• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
UDA Mlima Kenya wadai vyeo vya juu

UDA Mlima Kenya wadai vyeo vya juu

NA COLLINS OMULO

NJAMA ya eneo la Mlima Kenya kutaka chama cha United Democratic Alliance (UDA) kuwa na naibu kiongozi mmoja na eneo hilo kumezea mate wadhifa wa katibu mkuu imezua dhoruba ndani ya chama tawala.

Vita vipya vya ubabe wa kisiasa sasa vinatishia uchaguzi wa mashinani wa chama hicho kinachoongozwa na Rais William Ruto unaopangwa mwezi ujao, huku kukiwa na mvutano mkali wa kikanda.

Wabunge wa Magharibi wanashinikiza kupanuliwa kwa muundo wa chama kiwe na naibu viongozi wawili huku Kiranja wa Wengi katika Seneti Boni Khalwale akipendekezwa kuwa mmoja wao.

Hata hivyo, wenzao wa Mlima Kenya wamepinga mpangilio huo na sasa wanataka kugombania wadhifa wa katibu mkuu, ambao kwa sasa unashikiliwa na aliyekuwa Seneta wa Kakamega Cleophas Malala anayetoka Magharibi huku Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro akipendekezwa.

Wabunge wengi wa Mlima Kenya sasa wanadai mpango wa kuwa na zaidi ya naibu mmoja wa kiongozi wa chama ni sehemu ya mpango mpana wa kisiasa unaolenga kupunguza ushawishi wa Naibu Rais Rigathi Gachagua katika siasa za urithi kwenye uchaguzi wa 2032.

Haya yanajiri baada ya Bw Khalwale kuanzisha dhoruba katika chama tawala kwa kumuonya Bw Gachagua ajiandae kuona eneo la Magharibi likitawala Ikulu, muhula wa Rais Ruto utakapokamilika 2032 endapo atachaguliwa tena.

Seneta huyo wa Kakamega alionya kuwa, hakuna mtu katika ngazi ya kitaifa na kaunti atakayetumia watu wa Magharibi ya Kenya kabla na katika uchaguzi wa 2032.

“Naibu Rais anapaswa kunisikiliza na apende asipende, 2032 ni wakati wa urais wa Waluhya,” akasema Dkt Khalwale.

Huku kukiwa na hali ya wasiwasi katika nchi nzima chini ya mwezi mmoja kabla ya uchaguzi wa chama, Dkt Khalwale alimshutumu Bw Gachagua kwa kuwapandikiza viongozi aliowataja kuwa ‘wavulana wadogo’ katika maeneo tofauti huku akijinadi kumrithi Rais Ruto.

“Huko Mombasa, amepanda Omar Hassan, Magharibi, ana Malala na kuna wengine kadhaa katika maeneo mengine kuwazima wanasiasa wakuu katika maeneo ili wazee wasivuruge azima yake ya urais. Lakini narudia kusema apende asipende, 2032 ni wakati wa urais wa Waluhya,” alisema.

Jumapili, viongozi wa Mlima Kenya walisema hawataruhusu muundo wa chama ambao utakuwa na zaidi ya naibu mmoja wa kiongozi wa chama. Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga alisema nafasi hiyo inafaa kutengewa Bw Gachagua huku akitaka nafasi ya katibu mkuu ipewe kiongozi kutoka eneo hilo.

“Lazima kuwe na kiongozi wa chama na naibu kiongozi wa chama. Wengine wanaweza kuwa chochote wanachotaka kuwa na tunadai hivyo kama wanachama wa UDA,” akasema Bw Kahiga.

Wadhifa huo kwa sasa unashikiliwa na Bw Gachagua, hata hivyo, kuna ripoti chama hicho kinanuia kuanzisha nafasi nyingine ya naibu kiongozi kuhakikisha usawa wa kieneo.

“Tuna kiongozi mmoja wa chama na ni muhimu pia tuwe na naibu kiongozi mmoja wa chama,” alisema Seneta wa Nyeri Wahome Wamatinga.

Alisema katiba ya chama hairuhusu manaibu wawili wa chama kwa kuwa hii itasababisha kuundwa kwa vituo vingi vya mamlaka ambavyo vitasababisha migogoro ya kisiasa.

Seneta wa Kirinyaga James Murango alisema hakuna haja ya kupanua muundo wa chama ili kuwa na viongozi zaidi wa kanda wakati UDA tayari ina mwonekano wa kitaifa.

  • Tags

You can share this post!

Polo atoweka kazini ghafla kukwepa bosi wa kumtupia mistari...

Wavuvi Pwani wapokea mafunzo kukabidhiwa vibali wakome...

T L