• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Wanahabari wafukuzwa kikao cha kusikiliza kesi dhidi ya Obado kikiendelea

Wanahabari wafukuzwa kikao cha kusikiliza kesi dhidi ya Obado kikiendelea

NA RICHARD MUNGUTI

WANAHABARI walifukuzwa katika kesi ya mauaji inayomkabili aliyekuwa Gavana wa Migori Okoth Obado ili dereva wa teksi aliyemwokoa mwanahabari aliyetekwa nyara pamoja na mwanafunzi wa chuo kikuu marehemu Sharon Otieno atoe ushahidi.

Jaji Cecilia Githua aliwaamuru wanahabari watoke kortini kumwezesha Bw Kennedy Kasera kuhojiwa kuhusu nambari ya usajili wa teksi aliyotumia kumpeleka mwanahabari huyo Bw Barrack Oduor wa Nation Media Group katika kituo cha polisi cha Kadel baada ya kutekwa nyara akiwa na Sharon.

Bw Kasera alikataa kujibu maswali kuhusu nambari ya usajili wa gari lake akisema “atahatarisha maisha yake.”

Mawakili wanaomtetea Obado walipinga hatua ya kiongozi wa mashtaka Bi Gikui Gichuhi kukataa Kasera akifichua nambari ya usajili wa gari lake.

“Nilikuwa natazama televisheni ndani ya nyumba yangu niliposikia mtu akiomba afunguliwe mlango  akisema ‘Yauna Uru!’ (Mnifungilie jamani!),” Bw Kasera alimweleza Jaji Githua anayesikiliza kesi ya mauaji dhidi ya Obado na watu wengine wawili.

Bw Kasera alimfungulia mlango kisha Barrack akamweleza jinsi walivyotekwa nyara akiwa na Sharon aliyedai alikuwa ametiwa mimba na Obado.

“Nilimpeleka Barrack katika kituo cha polisi alipodai maisha yake yamo hatarini,” alisema Bw Kasera.

Alitumia gari lake la teksi kumpeleka katika kituo cha polisi.

Alieleza mahakama, “Hata mimi nilihofia maisha yangu ndipo nikampeleka kituoni. Sikutaka akae hata dakika moja kwa nyumba yangu.”

Obado ameshtakiwa pamoja na Michael Oyamo na Casper Obiero kwa mauaji ya Sharon na mtoto wake ambaye hakuwa amezaliwa mnamo Septemba 12, 2018.

Sharon alitekwa nyara kutoka hoteli moja Homa Bay kisha akauawa kinyama katika msitu baada ya kunajisiwa.

Alikuwa na umri wa miaka 26 maisha yake yalipokatizwa.

  • Tags

You can share this post!

Ni heri uchaguzi mkuu kupigwa marufuku – PSG

Jinsi wanafunzi wa Chadwick walivyonogesha tamasha za...

T L