• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 7:50 AM
Wabunge wa Azimio Magharibi wawashutumu Kuria na Ndii

Wabunge wa Azimio Magharibi wawashutumu Kuria na Ndii

NA SHABAN MAKOKHA

BAADHI ya wabunge wa Upinzani kutoka Magharibi mwa nchi sasa wanamtaka Waziri wa Biashara Moses Kuria na Mshauri wa Kiuchumi wa Rais William Ruto, David Ndii wawaombe Wakenya msamaha kwa matamshi tatanishi waliyoyatoa kuhusu kupanda kwa bei ya mafuta.

Wakati huo huo, viongozi hao pia walimshutumu Seneta wa Nandi Samson Cherargei na wanasiasa kadhaa kwa kupendekeza kuwa muhula wa rais uongezwe kutoka miaka mitano hadi miaka saba.

Mbunge wa Matungu Peter Nabulindo na mwenzake wa Mumias Mashariki Peter Salasya pia wamemtaka Kinara wa Upinzani Raila Odinga, awaondoe wanachama wa Azimio kwenye Kamati ya Kitaifa ya Mazungumzo yenye wanachama 10.

Wanasema viongozi wa Kenya Kwanza hawamakinikii mazungumzo hayo yanayostahili kusuluhisha changamoto ambazo zinawakabili Wakenya.

Bw Kuria na Dkt Ndii walikashifiwa kwa kutoa matamshi yaliyoonekana kuwakejeli Wakenya kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta.

“Ukiendelea kulalamika kuwa bei ya mafuta imepanda, kwa nini usichimbe tu kisima chako,” akasema Bw Kuria baada ya tangazo kutolewa kuhusu kupanda kwa bei ya mafuta, huku akisisitiza kuwa bei ya bidhaa hiyo itaendelea kupanda hadi Februari 2024.

Aidha, Bw Nabulindo aliwataka wanachama wa Azimio wajiondoe kwenye mazungumzo hayo iwapo wenzao wa Kenya Kwanza wataidhinisha pendekezo la Bw Cherargei.

Alikuwa akizungumza eneobunge lake mnamo Jumamosi, Septemba 23, 2023.

Bw Salasya naye aliwataka Wakenya wafunge mikanda na kupambana na maisha magumu kwa sababu huenda hali haitabadilika hivi karibuni.

Aliwataka wanasiasa nao wakome kutoa matamshi ya kuwakejeli Wakenya.

“Mwanaume mwenye njaa ana hasira nyingi. Baadhi ya matamshi ya viongozi wa Kenya Kwanza yanakejeli maisha magumu ambayo Wakenya wanapitia. Kuria na Ndii wanastahili kuwaomba Wakenya msamaha na hatutaruhusu matamshi hayo yatolewe kwa sababu yatazamisha Kenya kwenye ghasia,” akasema Bw Salasya.

Mwanasiasa huyo alisema kuwa viongozi wanastahili kuwapa Wakenya matumaini, nayo serikali iweke mikakati ya kuhakikisha taifa linajikwamua kiuchumi.

 

  • Tags

You can share this post!

Kajala awakataa wanaume wa Kenya kwa kumchezea...

Historia Kipchoge akitawala Berlin Marathon mara ya 5  

T L