• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Ni heri uchaguzi mkuu kupigwa marufuku – PSG

Ni heri uchaguzi mkuu kupigwa marufuku – PSG

NA CHARLES WASONGA

RAIS wa Shirika la kutetea utawala bora na unaozingatia uwajibikaji, Public Service Governance (PSG), Balozi Esther Waringa ametoa wito kubadilishwa mfumo wa uongozi nchini na kupigwa marufuku uchaguzi wa viongozi kupitia uchaguzi mkuu.

Akiwahutubia wanahabari Jumanne, Julai 18, 2023 katika mkahawa mmoja jijini Nairobi, Bi Waringa alipendekeza kusimamishwa kwa serikali ya sasa, upinzani, na vipengele vya Katiba ya Kenya vinavyohimiza uendeshaji wa masuala ya taifa hili kupitia viongozi waliochaguliwa.

“Tunapigia debe kuanzishwa kwa Mfumo wa Utawala wa Huduma kwa Umma ili kuokoa nchi hii kutoka kwa uchaguzi wa kila baada ya miaka mitano ambao ni ghali na huleta migawanyiko, uharibifu na hata maafa,” akasema.

Bi Waringa alisema chini ya mfumo wa Serikali ya Utumishi kwa Umma, shughuli za serikali zitaendeshwa na kusimamiwa na watumishi wa umma katika wizara za serikali kuanzia wakurugenzi wakuu hadi watumishi wa umma wa ngazi za chini.

“Maafisa hawa wataendesha shughuli za utoaji maendeleo na utoaji huduma kama vile za maji, elimu, kilimo, kawi, usalama miongoni mwa nyingine. Maafisa hawa watukuwa wameajiriwa katika wizara za serikali, lakini hawatakuwa wameteuliwa na wanasiasa,” akasema.

Bi Waringa alisema kuwa chini ya utawala anaopendekeza, maafisa watakaouendesha watakuwa ni watu ambao wameteuliwa na jopo maalum kwa kuzingatia uhitimu wao “wala sio miegemeo yao ya kisiasa.”

“Watumishi hawa wa serikali watakuwa wameteuliwa na asasi za kiusalama kama vile Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF), Makamanda wa Usalama na Maafisa wa Utawala wa Mkoa hadi ngazi za machifu na manaibu chifu,” akasema.

Bi Waringa, ambaye alikuwa ameandamana na wakurugenzi wa PSG Sheikh Mohamed Khan na Arvinder Sigh Mehta, alisema kuwa chaguzi kuu ambazo zimeandaliwa nchini tangu uhuru zimeleta madhara ya uongozi nchini kuliko faida.

“Chaguzi zetu huwa zinaleta uharibifu, migawanyiko na ukabila. Kwa hivyo, itakuwa bora ikiwa tutapiga marufuku chaguzi hizi na kuanzisha mfumo mpya wa uongozi unaoendeshwa na maafisa wa umma wasioteuliwa na wanasiasa ambao huchaguliwa katika chaguzi hizi,” akasema.

Bw Waringa alitoa mfano wa ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa 2007 ambazo zilichochewa na mvutano kuhusu matokeo ya uchaguzi wa urais.

“Na maandamano ambayo yameleta maafa katika taifa hili tangu kukamilika kwa uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022 pia yamechochewa na vuta nikuvute kuhusu matokeo ya uchaguzi wa urais. Hii ndio maana nawaomba Wakenya kuunga mkono mfumo huu mpya wa uongozi,” akasema.

Akitetea mfumo huo, Bw Khan alisema mataifa mengi ya Mashariki ya Kati yamestawi kwa sababu ya kukumbatia mfumo wa uongozi usiotegemea chaguzi za viongozi.

“Kenya pia inaweza kupiga hatua kubwa kimaendeleo ikiwa itaongozwa na maafisa wasiochaguliwa katika uchaguzi mkuu,” akaeleza.

PSG imeanzisha kampeni ya ukusanyaji wa saini za Wakenya kuunga mkono mfumo huo mpya wa uongozi.

Kampeni hiyo inajulikana kama ‘Kenya Bila Uchaguzi’.

Bi Waringa anapendekeza kusimamishwa uongozi wa sasa wa serikali ya Kenya Kwanza na mrengo wa upinzani, Azimio la Umoja-One Kenya.

Badala yake anasema utawala wa mpito wa nchi hii utawekwa chini ya Utumishi wa Umma, Idara ya Mahakama na asasi za usalama.

  • Tags

You can share this post!

Hatima ya Junior Starlets kushiriki dimba la CECAFA...

Wanahabari wafukuzwa kikao cha kusikiliza kesi dhidi ya...

T L