• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 4:39 PM
KRA yamezea mate mapato ya mama mboga, bodaboda

KRA yamezea mate mapato ya mama mboga, bodaboda

NA PATRICK ALUSHULA

MAMLAKA ya Ukusanyaji wa Ushuru Kenya (KRA), imetengewa Sh1.2 bilioni za kuajiri maafisa zaidi wa kijasusi na utekelezaji ambao jukumu lao litakuwa ni kuandama na kuwakamata wanaokwepa kulipa ushuru katika juhudi mpya za kuongeza mapato ya serikali ikome kutegemea mikopo.

Kamati ya Bunge ya Bajeti na Matumizi katika makadirio ya bajeti ya mwaka unaoanza Julai, imeomba Wizara ya Fedha kutoa mabilioni zaidi kwa KRA iajiri wafanyikazi zaidi.

Wafanyakazi hao wataimarisha ukusanyaji wa mapato kutoka kwa ushuru mpya uliopangwa kuanzishwa na kufuata wanaokwepa kulipa huku Wizara ya Fedha ikilenga kukusanya angalau Sh400 bilioni zaidi kutoka kwa ushuru mwaka wa kifedha unaoanza mwezi Julai.

Kamati hiyo imeongeza bajeti iliyowasilishwa na Wizara ya Fedha bungeni kwa Sh81 bilioni za matumizi hadi Sh3.67 trilioni, na hivyo kuweka presha zaidi kwa KRA.

Ili kuimarisha mapato, utawala wa Rais William Ruto umependekeza nyongeza ya ushuru kwa bidhaa kama vile mafuta, nyumba, utumaji pesa kwa njia ya simu na maudhui ya kidijitali, hali inayowakasirisha wananchi na upinzani wanaosema kwamba, gharama ya maisha tayari iko juu mno.

“Ongezeni Sh1.2 bilioni kwa KRA kuajiri wasaidizi wa kusaidia kukusanya ushuru,” inasema Kamati ya Bajeti na Matumizi katika mapendekezo ambayo yanasubiri kuidhinishwa na wabunge.

Mwanzoni mwa Mei, KRA ilitangaza kazi za wasaidizi wa huduma ya mapato, ikiorodhesha jukumu lao kama kusimamia utoaji wa stakabadhi za e-TIMS na wafanyabiashara, kuhakikisha wafanyabiashara waliosajiliwa kwa VAT wanatii na kufuata kanuni za ushuru.

Majukumu mengine ni kuandaa ripoti za kila wiki na kila mwezi za kesi zinazoshukiwa za ukwepaji ushuru, kutuma notisi za kukamatwa kwa bidhaa zilizozuiliwa kuhusiana na ushuru, kutwaa na kuhakiki stakabadhi za ushuru zinazotolewa na wafanyabiashara na walipa ushuru.

Dkt Ruto, ambaye alichaguliwa Agosti 2022 kwa ahadi ya kusaidia maskini, amejipata katika hali mbaya miezi ya kwanza ya muhula wake kutokana na kuongezeka kwa ulipaji wa deni la serikali, kupungua kwa ukusanyaji wa mapato na bei za juu za bidhaa za kimsingi.

Anakabiliwa na shinikizo za kuongeza mapato kutokana na kuongezeka kwa ulipaji wa madeni huku akisukumwa kuhakikisha kuna uthabiti wa kifedha na nafasi za ajira kwa vijana.

Ushuru unaokusanywa na KRA, ambao ni sehemu kubwa ya mapato ya serikali unabashiriwa kuongezeka hadi Sh2.43 trilioni kutoka Sh2.04 trilioni inazokusanya kufikia mwisho wa mwaka wa kifedha unaomalizika Juni.

Wizara ya Fedha itatumia data na uhusiano kati ya mifumo ya KRA na wahusika wengine kama vile benki na huduma za kutuma pesa kwa simu kama M-Pesa kuchunguza shughuli za walipa kodi na pia matumizi ya kamera zinazotumia mtandao kwenye mitambo ya kutengeneza bidhaa zinazotozwa ushuru.

Dkt Ruto amesema kwamba, juhudi za serikali za kukusanya ushuru zinahujumiwa na wafanyakazi fisadi wa KRA, anaosema wamekuwa wakisaidia wafanyabiashara kukwepa kulipa ushuru.

  • Tags

You can share this post!

Askari aangushiwa kichapo kwa madai ya wizi wa ng’ombe  

Eric Omondi na mpenziwe watarajia mtoto baada ya kupoteza...

T L