• Nairobi
  • Last Updated October 2nd, 2023 10:18 AM
Mackenzie na wenzake wasusia mlo wakidai matamshi ya Kindiki yanaashiria hawatapata haki

Mackenzie na wenzake wasusia mlo wakidai matamshi ya Kindiki yanaashiria hawatapata haki

NA BRIAN OCHARO

MHUBIRI tata wa dhehebu la Good News International Paul Mackenzie na wafuasi wake sasa wamesusia chakula kutokana na matamshi ya Waziri wa Usalama wa Ndani Prof Kithure Kindiki kwamba wataozea gerezani.

Washukiwa zaidi ya 30 ambao wanachunguzwa kuhusiana na mauaji ya Shakahola wamelalamika kwamba hawatapata haki kwa sababu waziri amewapata na hatia hata kabla ya kufunguliwa mashtaka rasmi dhidi yao.

Kupitia kwa wakili wao Wycliffe Makasembo, washukiwa hao wamelalamika kwamba matamshi ya Prof Kindiki yametishia haki yao ya kusikilizwa kwa haki na haki ya kikatiba kuchukuliwa kuwa hawana hatia hadi itakapothibitishwa vinginevyo.

“Ninapohutubia mahakama hii, baadhi ya washukiwa wamegoma kula. Maneno ambayo yalisemwa na Prof Kindiki ni hatari, ni kinyume cha sheria na hayastahili kabisa,” Bw Makasembo amemweleza Hakimu Mwandamizi Mkuu wa Shanzu Yusuf Shikanda.

Pia wametishia kususia kesi zaidi iwapo Prof Kindiki atakosa kubatilisha matamshi yake, ambayo walisema yana uwezo wa kuingilia utendakazi wa mahakama kuendesha mambo yake kwa njia inayozingatia haki.

Kulingana na wakili huyo, washukiwa wanahisi kuwa mchakato wa kimahakama unaofanywa kwa sasa hauna maana kwa sababu ya matamshi ya Prof Kindiki.

“Tunahitaji uhakikisho kutoka kwa Jaji Mkuu Martha Koome, Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai na Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili Kenya (LSK) kwamba washukiwa watapata haki, kusikilizwa kwa haki kwa kuwa Prof Kindiki tayari amewapata na hatia ,” amesema Bw Makasembo.

Prof Kindiki alisema wakati wa mkutano na waandishi wa habari huko Shakahola na wakati wa hafla ya kanisa wiki jana kwamba hata kama mahakama itamuachilia huru Mackenzie na wafuasi wake, atahakikisha kwamba anawarudisha gerezani ambapo wataozea huko maisha yao yote.

“Ikiwa yeye (Prof Kindiki) anahisi kuwa mahakama zetu hazina uwezo, anaweza kukaribisha mashirika ya kimataifa kama Umoja wa Mataifa (UN) kuja kuendesha kesi ya Mackenzie,” wakili huyo amesema.

Wakili huyo pia amelalamika kuwa polisi wamebomoa nyumba za washukiwa na pia kuchukua mifugo yao.

Hata hivyo, Kiongozi wa Mashtaka Ogega Bosibori ameomba mahakama kupuuza matamshi ya Bw Makasembo akisema wakili alileta kesi hiyo katika jukwaa lisilofaa.

“Iwapo wakili anahisi kudhulumiwa na kwamba haki za wateja wake zimekiukwa, anajua jukwaa sahihi la kuwasilisha malalamiko badala ya kutoa tuhuma hizo katika mahakama hii,” akasema.

Wakili wa waathiriwa Abubakar Yusuf ameiomba mahakama kupuuza madai hayo, akisema matamshi yaliyotolewa nje ya mahakama hayana thamani kwa kesi ambazo tayari ziko mahakamani.

“Hii ni mahakama ya sheria na haina jukumu la kutilia maanani chochote kinachosemwa sokoni na/au katika jukwaa la kisiasa. Ni makosa kwa Bw Makasembo kuwasilisha yale yaliyosemwa na Prof Kindiki. Huyo waziri si mhusika katika kesi hii,” akasema.

Hakimu hata hivyo amedokeza kuwa mahakama yake haiwezi kumtetea Prof Kindiki na kwamba maoni yake hayataathiri kwa vyovyote jinsi mahakama yake itakavyoshughulikia kesi hiyo.

“Prof Kindiki ni afisa wa ngazi za juu serikalini, na kwa mwananchi wa kawaida, matamshi yake yanaweza kuwa na uzito zaidi. Hata hivyo, ninawahakikishia washukiwa kwamba mahakama hii itasimamia haki,” amesema hakimu.

  • Tags

You can share this post!

Itumbi alia kucheleweshwa kwa kesi ya ‘njama ya...

Rais Samia Suluhu akatizia Wakenya ugali mpakani

T L