• Nairobi
  • Last Updated May 22nd, 2024 4:21 PM
Rais Samia Suluhu akatizia Wakenya ugali mpakani

Rais Samia Suluhu akatizia Wakenya ugali mpakani

Na STANLEY NGOTHO

TAKRIBANI malori 200 yaliyokuwa yakisafirisha mahindi ili kuyaingiza Kenya yamekwama mpakani Namanga baada ya maafisa wa Tanzania kusitisha utoaji wa vibali vya kusafirisha mahindi nje ya nchi hiyo.

Haya yanajiri wakati ambapo uhaba wa mahindi Kenya umesababisha bei ya unga kupanda na kulemea raia wa kawaida.

Baadhi ya malori hayo yamekwama mpakani, upande wa Tanzania, kwa muda wa wiki moja iliyopita.

Wafanyabiashara wanasema wamepata hasara kubwa hasa wale waliokodisha malori kusafirisha nafaka hiyo kuingia nchini.

Serikali ya Tanzania imesitisha mara moja utoaji wa vibali vya kuuza nje, ya nchi hiyo, kwa wafanyabiashara wa Kenya na kuwaacha wakikwama na shehena za mahindi katika mpaka wa Namanga.

Uchunguzi wa Taifa Leo mnamo Jumatano, Juni 7, 2023 ulibaini kuwa wafanyabiashara hao wamekata tamaa.

Malori yaliyokuwa yakisafirisha bidhaa hiyo adimu yalikuwa yameegeshwa huku malori mengine yakifika kila saa.

Wafanyabiashara wa mahindi na mawakala wa kupitisha bidhaa walilemaza shughuli mpakani wakitaka malori yaliyokwama yaruhusiwe kuingia Kenya.

Shughuli katika ofisi zote za forodha, Tanzania na Kenya zilikwama.

Baadhi ya wafanyabiashara waliketi kwenye barabara za maegesho baada ya juhudi za kutaka mizigo yao iondolewe kukosa kufaulu.

Madereva wa malori walionekana kuchoka na kukosa matumaini huku wengine wakitishia kushusha mizigo kwenye maegesho.

Bw Sammy Mwaura, dereva wa Brotherhood Transporter kutoka Nakuru alisema kwamba amezuiliwa tangu Jumanne wiki jana.

Alikuwa akisafirisha magunia 100 ya nafaka kutoka Katesi nchini Tanzania lakini alifahamishwa kuwa hangeruhusiwa na serikali ya Tanzania.

“Nimekwama kwa wiki moja iliyopita bila tumaini la kupata kibali. Tunapata hasara kubwa kila siku. Serikali za nchi hizi mbili zihakikishe biashara ya kuvuka mipaka haitatiziki,” alisema.

Mfanyabiashara aliyekuwa na malori kadhaa ya mahindi mpakani, ambaye alizungumza kwa sharti la kutotajwa jina, aliambia Taifa Leo kuwa amenunua mahindi ya Sh10 milioni kwa matumaini ya kupata faida katika soko la Kenya.

“Nilikuwa na agizo la kusambaza mahindi kwa msagaji wa unga nchini Kenya. Siwezi kusambaza licha ya kukopa mtaji kutoka kwa taasisi ya fedha,” alisema kwa uchungu.

Katibu wa Chama cha Kimataifa cha Usafirishaji na Mabohari Kenya (KEFWA) aliye Namanga, Zachary Mwangi alisema hatua mpya za serikali ya Tanzania zilipaswa kutekelezwa kuanzia Julai 1, 2023.

Bw Mwangi alisema wafanyabiashara wa Kenya wako katika hatari ya kupoteza mamia ya mamilioni ya pesa iwapo mzozo huo hautatatuliwa kwa njia ya amani.

“Serikali ya Tanzania ilipaswa kuwatahadharisha wafanyabiashara wa mahindi kuwa haitatoa vibali vya kuuza nje kwa wafanyabiashara kwa wakati unaofaa. Juhudi zetu za kufikia mamlaka husika zimegonga mwamba,” alisema Bw Mwangi.

Aidha, aliitaka serikali kuharakisha kuokoa wafanyabiashara wa Kenya ili wasipate hasara kubwa.

“Malori 200 yanayosafirisha mahindi yamekwama mpakani. Malori mengine yako njiani. Uhaba wa nafaka ya mahindi nchini Kenya unazidi ilhali maelfu ya tani za bidhaa hiyo zimezuiwa kwenye mpaka,” aliongeza.

  • Tags

You can share this post!

Mackenzie na wenzake wasusia mlo wakidai matamshi ya...

Mackenzie aambia Kindiki anachopigana nacho kitamramba

T L