• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 10:50 AM
Omtatah: Sheria ya Fedha 2023 imejaa ufisadi

Omtatah: Sheria ya Fedha 2023 imejaa ufisadi

NA RICHARD MUNGUTI

SENETA wa Busia Okiya Omtatah ameirarua Sheria ya Fedha 2023 kwa kuanika wazi sehemu 22 za sheria hiyo zilizopenyezwa na kupitishwa na Bunge kabla ya kujadiliwa na umma huku Serikali ikitetea na kuomba kesi 12 zinazoipinga zitupiliwe mbali.

Bw Omtatah aliwaomba majaji David Majanja, Christine Meoli na Lawrence Mugambi waharamishe sheria hiyo na kuwaokoa Wakenya.Akifafanua sehemu baada ya nyingine, Bw Omutatah alisema “Bunge lilikosea kuwabebesha Wakenya mzigo wa kugharimia bajeti ya Sh3.6trilioni kwa njia ya ujanja na uhuni.”

Alisema mswada wa bajeti hiyo haikupelekwa katika Bunge la Seneti kupata uungwaji mkono kabla ya kupitishwa na Bunge la Kitaifa.Seneta huyo alisema Wakenya watatozwa Sh211bilioni kinyume cha sheria.

Mwanasiasa huyo alifichua sehemu 22 kati ya sehemu 84 za Sheria ya Fedha 2023 ambazo hazikujadiliwa na uuma kutoa maoni yao.

“Ikiwa sehemu 22 zilipenyezwa wakati wa kusomwa kwa mara ya tatu kwa mswada wa fedha bungeni, basi sheria yote iko na kasoro, iharamishwe,” Bw Omtatah alifafanua huku akiwasihi majaji hao “wawaokoe Wakenya.”

Omtatah alisema kutokana na makosa hayo ya Bunge, sasa Wakenya watalazimika kuchanga Sh1.2 trilioni za kulipia madeni ambayo yangeepukwa.

Alisema sasa imebidi Waziri wa Fedha akope pesa kugharimia bajeti hiyo ya Sh3.6trilioni.

Seneta huyo alisema ufisadi mwingi umesheheni katika Sheria ya Fedha 2023 kutokana na ujanja wa kuingizwa kwa sehemu 22 kati ya 84 za sheria hiyo ya kutafuta fedha za kuendesha shughuli za Serikali ya Rais William Ruto.

Bw Omtatah alisema wakenya wanatozwa kodi ya nyumba ya asili mia tatu kimakosa.

 

  • Tags

You can share this post!

Muheria asema bei za mafuta zinalemea masikini  

Magaidi wawili wa Al-Shabaab wauawa na maafisa wa KDF...

T L