• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Mandago akamatwa kwa kashfa ya Sh1.1 bilioni

Mandago akamatwa kwa kashfa ya Sh1.1 bilioni

NA RICHARD MUNGUTI

SENETA wa Uasin Gishu Jackson Mandago alikamatwa Jumatano na kuzuiliwa kuhusiana na kashfa ya Sh1.1 bilioni ya kuwapeleka wanafunzi kwa masomo ya juu nchini Finland na Canada.

Mandago, aliyekuwa Gavana wa Kaunti hiyo kati ya 2013-2022, alitiwa nguvuni saa moja baada ya mahakama ya Nakuru kuamuru atiwe nguvuni pamoja na washukiwa wengine watatu.

Kamanda wa Polisi Nakuru Samuel Ndanyi amethibitisha Mandago atapandishwa kizimbani kesho Alhamisi.

Maafisa kutoka kitengo cha kuchunguza kesi sugu katika Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) walimkamata Mandago.

Hakimu mkuu katika mahakama ya Nakuru aliamuru Seneta huyo akamatwe pamoja na Joseph Kipkemoi Maritim, Meshack Rono na Joshua Kipkemboi Lelei.

Maritim, Rono na Lelei walikuwa maafisa wakuu katika Serikali ya Kaunti ya Uasin Gishu, Mandago akiwa Gavana.

Agizo la kutiwa nguvuni kwa Mandago lilifuatia ombi la Naibu wa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Victor Mule.

Akiwasilisha ombi kortini Mule alisema: “Faili ya malalamishi dhidi ya Mandago na wenzake watatu ilikaguliwa upya na ikapatikana kuna ushahidi wa kutosha kuwafungulia mashtaka. Naomba korti itoe kibali watiwe nguvuni.”

Katika mahojiano na Taifa Leo Bw Mule alidokeza kwamba uchunguzi huo ulifanywa na kitengo cha kushughulikia uhalifu sugu katika idara ya DCI na kupata upo ushahidi wa kuwezesha kushtakiwa kwa wanne hao.

Bw Mule alifichua kwamba tayari cheti cha mashtaka kimetayarishwa na ushahidi kuandikishwa kutoka kwa mashahidi.

“Afisi ya DPP iko tayari kuwafungulia mashtaka washukiwa hao wanne,” Bw Mule aliambia Taifa Leo.

Alisema ushahidi upo unaoonyesha jinsi pesa zilivyotolewa kutoka kwa akaunti ya Hazina ya Kaunti ya Uasin Gishu ya Kufadhili Masomo nchini Canada na Finland na baadhi ya washukiwa.

Pesa ziliwekwa katika akaunti ya hazina ya masomo nchini Finland na Canada na wazazi wa wahasiriwa.

Wanafunzi walirejeshwa Kenya kutoka Finland na Canada baada ya kukosa karo.

Wazazi wao waliweka pesa katika benki ya Kenya Commercial Bank, Eldoret.

Cheti cha mashtaka kimesema Mandago na wenzake watatu walikula njama za kulaghai wanafunzi Sh1.1 bilioni kati ya Machi 1 na Septemba 12, 2021.

Pia Mandago amekabiliwa na mashtaka ya matumizi mabaya ya mamlaka kwa kutia saini mkataba wa maelewano ya kaunti ya Uasin Gishu kufadhili masomo ya wanafunzi nchini Finland na Canada.

Mahakama ilielezwa wanafunzi walioathirika ni 202.

Kabla ya kukamatwa kwa Mandago, Rais William Ruto anayezuru kaunti hiyo alisema “wote waliohusika na kashfa hiyo watakumbana na makali ya sheria.”

Rais Ruto aliwaahidi wanafunzi walioathirika kwamba serikali itatafuta namna ya kufadhili elimu yao Finland na Canada lakini akaongeza, “Waliowatapeli wazazi hawa ni bure kabisa na Serikali itaonana nao barabara.”

Katika mashtaka yaliyoandaliwa na DPP, Mandago, Joseph Kipkemoi Maritim, Meshack Rono na Joshua Kipkemoi wamefunguliwa mashtaka ya kuiba, kutumia vibaya mamlaka ya afisi na kupanga njama za kuwatapeli wanafunzi pesa kupitia hazina ya ufadhili wa masomo nchini Finland na Canada

Maritim, Rono na Lelei wameshtakiwa kuiba Sh56,512,300 kutoka kwa akaunti ya hazina ya ufadhili ya masomo ng’ambo (UGOET) iliyoko benki ya KCB tawi la Eldoret Mashariki.

Watatu hao wameshtakiwa kuiba pesa hizo kati ya Juni 2021 na Septemba 12, 2022.

Maritim ameshtakiwa kuiba Sh660,000 pekee naye Rono ameshtakiwa kuiba Sh10,820 kati ya Juni 15, 2021 na Septemba 5, 2022 kutoka kwa akaunti ya UGOET.

Lelei ameshtakiwa kuiba Sh2,707,000 kutoka kwa akaunti hiyo ya UGOET.

Wote wanne wanakabiliwa na mashtaka ya kutumia vibaya mamlaka ya afisi zao kwa kudanganya akaunti hiyo ya UGOET ilikuwa inafadhiliwa na kaunti ya Uasin Gishu.

Mandago ameshtakiwa kutumia vibaya mamlaka ya afisi yake alipokuwa Gavana kwa kutia saini mkataba wa masomo kati ya serikali za Finland na Canada kwa niaba ya kaunti hiyo.

  • Tags

You can share this post!

Rais Ruto amtaka Mandago, wenzake wabebe msalaba kuhusu...

Omanyala tayari kutetemesha Budapest baada ya mazoezi...

T L