• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 2:59 PM
Mbinu za mrengo wa ‘Tangatanga’ kuchelewesha mswada tata wa marekebisho ya sheria za vyama

Mbinu za mrengo wa ‘Tangatanga’ kuchelewesha mswada tata wa marekebisho ya sheria za vyama

Na CHARLES WASONGA

SHUGHULI ya upigaji kura kwa marekebisho kadha yaliyopendekezwa kwenye Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Kisiasa ilihujumiwa na wabunge wandani wa Naibu Rais William Ruto.

Wabunge hao walitumia mbinu mbalimbali za kuchelewesha shughuli za utengenezaji sheria, hali iliyosababisha kikao maalum cha Jumatano kuahirishwa saa sita za usiku.

Kufikia wakati huo, wabunge walikuwa wamekamilisha hoja nne pekee za marekebisho kwa mswada huo kati ya jumla ya marekebisho 23 yaliyopendekezwa na wabunge; wengi wao wakiwa ni wandani wa Dkt Ruto.

Wabunge wa mrengo wa ‘Tangatanga’ wanaoegemea chama cha United Democratic Alliance (UDA), walihujumu upigaji kura kwa mtindo wa sauti za “Ndio” na “La”.

Hii ililazimisha wenyeviti wenza wa kikao cha Jumatano kukumbatia mtindo wa upigaji kura wa moja kwa moja.

Mbunge wa Garissa Mjini Aden Duale ndiye alikuwa wa kwanza kupendekeza upigaji wa kura kwa njia ya moja kwa moja badala ya kura ya sauti.

“Ni wazi kuwa hiki ni kikao maalum na kinaweza kuendelea hadi usiku wa manane. Mtindo wa kuita majina moja kwa moja ndio wa haki na tunapaswa kuutumia; hatuna haraka,” akasema.

Chini ya mtindo huo, wabunge walitumia muda wa karibu saa moja na nusu kupiga kura kwa hoja mbalimbali za marekebisho. Hii ni kwa sababu wengi wa wabunge wa ‘Tangatanga’ walishiriki sarakasi mbalimbali kwa kutoa hotuba ndefu walipopewa kipaza sauti wapige kura badala ya kusema “Ndio” au “La”.

Kwa mfano, mbunge wa Bahati Kimani Ngunjiri alimwambia spika wa muda Soipan Tuya hivi: “Mheshimiwa Bi mwenyekiti, ningependa kukujulisha kwamba mmoja wetu yuko hospitalini akifanyiwa upasuaji kwenye jicho. Ni jambo la kuhuzunisha na sasa ninaita wabunge wote wa UDA wasimame tuombe.”

Bw Ngunjiri alisema hayo alipopewa nafasi ya kupiga kura. Alipiga kura yake baada ya kukamilisha taarifa yake na maombi ambayo yalidumu kwa dakika 15.

Mbunge huyo alikuwa akipigia kura hoja iliyowasilishwa na Mbunge wa Kandara Alice Wahome kwamba sehemu ya mswada huo unaopendekeza kubuniwa kwa chama cha kisiasa cha muungano, kiondolewe.

Mbunge wa Kandara Alice Wahome. PICHA | MAKTABA

Baadhi ya wabunge wa ‘Tangatanga’ kama vile Benjamin Washiali (Mumias Mashariki), Gathoni wa Muchomba (Mbunge Mwakilishi wa Kiambu) na Dan Wanyama (Webuye Mashariki) na Ndindi Nyoro (Kiharu) walitumia nafasi zao za kupiga kura kutoa kauli za kusifia chama cha UDA na ndoto za Dkt Ruto za kuwania urais.

“Kwa niaba ya familia ya UDA, chama kikubwa zaidi nchini na vuguvugu la Hustler Nation na nikipinga utekaji wa taifa hili na watu wachache wenye nia ya kuchochea ghasia, ninapiga kura ya ndio kwa marekebisho yaliyopendekezwa na mwenzetu Alice Wahome,” akasema Bw Nyoro.

Wabunge wengine wa mrengo wa Dkt Ruto walitumia nafasi hiyo kuvumisha azma zao za kuwania nyadhifa mbalimbali huku wakiwakashifu wenzao wa mrengo wa Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga.

“Kwa niaba ya watu wa eneobunge la Soy ninakowakilisha na watu wa kaunti ya Uasin Gishu kwa ujumla na kama gavana wa Uasin Gishu mwaka ujao ninapiga kura ya ndio,” akasema Mbunge wa Soy Caleb Kositany.

Naye Mbunge Maalum David Sankok alitumia nafasi yake ya kupigia kura hoja mbalimbali za marekebisho kwa mswada huo kwa kutoa matamshi ya kudunisha Bw Odinga na vuguvugu lake la Azimio la Umoja.

Vile vile, nyakati fulani mbunge huyo anayewakilisha jamii ya walemavu nchini, alitoa kauli kadha kwa lugha yake ya Kimaasai, hali iliyochangia spika wa muda Bi Soipan kumwonya.

“Kwa niaba ya jumla ya watu 6.5 milioni wanaoishi na ulemavu nchini na kwa lengo la kutukinga dhidi ya azimio la fujo, wakora na waganga ndani na nje ya bunge hili, ninapiga kura ya ndio!” akafoka Bw Sankok.

Awali, wabunge walirushiana makonde wakati wa awamu ya kwanza ya upigaji kura kuhusu hoja hiyo ya Bi Wahome.

Spika wa muda wakati huo, Chris Omulele, alisitisha shughuli kwa muda wa dakika 15 ili kutuliza hali huku wabunge wa ‘Tangatanga’ wakimhimiza aahirishe kikao hicho.

Vurugu hizo zilichangia kufurushwa kwa kiongozi wa wachache John Mbadi kutoka bungeni kwa madai kuwa alitwanga makonde Mbunge wa Sigowet/Soin Benard Kipsengeret Koros na kumjeruhi uso.

“Bw Mbadi unaamriwa kuondoka bungeni kwa kosa la kuzua vurugu na utovu wa nidhamu. Umezimwa kuhudhuria vikao vya bunge hili kwa siku tano,” akaamuru Bw Omulele ambaye ni Mbunge wa Luanda.

Hatimaye wabunge walipopigia kura hoja hiyo ya Bi Wahome, wabunge wa mrengo wa handisheki waliwashinda wenzao wa ‘Tangatanga’ kwa kura 158 dhidi ya kura 134.

Hii iliashirikia kuwa juhudi za Bi Wahome na wenzake wandani wa Dkt Ruto za kutaka kufutiliwa mbali kwa sehemu ya sita ya mswada huo inayopendekeza kubuniwe chama cha muungano, ziligonga mwamba.

Hata hivyo, kufikia saa sita za usiku kuashiria kuanza kwa Alhamisi, wabunge walikuwa wameshughulikia na kupigia kura hoja nne pekee za marekebisho ya mswada huo kati ya hoja 23 zilizoratibiwa.

Kiongozi wa wengi Amos Kimunya aliahidi kuitisha kikao kingine maalum cha bunge la kitaifa muhsusi kukamilisha mswada huo ambao ulikuwa katika hatua yake ya tatu na ya mwisho.

You can share this post!

Waheshimiwa bila heshima

CHAKULA CHA UBONGO: Uchangamfu ni kiambata muhimu katika...

T L