• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 8:11 PM
Ajabu mama akidai mwanaye alifariki kisha kugeuka jiwe

Ajabu mama akidai mwanaye alifariki kisha kugeuka jiwe

Na BELDINA NYAKEKE (Mwandishi Mwananchi

UGUMU wa maisha umetajwa kuwa sababu ya Amina Rashidi (25), mkazi wa Kijiji cha Mwabuki wilayani Bariadi Mkoa wa Simiyu, kudai kuwa mtoto wake mchanga amefariki dunia na kugeuka kuwa jiwe.

Amina alifikia uamuzi huo baada ya mwanaume aliyempa ujauzito kutaka amzalie mtoto wa kiume, la sivyo asingeweza kumtunza kwani hitaji lake lilikuwa ni mtoto wa kiume na sio wa kike.

Kutokana na hitaji hilo la mwanaume huyo, aliyejulikana kwa jina la Hamisi, mzaliwa wa Mkoa wa Mara na mkazi wa jijini Dar es Salaam, Amina aliendelea kumhakikishia mwanaume huyo kuwa lazima angemzalia mtoto wa kiume.

Machi 17, mwaka huu katika Zahanati ya Kijiji cha Mwabuki, mama huyo alijaaliwa kujifungua mtoto wa kike hivyo kufifisha ndoto zake za kupata huduma kutoka kwa mzazi mwenzie kama alivyoahidiwa.

Baada ya kujifungua mtoto huyo wa kike, mama huyo alitoa taarifa kwa mzazi mwenzie kuwa amejifungua mapacha mmoja wa kike na mwingine wa kiume ambaye alifariki dunia na kugeuka jiwe, hali iliyosababisha kuibuka kwa taharuki kubwa.

Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Musoma Mjini (DC), Dk Halfan Haule aliunda timu ya kufuatilia suala hilo na mwisho wa wiki ametoa taarifa kwa umma akisema, kijana Hamisi alikubali kutoa matumizi ambapo alimtaka mazazi mwenzie kuwapeleka watoto hao nyumbani kwao ili waweze kuwaona.

“Aprili 19, Amina alianza safari ya kuja Musoma ambapo alifika usiku saa 3 na baada ya kupokelewa alidai mtoto mmoja wa kiume amefariki dunia akiwa njiani kuja Musoma,” amesema.

Amesema baada ya mama huyo kutoa tarifa hiyo, mwili wa mtoto uliingizwa ndani na kupelekwa moja kwa moja kwa bibi yake ambaye alikuwa ni mgonjwa ambapo kutokana na kutokuwepo kwa umeme bibi huyo aliomba kupewa simu yenye tochi ili aweze kuona maiti ya mjukuu wake.

“Baada ya kumulika bibi huyo alishtuka kuona jiwe hali ambayo ilizua taharuki na kutokana na hali hiyo Amina aliomba mazishi ya jiwe hilo yafanyike usiku huo jambo ambalo familia halikukubaliana nalo.

“Kesho yake kulizuka taharuki kubwa sana watu wengi walifika katika mtaa wa Mungaranjabo pale Buhare kushuhudia tukio hilo la ajabu na sisi baada ya kupata taarifa tulifika pale kwa hatua zaidi,” amesema.

DC Haule amesema waliamua kufanya uchunguzi huo ili kuepuka mambo ya ajabu ambayo yengeweza kutokea, likiwamo tukio la mwaka 2010 eneo la Mungaranjabo, ambapo watu 17 wa familia moja walifariki dunia kwa kukatwa katwa mapanga kwa imani za kishirikina.

Amesema alilazimika kuunda timu ya watu wanne ikiongozwa na mganga mkuu wa Manispaa ya Musoma kwa ajili ya kuchunguza tukio hilo.

Uchunguzi uliofanywa ulibaini madai hayo hayakuwa ya kweli isipokuwa mama wa mtoto alifanya hivyo ili aweze kupata fedha za matumizi kutoka kwa mzazi mwenzie.

“Kabla hata ya kwenda kule Bariadi tayari tulianza kubaini viashiria vya uongo, kwani tuliomba kadi ya kliniki ya huyo mtoto mwingine hatukuweza kupewa ilibidi kwa haraka haraka tuunde timu ya watu wachache kufuatulia ili kujua ukweli,” amesema

Amesema baada ya kufika kijijini walibaini mama huyo alijifungua mtoto mmoja wa kike taarifa ambazo pia zilithibitishwa na uongozi wa Zahanati kupitia nyaraka mbalimbali ikiwemo rejista ya wanawake waliojifungua kwenye zahanati hiyo Machi 17, mwaka jana.

“Huyu mama alipokuwa akitoka Mwabuki aliwaambia anakwenda Mwanza msibani na baada ya kufikishwa stendi na boda boda kwa ajili ya kupanda basi kabla ya kupanda basi alionekana akiokota jiwe na kuliweka kwenye begi.

“Tumebaini kuwa huyu mama ambaye kwa sasa tunamhifadhi kwa ajili ya usalama wake aliamua kudanganya kujifungua mtoto wa kiume kutokana na ugumu wa maisha, kwani tayari ana watoto watatu ambao kila mmoja ana baba yake lakini inaonekana hawatoi matunzo,” amefafanua.

Amesema kuwa tayari amemuagiza mkurugenzi wa manispaa ya Musoma kufanya taratibu za kumrejesha mama huyo nyumbani kwao Chato mkoani Geita kwa wazazi wake kuepuka madhara yanayoweza kutokea.

Akizungumzia taarifa hizo mama wa Hamisi, Christina Majinge amesema alipata mshtuko mkubwa baada ya kuambiwa mjukuu wake amebadilika na kuwa jiwe.

“Huyu binti alifika hapa usiku saa tatu na ndio mara yangu ya kwanza kumuona na kutuambia mtoto amefariki na kugeuka kuwa jiwe kwa kweli nilipata mshutuko na sikuweza kupata usingizi siku hiyo kwani tangu nizaliwe sijapata kushuhudia tukio kama hilo,” amesema mama huyo ambaye ni mgonjwa kwa zaidi ya miaka mitatu sasa.

Amesema ingawa hadi jana huyo mama pamoja na mtoto wake mchanga hawakuwepo nyumbani kwake, lakini wao kama familia wamemsamehe na kwamba wanampokea mtoto huyo wa kike aliyezaliwa.

Kwa upande wake, Meya wa Manispaa ya Musoma, William Gumbo amesema umefika wakati wanaume watambue kuwa ndio wenye uwezo wa kusabaisha mwanamke kuzaa mtoto wa kiume na sio mwanamke.

“Huyu mama alifikia hatua ya kudanganya kuwa amejifungua mtoto wa kiume wakati uwezo huo yeye hana, tunafundishwa katika Sayansi kuwa mwanaume ndiye ana mbegu ya kike na ya kiume na mwanamke yeye anayo ya kike kwa hiyo kupatikana kwa mtoto wa kiume kunamtegema baba na sio mama,” amesema

  • Tags

You can share this post!

Shamba la MacKenzie Shakahola lenye ukubwa wa ekari 800...

Mnifuinge gerezani ni salama kuliko nyumbani –...

T L