• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Magaidi wawili wa Al-Shabaab wauawa na maafisa wa KDF msituni Boni

Magaidi wawili wa Al-Shabaab wauawa na maafisa wa KDF msituni Boni

NA KALUME KAZUNGU

MAAFISA wa Jeshi la Ulinzi Kenya (KDF) wamewaua magaidi wawili wa Al-Shabaab baada ya kuvamia maficho yao eneo la Bodhei, msitu wa Boni, Kaunti ya Lamu.

Wakizungumza na Taifa Jumapili na kuomba kutotajwa majina yao, maafisa wanaohusika na operesheni ya kuwasaka Al-Shabaab msitu wa Boni (OAB) walithibitisha kuuawa kwa wawili hao wakisema wengine wengi walitoroka na majeraha makali ya risasi.

Silaha kadhaa za Al-Shabaab, ikiwemo bunduki aina ya AK47, maganda na risasi, vifaa vya kurushia gruneti ya mbali (RPG) miongoni mwa nyingine zilinaswa kwenye uvamizi huo.

Duru za walinda usalama pia ziliarifu kuwa uvamizi huo wa maficho ya Al-Shabaab ulitekelezwa kufuatia taarifa zilizotolewa awali za kijasusi kwamba magaidi walikuwa wameonekana sehemu fulani ya eneo hilo la Bodhei ambalo liko ndani ya msitu mkuu wa Boni.

“Kufuatia taarifa hizo za kijasusi, KDF walivamia maficho mawili ya Al-Shabaab eneo la Bodhei kaunti ya Lamu, ambapo makabiliano makali kati ya Al-Shabaab na walinda usalama yalizuka. Magaidi walishindwa nguvu, ambapo kadhaa waliuawa ilhali wengine wengi wakitokomea msituni na majeraha mabaya. Silaha hatari pia zilinaswa kwenye mahandaki yao. Operesheni ya kuwasaka wahalifu bado inaendelea Bodhei na viungani mwake,” akasema mmoja wa maafisa wanaohusika na operesheni hiyo.

Tangu Septemba 2015, serikali kuu imekuwa ikiendeleza operesheni ya usalama msitu wa Boni, madhumuni makuu yakiwa ni kuwanasa au kuwamaliza magaidi wa Al-Shabaab wanaoaminika kujificha ndani ya msitu huo wa Boni.

Kuuawa kwa magaidi hao wa Al-Shabaab mara kwa mara ndani ya msitu wa Boni ni dhihirisho tosha kwamba operesheni inayoendelea ya kiusalama inazaa matunda si haba.

Mbali na wawili waliouawa Jumapili, kuna wengine watano ambao pia waliuawa na walinda usalama siku tano zilizopita katika eneo la Harbole-Fafi, kaunti ya Garissa.

Makumi ya magaidi pia walitoroka wakiwa na majeraha mabaya ya risasi.

Uvamizi na mauaji ya watano hao ulitekelezwa na maafisa wa usalama wa kitengo maalum (SOG) baada ya kupokea ripoti za kijajusi kuhusu kuwepo kwa maficho ya Al-Shabaab eneo husika.

Silaha kadhaa ikiwemo bunduki, risasi, maganda ya risasi, vifaa vya kutengenezea vilipuzi, dawa za matibabu na vinginevyo pia vilinaswa kwenye uvamizi huo.

Walinda usalama pia walinasa mkongojo uliokuwa na maandishi, ikiwemo majina ya makamanda na watu wenye vyeo vikuu katika kundi hilo la kigaidi la Al-Shabaab.

Jumapili wiki iliyopita, washukiwa wa Al-Shabaab waliua na kujeruhi maafisa kadhaa wa KDF baada ya kutega gari walimokuwa wakisafiria walinda usalama hao kwa vilipuzi vya kutegwa ardhini eneo la Bodhei-Majengo, kwenye barabara ya Milimani-Baure, msitu wa Boni, kaunti ya Lamu.

Februari m2023, KDF waliua magaidi watatu wa Al-Shabaab eneo la Sarira, kaunti ya Lamu.

Eneo la Sarira liko karibu na mpaka wa Kenya na Somalia.

Mnamo Februari 2022, KDF wanaoendeleza operesheni ya Usalama Ndani ya Msitu wa Boni waliwaua magaidi wanne wa Al-Shabaab kwenye eneo hilo hilo la Sarira.

Julai 2022, KDF pia waliwaangamiza magaidi 10 wa Al-Shabaab wakati wa operesheni maalum ya kiusalama iliyotekelezwa kati ya Sarira na Kolbio, ndani ya msitu wa Boni, karibu na mpaka wa Lamu na Somalia.

Silaha mbalimbali za Al-Shabaab zilinaswa kwenye uvamizi huo ilhali makumi ya magaidi hao wakitorokea msituni wakiwa na majeraha makali ya risasi.

  • Tags

You can share this post!

Omtatah: Sheria ya Fedha 2023 imejaa ufisadi

Samidoh adai alitaka kuwa wakili, akifichua alama zake za...

T L