• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
Mwanamke anayedai ni binti ya Mvurya ataka alipiwe karo

Mwanamke anayedai ni binti ya Mvurya ataka alipiwe karo

NA BENSON AMADALA

MWANAMKE mwenye umri wa miaka 29, ameelekea mahakamani akidai ni binti ya Waziri wa Madini na Uchumi wa Baharini, Bw Salim Mvurya, ilhali ametelekezwa.

Kesi hiyo imewasilishwa na Bi Yvonne Anono Omazi, katika Mahakama ya Hakimu Mkuu wa Kakamega.
Kwenye hati za mahakama zilizowasilishwa na wakili wake, Bw Wafula Wawire, mwanamke huyo amedai kuwa, gavana huyo wa zamani wa Kwale ni babake mzazi na amekuwa akimsaidia kwa kiasi hadi alipotimiza umri wa miaka 18.

Mahakama inatarajiwa kutoa mwelekeo wa kesi hiyo baadaye kabla kuweka ya tarehe ya kusikilizwa.
Bi Omazi anatafuta maagizo ya kumshurutisha waziri huyo kutoa usaidizi wa kifedha kwa elimu yake chuoni.

Mwanamke huyo ambaye anaishi na nyanyake mzaa mama eneo la Lubao, Kaunti ya Kakamega, alisema hana njia ya kuchangisha pesa za kujiunga na chuo kikuu baada ya kumaliza masomo yake ya upili.

Katika malalamishi yake, Omazi anaomba mahakama iamue kwamba ana haki ya kupata usaidizi kutoka kwa Bw Mvurya hata baada ya kupitisha umri wa miaka 18, kutokana na hali anayoishi.

Aidha, anaomba amri ya kumtaka mshtakiwa kuwasilisha kiasi kinachofaa cha fedha kwake kama itakavyoamuliwa na mahakama kumudu masomo yake ya chuoni, pamoja na gharama za kesi hiyo.

Bi Omazi amedai kuwa, baada ya kumaliza elimu yake ya sekondari, aliwasiliana na Bw Mvurya ambaye kwa maneno aliahidi kugharamia masomo yake ya chuo kikuu kwa kumlipia karo lakini hajafanya hivyo hadi sasa.

“Mlalamishi anakubali kwamba yeye sasa ni mtu mzima lakini ana thibitisho zaidi ya kudhihirisha hali maalumu zinazohitaji usaidizi kutoka kwa mshtakiwa,” akasema Bi Omazi, kwenye stakabadhi zilizowasilishwa kortini.
“Babangu, mshtakiwa hapa, ni mtu mwenye uwezo ambaye amekuwa gavana wa Kaunti ya Kwale na kwa sasa anahudumu kama Waziri wa Madini, Uchumi wa Baharini na Masuala ya Ubaharia. Kutokana na hayo, nimeonyesha hali maalumu ambazo zinahitaji usaidizi kutoka kwa mshtakiwa ,” akasema Bi Omazi.
Nakala ya cheti cha kuzaliwa kilichoambatanishwa na mlalamishi inaonyesha kuwa, Bi Omazi alizaliwa mnamo Novemba 27, 1994 eneo la Isanjiro, Kaunti Ndogo ya Kakamega Kaskazini. Jina la babake lililo katika cheti cha kuzaliwa ni Salim Mvurya Ngallah.

  • Tags

You can share this post!

Ruto aonya wabunge dhidi ya kupinga Mswada wa Fedha

ODM wamchoka Owalo na misaada yake ya chakula Luo Nyanza

T L