• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 8:55 PM
Masoja waomba kumiliki bastola badala ya nyongeza ya mshahara 

Masoja waomba kumiliki bastola badala ya nyongeza ya mshahara 

NA RICHARD MAOSI

BAADHI ya kampuni zinazotegemea ulinzi wa mabawabu nyakati za usiku zinaomba serikali kuzipa vibali kumiliki bastola, zikidai rungu hazitoshi kulinda mali ya Wakenya.

Kwenye mahojiano ya kipekee na Taifa Leo Dijitali, baadhi ya masoja wa kampeni hizo wanasema hawaoni haja ya kuongezewa mishahara ilhali maisha yao yapo hatarini.

“Maeneo kama vile Kariobangi, Kayole, Mwiki, na Githurai ni hatari sana nyakati za usiku, hivyo basi tunaomba serikali kuangazia maslahi yetu ya kiusalama kwanza kabla ya kutuangalia kiuchumi,” anasema Bw Pius Baraza, mlinzi kutoka Makadara.

Hili linajiri siku chache tu baada ya serikali kushinikiza kampuni za kibinasi kuajiri walinzi, zianze kulipa mabawabu kuanzia mshahara usiopungua Sh30,000 kwa mwezi.

Hatua hiyo, serikali ya Rais William Ruto inasema ni njia mojawapo kuwakwamua kiuchumi kutokana na hali ngumu ya maisha inayoendelea kushuhudiwa nchini.

Ali Ndanu mlinzi kutoka kampuni ya Riley Africa aliambia Taifa Leo Dijitali kuwa kazi yao huwa ni ngumu na baadhi ya maeneo yanahitaji watumie nguvu ya ziada kama vile bastola au bunduki kukabiliana na wahalifu usiku.

Kulingana na Ndanu, baadhi ya maeneo hayakaliki visa vya wizi vinapotokea huku wakiishia kulaumiwa kuzembea kazini.

“Imefika wakati ambapo pia sisi tunastahili kupatiwa hadhi kama polisi,” Ndanu akasema.

Katika suala la mishahara, mlinzi huyo anasema wanapewa mapato kidogo mno, Sh8, 000 na wenye bahati wakilipwa Sh15, 000 kwa mwezi.

Malipo hayo duni yamechochea baadhi yao kuwa na mikono mirefu, wizi.

Kwingineko, Alice Chebet (sio jina halisi) mlinzi katika kampuni ya Ultimate Security ameapa kushinikiza viongozi wao kufuatilia mapendekezo ya serikali, akidai kwamba haoni dalili ya wao kuongezewa mshahara.

Kwa upande mwingine, Wakenya mitandaoni wameponda serikali wakihoji kwamba pendekezo la nyongeza ya mishahara kwa walinzi wa kibinafsi ni ndoto za mchana, kwa sababu waajiri wengi hawako tayari kuongeza mishahara.

Aidha, wanashangaa, ikiwa waajiri wanakosa kuongezea mabawabu suala la kuwapa silaha kama vile bastola na bunduki ndilo litawezekana?

Baadhi wanapinga hatua ya walinzi kupewa silaha.

Mark Sigei, mtandaoni anasema walinzi wa usiku huwa wana hasira nyingi hivyo basi wataishia kupiga wattu risasi.

Natasha Meta, kwa upande mwingine anasema hakuna haja ya kuitisha bunduki kwa sababu hela ni muhimu kushinda silaha.

Naye Proteus Terer, naye anaomba masoja kukoma kusumbua Wakenya kwa malalamishi yao ya mara kwa mara, kuhusu nyongeza ya mshahara.

  • Tags

You can share this post!

Chuma cha Gavana Arati motoni mahasimu wake kisiasa...

Jicho Pevu aahidi maskwota ardhi akisema Ruto atainunua ili...

T L