• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 10:48 AM
Njaa kutesa Wakenya hadi 2024 – Ripoti

Njaa kutesa Wakenya hadi 2024 – Ripoti

NA LEON LIDIGU

BAA la njaa linalohangaisha mamilioni ya Wakenya litaendelea hadi mwaka 2024, ripoti ya Umoja wa Mataifa (UN) imeonya.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa Kenya ni miongoni mwa nchi zilizo na idadi kubwa ya watu wanaoandamwa na makali ya njaa duniani. Nchi nyingine zinazokabiliwa na baa la njaa ni Pakistan, Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR), Ethiopia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Syria.

Ripoti inaonyesha kuwa Wakenya milioni 5.4 sawa na asilimia 32 ya Wakenya, hawana chakula na wanahitaji msaada kwa dharura. Ripoti hiyo inadokeza kuwa mvua ya kutosha inatarajiwa kunyesha katika maeneo mengi ya Kenya hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu wa 2023.

Lakini madhara ya kiangazi cha muda mrefu kilichoshuhudiwa nchini ndani ya miaka mitano iliyopita, ni makubwa mno. Chakula kitakachozalishwa mwaka huu wa 2023 hakitatosha.

“Madhara yaliyosababishwa na kiangazi hicho ni makubwa na itachukua miaka mingi kwa Kenya kuwa na chakula cha kutosheleza,” inasema ripoti.

Umoja wa Mataifa umehimiza wahisani wa kimataifa kuingilia kati na kutoa msaada kwa nchi zilizoathiriwa na njaa, ikiwemo Kenya. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, uchumi Kenya na nchi nyinginezo utatatizika mwaka huu, hivyo kuongezea raia mahangaiko.

“Kudorora kwa sarafu ya Kenya dhidi ya Dola ya Amerika na bei ya juu ya bidhaa kunasababisha maisha kuendelea kuwa magumu,” inasema ripoti hiyo.

UN imetoa ripoti hiyo huku mjadala kuhusu Mswada wa Fedha wa 2023 unaopendekeza kuongezwa kwa ushuru wa bidhaa mbalimbali ukiendelea kuchacha nchini.

Jana Jumatatu, washiriki kutoka vyama vya wafanyakazi wa vyuo vikuu, madaktari, walimu na wafanyakazi wengineo waliandamana hadi katika majengo ya Bunge kupinga pendekezo la serikali kutaka kukata asilimia 3 ya mishahara ya wafanyakazi ili kufadhili mradi wa ujenzi wa nyumba nafuu. Mswada huo pia unapendekeza nyongeza ya ushuru wa mafuta.

  • Tags

You can share this post!

Haaland alivyoweka rekodi kwa kuibuka Mchezaji Bora na...

Atwoli atengwa vyama vikipinga mswada wa Ruto

T L