• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 8:55 PM
Hatima ya Junior Starlets kushiriki dimba la CECAFA haijulikani

Hatima ya Junior Starlets kushiriki dimba la CECAFA haijulikani

NA TOTO AREGE

HATIMA ya Kenya kushiriki katika dimba la Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) kwa vijana wa kike wasiozidi umri wa miaka 18, haijulikani kufikia sasa.

Awali, mashindano hayo yalipangwa kuanza Juni 24 jijini Nairobi lakini yakaahirishwa Juni 20, 2023 na kuahirishwa tena Juni 29, 2023 kutokana na sababu za kifedha.

CECAFA kupitia Auka Gecheo ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji alithibitisha Jumatatu wiki hii alitangaza kuwa, michuano hiyo  itachezwa kuanzia Julai 25 hadi Agosti 7 jijini Dar es Salaam, Tanzania.

Haya yalijiri baada ya wanachama wa CECAFA kukutana mjini Abidjan, Cote d’Ivoire wiki iliyopita na kuamua kuwa, michuano hiyo iandaliwe nchini Tanzania katika uwanja wa Chamazi.

Kulingana na Afisa wa Habari na Mawasiliano wa Shirikisho la Soka (FKF) Kenn Okaka, watapeana taarifa kamili kuhusu Junior Starlets kushiriki katika mashindano hayo mwishoni mwa wiki hii.

“Hatuna uhakika ikiwa Kenya itashiriki manake wachezaji hawako kambini tena. Wanafunzi kwa sasa wako shuleni na wanajiandaa kufanya mitihani ya mwisho wa muhula. Wakati uo huo, michezo ya shule za upili inaendelea ambapo wachezaji hao wanashiriki,” alisema Okaka.

Wenyeji Tanzania, Kenya, Ethiopia, Burundi, Rwanda na Zanzibar ni washiriki waliothibitisha kushiriki michuano hiyo hapo awali.

Starlets chini ya mtaalamu Beldine Odemba waliripoti kambini Juni 24, 2023, Nairobi lakini ni wachezaji 30 tu kati ya 44 walioripoti kambini.

 

  • Tags

You can share this post!

Afisa adai baadhi ya wachezaji wa Mathare United walihusika...

Ni heri uchaguzi mkuu kupigwa marufuku – PSG

T L