• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 6:24 PM
Mashujaa Dei: Ruto ‘apuliza vuvuzela’ Wakenya watambue mfumo wa ‘bottom-up’

Mashujaa Dei: Ruto ‘apuliza vuvuzela’ Wakenya watambue mfumo wa ‘bottom-up’

Na SAMMY WAWERU

NAIBU Rais William Ruto ameendeleza siasa za kuuvumisha mfumo wa kukwamua uchumi wa ‘bottom-up’ ili kupiga jeki azma yake ya kuwania urais kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.

Akihutubu katika sherehe za kuadhimisha Sikukuu ya Mashujaa 2021 zilizofanyika Kaunti ya Kirinyaga, Jumatano, Dkt Ruto alisema mfumo huo utasaidia kupeleka Kenya mbele kimaendeleo.

Naibu wa Rais akionekana kuahidi kuendeleza sera za Rais Uhuru Kenyatta, alisema ajenda za Rais na mfumo wake, kwa pamoja zitaboresha uchumi.

“Uongozi na rekodi yako bora ya utendakazi itaongoza watakaokufuata (akimaanisha warithi wa Rais),” Ruto akasema.

Kufuatia salamu za mapatano kati ya Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga Machi 2018, almaarufu Handisheki, Naibu wa Rais amekuwa akilalamikia kupokonywa majukumu yake akidai yametwaliwa na Waziri wa Usalama wa Ndani na Mikakati ya Serikali, Dkt Fred Matiang’i.

Licha ya kukosoa serikali tawala ya Jubilee aliyomo, Dkt Ruto amekuwa akitumia miradi ya maendeleo iliyotekelezwa kufanya kampeni kumrithi Rais Kenyatta 2022.

Wakati wa maadhimisho ya Mashujaa Dei yaliyofanyika katika uwanja wa Wang’uru, Dkt Ruto alisema yeye pamoja na wapinzani wake wataendeleza sera na ajenda za Rais Kenyatta.

“Wewe ni shujaa wetu na pamoja na wapinzani wangu, miradi ya maendeleo uliyoanzisha tutaiendeleza. Nimekuwa naibu wako kwa muda wa miaka tisa sasa, na ajenda zako pamoja na mfumo wa ‘bottom-up’ utapeleka taifa hili mbele kimaendeleo,” akasema.

Rais Kenyatta ameongoza taifa katika kuadhimisha siku hii muhimu, na ambayo inalenga kukumbuka mashujaa waliopigania uhuru wa Kenya na Wakenya waliochangia kuboresha nchi.

Bw Odinga, kiongozi wa ANC, Musalia Mudavadi, Moses Wetangula (Ford-Kenya), Gideon Moi (Kanu), ni miongoni mwa viongozi na wanasiasa mashuhuri waliohudhuria.

Rais wa Malawi Lazaru Chakwera amehudhuria kama mgeni mashuhuri.

You can share this post!

Zidane, Conte kati ya wakufunzi wa haiba wanaohusishwa na...

Mawaziri wamng’ang’ania Raila shereheni

T L