• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 9:50 AM
Uhuru alivyofaulu kukwepa ‘mtego’ wa polisi Karen

Uhuru alivyofaulu kukwepa ‘mtego’ wa polisi Karen

NA WANDERI KAMAU

IMEBAINIKA kuwa maagizo ya haraka aliyotoa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta kwa mwanawe, Jomo Kenyatta, ndiyo yaliyowazuia watu waliofika katika makazi yake Ijumaa “kutafuta silaha” kutofanikiwa kuingia.

Bw Kenyatta alifichua kwamba alimwagiza mwanawe kutowafungulia wala kuwaruhusu watu hao kuingia katika makazi yake, mtaani Karen, jijini Nairobi, kwani kuna utaratibu maalum ambao polisi huwa wanafuata wanapotaka kufanya msako katika nyumba ya mtu yeyote.

“Nilimwambia mwanangu kutowaruhusu watu hao kuingia kwani kwanza, magari yao hayakuwa na nambari za usajili za serikali. Kwa kawaida, lazima polisi wamfahamishe mtu wanapotaka kutafuta chochote nyumbani mwake. Pili, lazima magari yao yawe na nambari za usajili za serikali,” akasema Bw Kenyatta, kwenye mahojiano na wanahabari nje ya makazi hayo Ijumaa usiku.

Bw Kenyatta alisema watu hao, ambao walijitambulisha kama polisi, walikuwa na magari yaliyokuwa na nambari za usajili za nchi ya Sudan Kusini.

“Ni polisi gani ambao huwa wanasafiri kwa magari ambayo hayana nambari za usajili za Kenya? Mbona walikosa kujitambulisha inavyofaa?” akashangaa Bw Kenyatta, akisema kuwa hilo ndilo lilimfanya kufika katika makazi ya mwanawe haraka mara tu baada yake kumwambia hayo.

“Ninajua polisi wanavyofanya kazi. Niliacha kazi yangu niliyokuwa nikifanya afisini na kuelekea kwake mara moja,” akaongeza.

Baada ya Bw Kenyatta kutoa kauli hiyo, Waziri wa Usalama wa Ndani, Prof Kithure Kindiki, alitoa taarifa akieleza kuwa polisi wamebaini baadhi ya silaha ambazo zimekuwa zikitumika wakati wa maandamano ya mrengo wa Azimio la Umoja zimekuwa zikitolewa na raia wanaomiliki bunduki.

Bila kutoa ithibati yoyote, Prof Kindiki alisema kuwa uchunguzi wa polisi umebaini makazi matatu katika mtaa wa Karen ndiyo yamekuwa yakitumika “kusambaza silaha hizo”.

“Mnamo Julai 19, mshukiwa mkuu alikamatwa na polisi akijitayarisha kusambaza kasha kubwa la silaha kwa wahalifu ili kutumika kuendeleza ukatili wakati wa maandamano. Mshukiwa huyo alinaswa akiwa na sime 14, mapanga 24, rungu 46 na pakiti zaidi ya 300 ya dawa tofauti za kulevya,” akasema Prof Kindiki.

Pia, alisema polisi walimpata mshukiwa huyo na Sh42 milioni, na stakabadhi zilizoeleza utaratibu ambao ungetumika kusambaza fedha hizo katika jumla ya kauti 11 katika maeneo ya Nairobi, Kati na Bonde la Ufa.

Serikali ya Kenya Kwanza imekuwa ikidai kuwa Bw Kenyatta na familia yake ndio wamekuwa wakifadhili maandamano ambayo yamekuwa yakiongozwa na kiongozi wa Azimio la Umoja, Bw Raila Odinga.

Hata hivyo, Bw Kenyatta alijitetea vikali, akisema urafiki baina yake na Bw Odinga hauna uhusiano wowote na maandamano hayo.

Akiwa mwenye ghadhabu, alimwambia Rais William Ruto kumkabili yeye binafsi, badala ya kuwahangaisha watoto wake au mamake, Mama Ngina Kenyatta.

 

  • Tags

You can share this post!

Sukari: Kamati yaambiwa wabunge 2 walipelelezwa na DCI

Wandayi, Cherargei wakorogana kuhusu utendakazi wa polisi

T L