• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
Koome adai Azimio ‘walinunua’ maiti za maandamano

Koome adai Azimio ‘walinunua’ maiti za maandamano

NA MWANGI MUIRURI

INSPEKTA Jenerali wa Polisi Japhet Koome amedai kwamba viongozi wa Azimio la Umoja-One Kenya walikodisha maiti za kuonyesha wanahabari ili kusuka stori ya ukatili wa maafisa wa polisi katika kuzima maandamano.

Bw Koome akihutubia kikao cha wanahabari katika taasisi ya masomo ya polisi ya Kiganjo katika Kaunti ya Nyeri alisema kwamba “huo ndio ujanja wa wanasiasa wenu”.

Alisema kwamba ripoti za ujasusi zilionyesha wazi kwamba wanasiasa hao walikodisha miili kutoka mochari za kibinafsi ili kuharibia polisi jina.

“Sitaki kusema zaidi ya hapo lakini nitawatetea maafisa wangu mpaka mwisho kwamba tulifanya kazi kwa kufuata sheria,” akasema.

Akishikilia msimamo wa Rais William Ruto na wandani wake wa Kenya Kwanza kwamba hakuna wakati mwingine maandamano yatakubalika hapa nchini.

“Tuliwapa nafasi ili watekeleze maandamano yao kwa msingi wa kikatiba. Lakini walijigeuza kuwa majambazi wa kuharibu, kupora na kushambulia na kwa mujibu wa sheria tukaingilia kati kulinda maisha na mali,” akasema.

Bw Koome aliongeza kwamba idara ya polisi haijalishwi na vitisho kwamba itaandaliwa kesi katika Mahakama ya Kimataifa kuhusu Uhalifu dhidi ya binadamu (ICC) akisema “ikiletwa tutaichangamkia”.

Bw Koome alisema kwamba kutisha idara ya polisi ni sawa na kupanda mchongoma.

Alisema maafisa wake wakishambuliwa huku wengine wakiaga dunia, makumi ya wengine wakapata majeraha huku hata magari ya polisi yakichomwa.

Hata hivyo, aliyekuwa Waziri Msaidizi (CAS) katika wizara za Elimu na Spoti Bw Zack Kinuthia alitaja taarifa ya Bw Koome kama ya kishenzi.

Alisema kwamba ni kinyume na sheria kusumbua maiti na ikiwa Bw Koome ana ushahidi wa asemayo, anafaa kuwafunguliwa kesi mahakamani washukiwa hao anaowataja.

“Ni aibu kwamba kiongozi wa Idara muhimu ya polisi amejigeuza kuwa mwanasiasa wa pesa nane wa kusambaza propaganda za aibu,” akasema.

Mbunge wa Embakasi Mashariki Bw Babu Owino alisema “ushahidi wetu kwamba hii serikali imepoteza mwelekeo kabisa ndio huo kwa kuwa hatukutarajia isherehekee mauti ya udhalimu wa polisi na hatimaye itoe taarifa za kujitakasa zilizojaa upuzi”.

Seneta wa Nairobi pamoja na aliyekuwa Gavana wa Murang’a Bw Mwangi wa Iria walisema kwamba wamesikitishwa si haba na matamshi hayo ya Bw Koome.

“Ni aibu isiyo na kifani. Tutaendelea kusaka haki dhidi ya wahanga wa dhuluma hizo za polisi. Pole sana kwa familia za waathiriwa ambao kwa sasa wametwikwa kicheko cha dharau na serikali hii katika majonzi yao,” akasema Wa Iria.

  • Tags

You can share this post!

Mzungu atupwa jela miaka 81 kwa kuwadhulumu kingono...

Hofu Mung’aro akiamuru idara ziamue hatima ya vibarua

T L