia walihama wasirudi tena kwa kuhofia kulengwa na kumalizwa na Al-Shabaab.

Tangu hapo, wakazi wamekuwa wakiishi kwa kutegemea rehema kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwani kila anayepatwa na dharura au kushikwa na uhitaji wowote wa matibabu lazima atumie angalau Sh12,000 kusafiri awamu moja kufikia huduma za matibabu mjini Lamu ambako ni mbali mno.

Barabara za msitu wa Boni pia zimekuwa zikikwepwa na wakazi kutokana na hulka ya Al-Shabaab kuzika vilipuzi vya ardhini ambavyo vimeishia kuua mamia ya walinda usalama na wakazi kila mwaka.

Si mara ya kwanza kwa KDF kutoa huduma kwa jamii ya Lamu.

Mnamo Februari 2023, maafisa hao waliwafadhili kimasomo wanafunzi watatu werevu waliokuwa wamefanya vyema katika KCPE Lamu, ambapo waliwasafirisha kwa helikopta ya kijeshi kutoka Lamu hadi kwenye Shule ya Upili ya Jeshi ya Moi Forces Academy iliyoko Eastleigh, jijini Nairobi wanakoendelea na masomo.

Wanafunzi hao ni Nathaniel Ushindi Chanzera (17), Ryan Karisa (16) na Ali Mohamed (15).

Mwezi huo huo, KDF waliwapeperusha kwa helikopta walimu 25 kutoka Lamu Magharibi hadi kwenye shule za vijiji vya msitu wa Boni vilivyoko Lamu Mashariki ili kufundisha.

Maafisa wa KDF wakimbeba hobelahobela kijana Omar Hamisi,16, kumuingiza kwa ndege kumpeleka hospitalini upesi baada ya kuumwa na nyoka kijijini Mangai, Lamu Mashariki mnamo Jumanne, Agosti 8, 2023. PICHA | KALUME KAZUNGU

Hii ni baada ya usafiri wa aina nyingine, ikiwemo barabara na maji kushinikana.

Desemba 2018, wakazi wa msitu wa Boni waliwatambua wanajeshi wa KDF na walinda usalama wengine wanaoendeleza operesheni ya kusaka Al-Shabaab msituni kama mashujaa wao wa mwaka huo.

Desemba iyo hiyo, wanajeshi wa KDF waliteka nyoyo za wengi pale walipookoa maisha ya mama mjamzito kutoka kijiji cha Mangai, ambapo walimsafirisha haraka kwa ndege hadi hospitali kuu ya King Fahd mjini Lamu alikojifungua mapacha.

Mwananua Mahazi alikuwa ameumwa na tumbo ya uzazi kwa muda wa siku nne mfululizo kabla ya hali yake kuwa mbaya zaidi na kulazimu KDF kuingi,lia kati na kumuokoa kwa kumpeleka hospitalini kujifungua salama salmini.

Tangu walipofikishwa msitu wa Boni kuendeleza operesheni ya kusaka Al-Shabaab Septemba 2015, KDF pia wamekuwa wakiandaa kambi za bure za matibabu mara kwa mara, ambapo maelfu ya wakazi wa msitu wa Boni wamenufaika pakubwa.

  • Tags

You can share this post!

Afisa wa DCI auawa, mkewe ajeruhiwa

Baadhi ya changamoto za wanafunzi katika mitaa ya mabanda

T L