• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Mnifuinge gerezani ni salama kuliko nyumbani – mshukiwa wa mauaji aambia korti

Mnifuinge gerezani ni salama kuliko nyumbani – mshukiwa wa mauaji aambia korti

NA TITUS OMINDE

MSHUKIWA wa mauaji alishangaza korti alipoambia Mahakama Kuu ya Eldoret kwamba hataki kuachiliwa huru kwa dhamana akisema kuwa anapendelea kuishi gerezani.

Fredrick Cheserek, 31, anayehusishwa na mauaji ya mwanamke aliyepatikana akivuna maembe katika shamba lake, alisema ukosefu wa usalama kijijini kwao katika eneo la Kerio Valley kumemfanya kuogopa kuachiliwa huru.

Cheserek alisikitika kuwa ndugu zake waliuawa na majangili alipokuwa kizuizini hivyo anahofia maisha yake iwapo ataachiliwa kwa dhamana.

Alimwambia Jaji John Wananda kuharakisha usikilizwaji na uamuzi wa kesi yake akisema hataki tena kufuatilia suala la kuachiliwa kwa dhamana.

Mshatakiwa huyo alionyesha kukata tamaa ya kushinda kesi hiyo huku akionyesha imani ya kufungwa badala ya kuachiliwa huru na kisha auawe na majangili.

Kupitia kwa wakili wake Amos Songok, mshukiwa ambaye ni yatima aliambia mahakama kuwa hana mwanafamilia wa kuwa mdhamini wake tangu wazazi wake wauawe kutokana na mashambulizi ya ujambazi katika eneo la Kerio Valley.

“Nilipoteza baba na mama yangu kupitia mashambulizi mabaya ya ujambazi katika eneo lenye hali tete la Kerio Valley na wanafamilia wengine wametoroka eneo hilo kwa ajili ya usalama,” alisema Cheserek.

Alifahamisha mahakama kwamba kutokana na hali tete ya usalama Kerio Valley, hakuna hata mmoja wa wanafamilia yake aliyesalia atafanikiwa kusafiri hadi Eldoret na kuwa mdhamini wake.

Pia aliambia mahakama kwamba anahisi salama zaidi akiwa gerezani kuliko kuwa nje kutokana na ujambazi.

“Ninahisi salama gerezani kuliko nyumbani kwangu kijijini ambako usalama umedorora kutokana na ujambazi,” aliambia mahakama.

Bw Cheserek amekana kumuua Alice Pokot kwa kutumia panga mnamo Desemba 8, 2021 katika kijiji cha Keu, kata ya Keben, Marakwet Mashariki, Kaunti ya Elgeyo Marakwet.

Mshukiwa huyo alikamatwa na kikosi cha polisi wa upelelezi katika maficho yake kuhusiana na mauaji ya marehemu baada ya kumzingira shambani mwake akivuna maembe kwenye gunia.

Inasemekana alikabiliana na marehemu huku akitaka kujua ni kwa nini alikuwa akivuna matunda yake bila idhini yake.

Mshtakiwa alichukua panga na kumlenga marehemu ambaye alizirai na kufariki papo hapo.

Punde tu baada ya tukio hilo, mshtakiwa alienda mafichoni.

Hakimu aliagiza kesi hiyo itajwe Juni 28, atakapopanga tarehe ya kusikilizwa.

 

  • Tags

You can share this post!

Ajabu mama akidai mwanaye alifariki kisha kugeuka jiwe

Wakazi wa Shakahola wataka serikali iwajengee kituo cha...

T L