• Nairobi
  • Last Updated December 5th, 2023 8:55 PM
Omanyala tayari kutetemesha Budapest baada ya mazoezi Miramas

Omanyala tayari kutetemesha Budapest baada ya mazoezi Miramas

GEOFFREY ANENE na AYUMBA AYODI

MSHIKILIZI wa rekodi ya Afrika mbio za mita 100, Ferdinand Omanyala ametangaza yuko tayari kwa Riadha za Dunia nchini Hungary zitakazoanza Agosti 19 baada ya uchaguzi wa Shirikisho la Riadha Duniani.

Bingwa huyo wa Kenya, Afrika na Jumuiya ya Madola aliwasili katika eneo la mashindano jijini Budapest mnamo Agosti 15 akitokea mjini Miramas nchini Ufaransa alikofanyia mazoezi yake.

“Bila shaka, nimepata vifaa vya hali ya juu.  Miramas ilikuwa sehemu nzuri ya kufanyia mazoezi kwa sababu ilikuwa tulivu sana na rahisi kufanya mazoezi. Niko tayari kwa mashindano,” alieleza Taifa Leo hapo Jumatano.

Omanyala ni mmojawapo wa wanariadha Kenya ina matumaini nao kupata medali, ingawa atalazimika kujituma vilivyo kupata kitu kwa sababu mashindano haya yamevutia watimkaji wote wakali wakiwemo Fred Kerley (bingwa mtetezi) kutoka Amerika, Letsile Tebogo (Botswana) na Akani Simbine (Afrika Kusini).

Rais wa Shirikisho la Riadha Kenya (AK) Jackson Tuwei atawania kuwa mmoja wa manaibu rais wa Shirikisho la Riadha Duniani jijini Budapest wakati wa kongamano la 54 la shirikisho litakalofanyika Agosti 17 na Agosti 18 katika jumba la mikutano la Hungexpo.

Uchaguzi wa rais, manaibu rais na wanachama wa baraza ni Agosti 17.

Ripoti za kifedha, tume na kitengo cha riadha cha maadili zitawasilishwa wakati wa mkutano huo.

Mwingereza Sebastian Coe, ambaye alirithi urais kutoka kwa raia wa Senegal Lamine Diack mwaka 2015, anatarajiwa kuhifadhi kiti chake bila kupingwa.

Wadhifa wa naibu mkuu wa rais uko wazi baada ya Sergey Bubka kuamua hatautetea.

Wadhifa huo pamoja na nyadhifa nne za manaibu rais zitawaniwa na wagombea wanane akiwemo Tuwei ambaye pia ni naibu mkuu wa rais wa Shirikisho la Riadha barani Afrika (CAA).

Kati ya wanane wanaomezea mate nyadhifa nne za manaibu rais ni Nawaf Bin Mohammed Al Saud kutoka Saudi Arabia, Geoff Gardner (Norfolk Island) na Ximena Restrepo (Chile) wanaotetea viti vyao.

Pia, kuna wanawake wawili – Restrepo na Abby Hoffman kutoka Canada.

Tuwei anaamini kuwa kusajiliwa kwa zaidi ya wanariadha 5,000 nchini Kenya, uungwaji mkono na serikali na kuwa mstari wa mbele katika masuala ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, pamoja na mipango kabambe ya maendeleo, Kenya inastahili kupata kiti katika Shirikisho la Riadha Duniani ambako maamuzi mengi kuhusu riadha hufanywa.

Tuwei pia ni mmoja wa wagombea 27 wanaotaka mojawapo ya viti 13 vya wanachama wa baraza.

  • Tags

You can share this post!

Mandago akamatwa kwa kashfa ya Sh1.1 bilioni

Uingereza watinga fainali ya Kombe la Dunia baada ya...

T L