• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 4:32 PM
Matian’gi, Michuki na Magoha, sura na sauti anazokosa Rais Ruto kutisha waandamanaji

Matian’gi, Michuki na Magoha, sura na sauti anazokosa Rais Ruto kutisha waandamanaji

NA MWANGI MUIRURI 

WAANDANI wa Rais William Ruto sasa wamekiri kwamba wanakosa sura na sauti sawa na za Dkt Fred Matian’gi, John Michuki na George Magoha ili kukabiliana na waandamanaji wa upinzani.

Katika mkutano wa pamoja uliohudhuriwa na wanasiasa 241 wa United Democratic Alliance (UDA) katika Ikulu ya Nairobi mnamo Julai 15, 2023 walimtaka Rais awajibikie suala hilo.

Dkt Matian’gi alikuwa Waziri wa Usalama wa Ndani katika serikali ya Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, naye Michuki akihudumu katika serikali ya Mwai Kibaki.

Bw Magoha alihudumu katika serikali ya Bw Kenyatta kama Waziri wa Elimu.

Bw Michuki na Prof Magoha kwa sasa ni marehemu.

Wanasiasa hao walitia shaka uwezo wa Waziri wa Usalama wa Ndani katika serikali ya Kenya Kwanza, Prof Kithure Kindiki kuweza kuongea kwa makali, mwito na mvuto sawa na watangulizi wake.

“Ni ukweli kwamba tulijadili suala la jinsi vitengo vyetu vya kiusalama vinaongozwa na pia uwezo ulioko wa kutoa misimamo kupitia maongezi yaliyo na ustadi wa kujiangazia kama tusio na mzaha,” mmoja wa wandani wa Ruto kutoka Kisii akafichulia Taifa Leo Dijitali.

Mbunge huyo alisema kwamba ni kamanda tu wa polisi wa Kaunti ya Nairobi Bw Adamson Bung’ei ambaye amejiangazia kama anayeelewa jinsi ya kutoa misimamo mikali.

“Wengine tulio nao ni kama wanasarakasi. Leo wanatisha hivi na kesho wanakiukwa na hakuna lolote wanafanya. Wengine wanatupa hotuba za wasomi huku ujambazi wa ugaidi, wizi wa mifugo na siasa za uharibifu wa mali ukiendelezwa,” akasema mwingine wa viongozi hao.

Vinara wa walio wengi katika mabunge ya kitaifa na Seneti Mbw Kimani Ichung’wa na Aaron Cheruiyott mtawalia walitoa taarifa ya pamoja wakisema kwamba ni lazima vitengo vya kiusalama viwajibike.

“Huku tukiwaomba wajitume kuzima matukio ya uhuni na mauaji, hata sisi kama viongozi na wafuasi wetu tutakuwa tumejipanga kulinda nyoyo, biashara, nchi na demokrasia yetu dhidi ya wakora wa maandamano,” wakasema katika taarifa ya pamoja.

 

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Wanawake wa kaunti waingie uongozini -Achani

Kamene Goro ashangazwa na matamshi ya mumewe DJ Bonez kuwa...

T L