• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 8:50 AM
Rosa Buyu: Marufuku ya muda kwa wabunge wa Azimio ni njama kupitisha Mswada wa Fedha 2023  

Rosa Buyu: Marufuku ya muda kwa wabunge wa Azimio ni njama kupitisha Mswada wa Fedha 2023  

NA SAMMY WAWERU

MBUNGE wa Kisumu Magharibi Rosa Buyu, ametaja marufuku ya muda bungeni kwa baadhi ya wabunge wa Azimio kama njama ya serikali kuhakikisha Mswada tata wa Fedha 2023 unapitishwa.

Bi Rosa alisema Alhamisi, Juni 8, 2023 baada ya wabunge kadha wa upinzani kufurushwa bungeni na spika Moses Wetangula, ni mahesabu kupunguza idadi ya wabunge wanaopinga mswada huo.

Kadha walipewa marufuku ya majuma mawili, na wengine siku tano kufuatia vurugu zilizozuka kati ya wabunge wa Azimio la Umoja-One Kenya na Kenya Kwanza, Azimio ikishikiniza kubanduliwa kwa mbunge maalum Sabina Chege kama naibu kiranja wa wachache bungeni.

“Hii ni njama ya serikali ya Kenya Kwanza kuhakikisha idadi ya wabunge wanaopinga Mswada wa Fedha 2023 inapungua, ili upitishwe,” Bi Rosa alisema.

Mwanasiasa huyo ambaye amewahi kuhudumu kama mbunge mwakilishi wa wanawake Kisumu, ni miongoni mwa wabunge 7 ambao spika Wetangula aliwapa marufuku ya wiki mbili na siku tano, mtawalia.

Wengine ni Bi Millie Odhiambo (Suba Kaskazini), TJ Kajwanga wa Ruaraka, Catherine Omanyo (Busia), Joyce Kamene (Machakos), Amina Mnyazi wa Malindi, na Sabina Chege mwenyewe.

Bw Wetangula alisusia kumbandua Bi Sabina, akihoji “nimefungwa mikono na amri ya korti”.

Jubilee ilimfurusha mbunge huyo maalum kama kiongozi wa chama.

Upinzani, unaoongozwa na kinara wa Azimio, Raila Odinga umeapa kutumia mbinu zote kuangushwa Mswada wa Fedha 2023 unaopendekeza nyongeza ya ushuru (VAT), ikiwemo ya mafuta na asilimia 3 ya mshahara wa kila mfanyakazi kukatwa kwa minajili ya mpango wa ujenzi wa nyumba za bei nafuu.

Wengi wa Wakenya, mashirika na vyama kutetea wafanyakazi wanapinga mswada huo unaotarajiwa kuwasilishwa bungeni kujadiliwa kupitishwa au kuangushwa kabla Makadirio ya Bajeti 2023/24 kusomwa.

  • Tags

You can share this post!

NiE: Mkataba wa NMG na KIWASCO unavyopiga jeki elimu Kisumu

Gor, Tusker na Homeboyz taabani kwa kukosa timu za wanawake

T L