• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 7:53 AM
Ndoa mashakani EACC ikitwaa pesa za mahari

Ndoa mashakani EACC ikitwaa pesa za mahari

NA RICHARD MUNGUTI

MIPANGO ya ndoa ya mhasibu katika mamlaka ya ujenzi wa barabara (KeRRa) imepigwa na dhoruba kali baada ya pesa za mahari kukamatwa na Tume ya Kupambana na Ufisadi Nchini (EACC).

Kufuatia hatua hii ya EACC, Daniel Munywoki Wambua amewasilisha kesi ya dharura katika Mahakama Kuu Milimani akiomba akaunti hiyo yenye Sh21 milioni ifunguliwe tena.

Jaji Esther Maina ameombwa na Wambua aharamishe agizo la kufunga akaunti zake akisema, “EACC imeyumbisha mipango yake kufunga pingu za maisha na kiosha roho.”

Pia ameeleza mahakama EACC inajaribu kukaidi amri ya Mungu kwamba “sio vyema mtu aishi peke yake bali atamuoa mwanamke.”

Mlalamishi huyo anadai EACC imekandamiza haki yake ya kufunga ndoa kinyume cha Kifungu 45 (2) cha Katiba na pia neno la Mungu (Mwanzo 2:18) linalosema: “Mwanaume atamwacha mama yake na baba yake na kuambatana na mke wake.”

Mnamo Agosti 10, 2023, EACC iliwasilisha kesi mbele ya Jaji Esther Maina na kueleza inahofia pesa zilizo katika akaunti ya Wambua katika Benki ya Equity alizipata kwa njia ya ufisadi.

EACC iliomba akaunti tatu za Wambua zifungwe ikiwamo akaunti ya pesa za kulipia mahari iliyokuwa na Sh21 milioni.

Akaunti hiyo kwa jina Daniel Wambui ikiwa na Sh21 milioni, Wambua anasema zilichangwa na kamati ya kupanga ndoa yake pamoja na marafiki 950.

Baada ya EACC kueleza tashwishi hiyo ya EACC, Jaji Maina alifunga akaunti tatu za Wambua katika benki hiyo zikiwa na zaidi ya Sh26 milioni.

Jaji Maina aliamuru akaunti hizo za Wambua zisalie zimefungwa kwa kipindi cha miezo sita EACC ikamilishe uchunguzi.

Lakini Wambua amewasilisha kesi ya dharura kupitia mawakili Danstan Omari na Martina Suiga, akilia hoi na kueleza wasiwasi wake kwamba “huenda akakosa kufunga ndoa na mwanamke ambaye moyo wake unampenda.”

“Ni haki yangu kufunga ndoa kulingana na Kifungu nambari 45 (2) cha Katiba… nifunge pingu za maisha na mwanamke moyo wangu unampenda,” Wambua amesema katika kesi iliyowasilishwa na Omari chini ya sheria za dharura.

Mawakili Omari na Suiga wameeleza mahakama kuu itenge siku ya karibu ya kusikilizwa kwa kesi hiyo badala ya siku ya Februari 2024.

“Wambua anahitaji kuoa. Mipango yake imeyumbishwa na EACC inayokandamiza haki yake ya kufunga ndoa na kipenzi cha moyo wake,” Omari amesisitiza katika cheti cha dharura cha kesi hiyo.

Katika taarifa ya kiapo Wambua amesema kwamba yeye sio mfisadi na kamwe hajashiriki katika uhalifu.

“Mimi ni mhasibu katika KeRRa. Mshahara wangu ni Sh170,000 na ukikatwa kodi na mkopo nasalia na Sh61.207,” Wambua amefichua katika taarifa ya kiapo kortini.

Ameeleza kwamba EACC ilipotosha mahakama ilipoeleza mshahara wake ni Sh55,207.

Pia amefichua EACC ilikuwa na hila mbaya kwa vile ilimficha Jaji Maina kwamba akaunti yake ya Mahari katika Benki ya Equity iko na jina Daniel Wambui na wale sio Daniel Munywoki Wambua kama vile ilivyo katika akaunti zake nyingine mbili.

“Kama EACC ingelieleza Jaji Maina ukweli hangetoa agizo hilo la kufunga akaunti yangu ya mahari,” Wambua akalia hoi.

Wambua anaomba mahakama ifutilie agizo hilo la kufungwa kwa akaunti zake ndipo afunge ndoa.

Mbali na kufanya kazi ya serikali, Wambua ameeleza ni kulima, mfungaji wa mifugo , kuku , nyuki, na biashara ndogo ndogo.

“Mimi sio mfisadi. Nakula jasho langu,” asema Wambua katika afidaviti kwa mahakama.

  • Tags

You can share this post!

DK Kwenye Beat asema hapo kwa wash wash humpati

Wavuvi 200 walifariki kabla ya kuonja fidia ya Lapsset...

T L